Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday, 13 March 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1 Wafalme 7...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana
Tumshukuru Mungu katika yote...

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyo onekana
Mungu mwenye nguvu,Mungu wa wote walio hai,Mungu  wa Abrahamu,
Isaka na Yakobo,Baba wa Upendo,Baba wa Baraka,Mungu mwenye huruma
Baba mwenye kusamehe,Baba wa yatima,Mume wa wajane,Muweza
wa yote,Alfa na Omega...!!


Yesu alipomaliza kuwapa wanafunzi kumi na wawili maagizo, alitoka hapo, akaenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao. Yohane Mbatizaji akiwa gerezani alipata habari juu ya matendo ya Kristo. Basi, Yohane akawatuma wanafunzi wake, wamwulize: “Je, wewe ni yule anayekuja, au tumngoje mwingine?” Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie Yohane mambo mnayoyasikia na kuyaona: Vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa Habari Njema. Heri mtu yule ambaye hana mashaka nami.”

Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha
kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana,wala si kwa akili zetu
si kwa nguvu zetu na si kwamba sisi ni wazuri mno..
Nikwa neema/rehema zako ni kwa mapenzi yako Mungu wetu
sisi kuwa hivi tulivyo leo hii..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu wetu...!!!



Yahweh tazama jana imepita leo ni siku mpya na kesho ni siku
nyingine..
Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza
kuwasamehe wale wote waliotukosea...
Baba wa Mbinguni usitutie katika majaribu Yahweh utuokoe
na yule mwovu na kazi zake zote
Nguvu za giza,nguvu za mapepo,nguvu za mizimu,nguvu za 
mpinga Kristo zikashindwe katika jina la Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo...
Jehovah tunaomba ukatutakase miili yetu na akili zetu
Mungu wetu ukatufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi
tupate kupona,kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona...


Basi, hao wajumbe wa Yohane walipokuwa wanakwenda zao, Yesu alianza kuyaambia makundi ya watu habari za Yohane: “Mlikwenda kutazama nini kule jangwani? Je, mlitaka kuona mwanzi unaotikiswa na upepo? Basi, mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona mtu aliyevaa mavazi maridadi? Watu wanaovaa mavazi maridadi hukaa katika nyumba za wafalme. Lakini, mlikwenda kuona nini? Nabii? Naam, hakika ni zaidi ya nabii. “Huyu ndiye anayesemwa katika Maandiko Matakatifu: ‘Tazama, mimi namtuma mjumbe wangu akutangulie, ambaye atakutayarishia njia yako’. Kweli nawaambieni, miongoni mwa watoto wote wa watu, hajatokea aliye mkuu kuliko Yohane Mbatizaji. Hata hivyo, yule aliye mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni, ni mkubwa kuliko yeye. Tangu wakati wa Yohane Mbatizaji mpaka leo hii, ufalme wa mbinguni unashambuliwa vikali, na watu wakali wanajaribu kuunyakua kwa nguvu. Mafundisho yote ya manabii na sheria mpaka wakati wa Yohane yalibashiri juu ya nyakati hizi. Kama mwaweza kukubali basi, Yohane ndiye Elia ambaye angekuja. Mwenye masikio na asikie! “Basi, nitakifananisha kizazi hiki na kitu gani? Ni kama vijana waliokuwa wamekaa uwanjani, wakawa wakiambiana kikundi kimoja kwa kingine: ‘Tumewapigieni ngoma lakini hamkucheza! Tumeimba nyimbo za huzuni lakini hamkuomboleza!’ Kwa maana Yohane alikuja, akafunga na wala hakunywa divai, nao wakasema: ‘Amepagawa na pepo’. Mwana wa Mtu akaja, anakula na kunywa, nao wakasema: ‘Mwangalieni huyu, mlafi na mlevi, rafiki yao watozaushuru na wenye dhambi!’ Hata hivyo, hekima ya Mungu inathibitishwa kuwa njema kutokana na matendo yake.”

Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Mungu wetu nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji...

Mungu wetu tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu tunaomba ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni
tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Yahweh tunaomba
ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Mungu wetu
tunaomba ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Mwanao
mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo...
Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika
maisha yetu,Mungu wetu tukawe salama rohoni Baba wa Mbinguni
tunaomba ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti
yako na kuitii,Jehovah tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia
zako Mungu wetu tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku
zote za maisha yetu,Yahweh ukatupe neema ya kutambua
mema na mabaya,Mungu wetu Nuru yako ikaangaze katika maisha 
yetu,Baba wa Mbinguni ukatufanye barua njema nasi tukasomeke
kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...



Kisha Yesu akaanza kuilaumu miji ambayo, ingawaje alifanya miujiza mingi humo, watu wake hawakutaka kutubu: “Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika kule Tiro na Sidoni, watu wake wangalikwisha vaa mavazi ya gunia kitambo na kujipaka majivu kutubu. Hata hivyo, nawaambieni, siku ya hukumu, nyinyi mtapata adhabu kubwa kuliko ya Tiro na Sidoni. Na wewe Kafarnaumu, je, utajikweza mpaka mbinguni? Utaporomoshwa mpaka kuzimu! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika kule Sodoma, mji huo ungalikuwako mpaka hivi leo. Lakini nawaambieni, siku ya hukumu wewe utapata adhabu kubwa kuliko ya Sodoma.”

Yahweh tazama wenye shida/tabu,Wagonjwa,wenye njaa,
wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,walio kata tamaa,
walio kataliwa,wenye hofu na mashaka,walio katika vifungo vya
yule mwovu,walio magerezani pasipo na hatia,walioanguka/potea
waliokwenda kinyume nawe,wote walio elemewa na mizito mizito,
walioumizwa rohoni,walio kwama kibiashara,wanaotafuta kazi,
wenye kutafuta watoto na wengine wote kila mmoja na hitaji lake..
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaponye kiroho na kimwili pia
Jehovah tunaomba ukawavushe salama,Mungu wetu ukawaoke
na kuwalinda,Baba wa Mbinguni haki ikatendeke
Yahweh tunaomba ukabariki mashamba yao,vyanzo vyao
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea na kufuata
njia zako,Jehovah tunaomba ukawasamehe na kuwasimamisha tena
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao Baba wa Mbinguni ukawafute
machozi yao,Mungu wetu ukaonekane katika maisha yao
Nuru yako ikaangaze,Neema/rehema zikawe nao
Baba wa Mbinguni tunaomba ukasikie,ukapokee sala/maombi yetu

Wakati huo Yesu alisema, “Nakushukuru ee Baba, Bwana wa mbingu na dunia, maana umewaficha wenye hekima na wenye elimu mambo haya, ukawafunulia wadogo. Naam, Baba, ndivyo ilivyokupendeza. “Baba yangu amenikabidhi vitu vyote. Hakuna amjuaye Mwana ila Baba, wala amjuaye Baba ila Mwana, na yeyote yule ambaye Mwana anapenda kumfunulia. Njoni kwangu nyinyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jifungeni nira yangu, mkajifunze kwangu, maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtatulizwa rohoni mwenu. Maana, nira niwapayo mimi ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”
Mungu wetu ukawatendee sawaswa na mapenzi yako
Kwakuwa ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina....!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwa kuwa nami/kunisoma
Mungu wetu aendelee kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye...
Amani ya Kristo Yesu ikawe nayi daima....
Nawapenda.

Ikulu ya Solomoni

1Solomoni alijijengea ikulu, nayo ilimchukua miaka kumi na mitatu kumalizika. 2Kisha, akajenga jengo lililoitwa Nyumba ya Msitu wa Lebanoni. Urefu wake ulikuwa mita 44.5, upana wake mita 22.25, na kimo chake mita 13.5. Ilikuwa imejengwa juu ya safu 3 za nguzo za mierezi, nguzo ambazo zilishikilia boriti za mierezi kwa upande wa juu. 3Kila safu ilikuwa na nguzo 15; basi zote pamoja zilikuwa nguzo 45. Vyumba vilivyojengwa juu ya nguzo hizo, alivitilia dari ya mbao za mierezi. 4Kulikuwa na safu tatu za madirisha yaliyoelekeana. 5Milango yote ilikuwa ya mraba, na miimo ya madirisha hayo yaliyoelekeana ilikuwa pia ya mraba.
6Alijenga ukumbi wa nguzo, ambao urefu wake ulikuwa mita 22.25, na upana wake mita 13.5. Kwenye sehemu ya mbele ya jengo hilo kulikuwa na sebule. Mbele ya sebule kulikuwa na nguzo; na mbele ya nguzo kulitokeza paa dogo.
7Solomoni alijenga ukumbi wa kiti cha enzi ambamo aliamulia kesi za watu. Huu uliitwa pia Ukumbi wa Hukumu. Ulikuwa umepambwa kwa mbao za mierezi kutoka sakafu mpaka dari.
8Nyumba yake ya kukaa mwenyewe, iliyokuwa nyuma ya Ukumbi wa Hukumu, ilikuwa imejengwa kama zile nyingine. Solomoni pia alijenga nyumba kama ukumbi huo kwa ajili ya binti Farao, ambaye alikuwa amemwoa.
9Majengo hayo yote yalijengwa kwa mawe ya thamani kutoka msingi mpaka juu, mawe ambayo yalikuwa yamechongwa kwa vipimo maalumu, na kukatwa kwa msumeno upande wa ndani na wa nje. 10Msingi ulikuwa wa mawe ya thamani na makubwa yenye urefu wa mita 3.5, na upana mita 4.5. 11Sehemu za juu zilijengwa kwa mawe mengine yaliyochongwa kwa vipimo maalumu, na kwa mbao za mierezi.
12Ua wa nyumba ya mfalme ulikuwa na kuta zenye safu moja ya mbao za mierezi na safu tatu za mawe ya kuchongwa kila moja; ndivyo ilivyokuwa hata kwa ua wa ndani wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kwa ukumbi wa nyumba.

Kazi za Hiramu

13Kisha mfalme Solomoni alimwita Hiramu kutoka Tiro. 14Huyo, alikuwa mwana wa mjane wa kabila la Naftali, na baba yake alikuwa mkazi wa Tiro, mfua shaba. Hiramu alikuwa na hekima nyingi na akili, na fundi stadi wa kazi yoyote ya shaba. Basi, alikuja kwa mfalme Solomoni, akamfanyia kazi yake yote.

Nguzo mbili za shaba za hekalu

(2Nya 3:15-17)

15Hiramu alitengeneza nguzo mbili za shaba, kila moja ikiwa na urefu wa mita 54, na mzingo wa mita 5.5. Ndani zilikuwa na tundu ambalo unene wa pande zake ulikuwa sentimita 2. 16Akatengeneza pia taji mbili za shaba, kila moja ikiwa na kimo cha mita 2.25; akaziweka juu ya nguzo hizo. 17Halafu, alifuma nyavu mbili zenye mapambo ya mrabamraba, akatengeneza na taji kwa kusokota mkufu: Vyote hivyo kwa ajili ya kupamba taji za shaba zilizowekwa juu ya zile nguzo. 18Hali kadhalika, alitengeneza matunda aina ya makomamanga, akayapanga safu mbili kuzunguka zile taji juu ya kila nguzo. 19Na taji hizo zilizokuwa juu ya nguzo mbele ya sebule, zilipambwa kwa mifano ya maua ya yungiyungi, kimo chake mita 1.75. 20Taji hizo zilikuwa juu ya hizo nguzo mbili, na pia zilikuwa juu ya sehemu ya mviringo iliyojitokeza karibu na zile nyavu. Palikuwa na mifano 400 ya matunda ya mkomamanga, imepangwa safu mbili kuzunguka kila taji.
21Hiramu aliziweka nguzo hizo kwenye sebule ya hekalu; nguzo aliyoisimika upande wa kusini iliitwa Yakini, na ile aliyoisimika upande wa kaskazini iliitwa Boazi. 22Vichwa vya nguzo hizo vilipambwa kwa mfano wa maua ya yungiyungi. Na hivyo kazi ya kutengeneza nguzo ikamalizika.

Tangi la shaba

(2Nya 4:2-5)

23Hiramu alitengeneza Birika liitwalo Bahari. Lilikuwa la mviringo lenye upana wa mita 4.5 kutoka ukingo hadi ukingo, na urefu wa mita 2.25 na mzingo wa mita 13.5. 24Chini ya ukingo wake, kulizunguka tangi hilo, kulikuwa na safu mbili za vibuyu, kila kimoja mita 13.5. Vibuyu hivyo vilikuwa vimetengenezwa wakati huohuo tangi hilo lilipofanywa. 25Nalo tangi lilikuwa limewekwa juu ya sanamu za mafahali kumi na wawili; tatu zikielekea upande wa kaskazini, tatu zikielekea magharibi, tatu kusini, na nyingine tatu mashariki. Tangi liliwekwa juu ya mafahali hao, sehemu zao za nyuma zikiwa ndani. 26Unene wa ukingo wake ulikuwa sentimita 7.5; nao ulikuwa ukifanana na ukingo wa kikombe na kama ua la yungiyungi. Tangi liliweza kujaa maji kiasi cha lita 40,000.

Magari ya shaba

27Hiramu pia alitengeneza magari kumi ya shaba, kila gari likiwa na urefu wa mita 1.75, upana wa mita 1.75, na kimo cha mita 1.25. 28Magari hayo yalikuwa yameundwa hivi: Kulikuwa na mabamba ya chuma ambayo yalikuwa yameshikiliwa na mitalimbo. Juu ya mabamba hayo yaliyoshikiliwa na mitalimbo, 29kulikuwa na sanamu za simba, mafahali na viumbe wenye mabawa. Sanamu hizo za simba na mafahali, zilikuwa zimefunikwa na kutandikwa mapambo yaliyosokotwa vizuri. 30Isitoshe, kila gari lilikuwa na magurudumu manne ya shaba, na vyuma vya katikati vya kuyazungukia magurudumu hayo, vilikuwa vya shaba. Kwenye pembe nne za gari kulikuwa na vishikizo vya shaba kwa ajili ya birika kubwa. Karibu ya kila kishikio kuliwekwa mapambo ya maua ya kusokotwa. 31Mlango wa gari ulikuwa katika sehemu iliyotokeza juu kwa kiasi cha nusu mita. Kwa nje, mlango ulikuwa umetiwa michoro; na mabamba yake yalikuwa ya mraba, si ya mviringo. 32Na hayo magurudumu manne yalikuwa chini ya yale mabamba; vyuma vya katikati kuzunguka magurudumu hayo vilikuwa vimeunganishwa na mfumo wa gari lenyewe; na kimo cha magurudumu hayo kilikuwa sentimita 66. 33Hayo magurudumu yalikuwa kama magurudumu ya magari ya kukokotwa; na vyuma vyake vya katikati, duara zake, mataruma yake na vikombe vyake: Hivyo vyote vilikuwa vya kusubu. 34Chini ya kila gari kulikuwa na mihimili minne kwenye pembe zake, nayo ilishikamanishwa na gari. 35Na juu ya kila gari palikuwa na utepe uliofanyiza duara ya kimo cha sentimita 22; na vishikio na mabamba yaliyokuwa upande wa juu yalishikamana na gari lenyewe. 36Kwenye nafasi wazi iliyopatikana katika vishikio na mabamba ya kila gari, Hiramu alichonga michoro ya viumbe wenye mabawa, simba na miti ya mitende, akazungushia na mashada ya mapambo. 37Mifano hiyo yote kumi ya magari ilifanana, ikiwa na kimo kimoja na muundo uleule.
38Hiramu, pia alitengeneza mabirika kumi ya shaba, moja kwa kila gari. Kila birika ilikuwa na upana wa mita 1.75, na iliweza kuchukua maji kadiri ya lita 880. 39Akaweka magari matano upande wa kusini wa nyumba, na matano upande wa kaskazini; na lile tangi akaliweka kwenye pembe ya kusini-mashariki ya nyumba.

Vifaa vya hekalu

(2Nya 4:11–5:1)

40Hiramu alitengeneza pia vyungu, sepetu na mabirika. Basi, Hiramu akamaliza kazi aliyoamriwa na mfalme Solomoni kuhusu nyumba ya Mwenyezi-Mungu: 41Nguzo mbili, mabakuli mawili ya taji zilizowekwa juu ya nguzo, na nyavu mbili kwa ajili ya kufunika hizo taji mbili, 42mifano ya makomamanga 400 kwa ajili ya nyavu hizo mbili, safu mbili za makomamanga kwa kila wavu ili kupamba zile taji mbili zilizokuwa juu ya nguzo. 43Hali kadhalika, alitengeneza magari kumi, na vishikio kumi katika magari hayo; 44na tangi lile moja na sanamu za mafahali kumi na wawili, chini ya hilo tangi. 45Halafu vile vyungu, sepetu na mabirika, vyombo hivyo vyote vilivyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu ambavyo Hiramu alimtengenezea mfalme Solomoni, vilikuwa vya shaba iliyongarishwa. 46Vitu hivyo vyote mfalme alivitengeneza katika uwanda wa Yordani, sehemu ya udongo wa mfinyanzi iliyokuwa kati ya Sukothi na Sarethani. 47Solomoni hakupima uzani wa vifaa hivi vyote kwa kuwa vilikuwa vingi sana, na kwa sababu uzani wa shaba haukujulikana.
48Solomoni alitengeneza vifaa vyote vilivyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu: Madhabahu ya dhahabu, meza ya dhahabu kwa ajili ya mikate ya kuwekwa mbele ya Mungu, 49vinara vya taa vya dhahabu safi vilivyowekwa mbele ya mahali patakatifu sana, vitano upande wa kusini na vitano upande wa kaskazini; maua, taa, koleo, vyote vikiwa vya dhahabu; 50vikombe, makasi ya kukatia tambi za mishumaa, mabakuli, vyetezo vya kuwekea ubani, miiko ya kuchukulia moto, vyote vya dhahabu safi; bawaba za milango ya sehemu ya ndani kabisa ya nyumba – pale mahali patakatifu sana – na bawaba za milango ya ukumbi wa ibada wa hekalu bawaba zote za dhahabu.
51Basi, mfalme Solomoni akamaliza kazi zote zilizohusu nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Kisha Solomoni akaleta mali yote ambayo baba yake Daudi, alikuwa ameiweka wakfu, yaani: Fedha, dhahabu na vyombo; akaiweka katika hazina za nyumba ya Mwenyezi-Mungu.



1Wafalme7;1-51


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: