Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday, 1 March 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Samueli 23...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana..
Tumshukuru Mungu katika yote...

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu mwenye nguvu,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu uponyae,
Mungu unayebariki,Mungu wetu akisema ndiyo nani atasema siyo,
Mungu wetu si Mungu wa fujo ila  ni  wa amani...
Utukuzwe ee Baba wa Mbinguni,Unasthahili sifa Mungu wetu
Unastahili kuabudiwa Jehovah,Unastahili Kuhimidiwa Yahweh..
Neema yako yatutosha ee Baba wa Mbinguni...!!


Mwimbieni kwa sauti Mungu, nguvu yetu, mshangilieni Mungu wa Yakobo; vumisheni wimbo wa shangwe, pigeni ngoma, chezeni zeze na kinubi cha sauti nzuri. Pigeni tarumbeta kutangaza mwezi mwandamo, na pia mwezi mpevu, wakati wa sikukuu yetu.


Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu..
Sifa na Utukufu tunakurudishia wewe Mungu wetu...!

Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na 
kujiachilia mikononi mwako ee Mungu wetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
 wale wote waliotukosea...
Jehovah tunaomba utuepushe katika majaribu Baba wa Mbinguni
utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi
wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili 
sisi tupate kupona....


Hiyo ndiyo kanuni katika Israeli; hilo ndilo agizo la Mungu wa Yakobo. Aliwapa watu wa Israeli agizo hilo, alipoishambulia nchi ya Misri. Nasikia sauti nisiyoitambua ikisema: “Mimi nilikutua mizigo yako mabegani, nilikuondolea matofali uliyochukua mikononi. Ukiwa shidani uliniita, nami nikakuokoa. Nilikujibu nikiwa mafichoni katika ngurumo. Nilikujaribu kwenye maji ya Meriba.



Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa
katika utendaji Yahweh nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji..
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni
ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika
maisha yetu...
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu ukatubariki tuingiapo/tutokapo Jehovah tunaomba 
ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni
ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Jehovah ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tukawe
salama moyoni Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio
ya kusikia sauti yako na kuitii..
Yahweh ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu..
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu,popote tupitapo
na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni..
Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu,mani ikatawale,
upendo ukadumu kati yetu...
Jehovah tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku
zote za maisha yetu....
Ukatufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Enyi watu wangu, sikieni onyo langu. Laiti ungenisikiliza, ee Israeli! Asiwepo kwako mungu wa kigeni; usiabudu kamwe mungu mwingine. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri. Fumbua kinywa chako, nami nitakulisha. “Lakini watu wangu hawakunisikiliza; Israeli hakunitaka kabisa. Hivyo, nikawaacha wabaki na ukaidi wao; wafuate mashauri yao wenyewe. Laiti watu wangu wangenisikiliza! Laiti Israeli angefuata njia yangu! Ningewashinda maadui zao haraka; ningenyosha mkono dhidi ya wadhalimu wao. Wanichukiao wangenipigia magoti kwa hofu, na adhabu yao ingekuwa ya milele. Lakini wewe ningekulisha kwa ngano bora, ningekushibisha kwa asali ya mwambani.”

Yahweh tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
wenye shida/tabu Mungu wetu tunaomba ukawaponye wagonjwa
Yahweh ukawape nguvu na uvumilivu wanaowauguza
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawape chakula wenye njaa
Munguwetu tunaomba ukabariki mashamba/kazi zao
Jehovah wakapate chakula cha kutosha kuweka akiba na kuisaidia
wengine..
Mungu wetu tunaomba ukawavushe salama wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali..Jehovah ukawaokoe wote walio katika 
vifungo vya yule mwovu Baba wa Mbinguni tunaomba ukawawe
huru...
Mungu wetu tazama walio magerezani pasipo na hatia
Yahweh tunaomba ukawatendee na haki ikatendeke..
Mungu wetu tunaomba ukawe tumaini kwa walio kata tamaa,
waliokataliwa,wenye hofu na mashaka Jehovah tunaomba
ukawasamehe wale wote waliokwenda kinyume nawe
Mungu wetu tunaomba ukawape neema ya kujiombea,
kufuata njia zako na kusimamia Neno lako nalo likawaweke huru
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao..
Yahweh tunaomba ukasikie sala/maombi yetu Mungu wetu
ukatende sawasawa na mapenzi yako..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na utukufu hata Milele..
Amina..!!

Wapendwa/waungwana asanteni sana kwakuwanami/kunisoma
Baba wa Mbinguni aendelee kuwabariki na msipungukiwe katika 
mahitaji yenu Mungu akawape sawasawa na mapenzi yake....
Nawapenda.




Maneno ya mwisho ya Daudi

1Yafuatayo ni maneno ya mwisho ya Daudi. Ni ujumbe wa Daudi mwana wa Yese; ujumbe wa mtu ambaye Mungu alimfanya awe mkuu. Mungu wa Yakobo alimteua Daudi kuwa mfalme na maneno yake Waisraeli walifurahi kuyaimba.
2“Roho ya Mwenyezi-Mungu imesema kwa njia yangu,
aliyaweka maneno yake kinywani mwangu.
3Mungu wa Israeli amesema,
Mwamba wa Israeli ameniambia,
‘Mtu anapowatawala watu kwa haki,
atawalaye kwa kumcha Mungu,
4yeye ni kama mwanga wa asubuhi,
jua linapochomoza asubuhi isiyo na mawingu;
naam, kama mvua inayootesha majani ardhini’.
5Hivyo ndivyo Mungu alivyoujalia ukoo wangu.
Maana amefanya nami agano la kudumu milele;
agano kamili na thabiti.
Naye atanifanikisha katika matakwa yangu yote.
6Lakini wasiomcha Mungu
wote ni kama miiba inayotupwa tu,
maana haiwezi kuchukuliwa kwa mkono;
7kuishika, lazima kutumia chuma au mpini wa mkuki.
Watu hao wataangamizwa kabisa kwa moto.”

Orodha ya mashujaa wa Daudi

(1Nya 11:10-41)

8Yafuatayo ni majina ya mashujaa aliokuwa nao Daudi: Yosheb-bashebethi, Mtakmoni, aliyekuwa kiongozi wa wale watatu,23:8 watatu: Makala ya Kiebrania si dhahiri. yeye alipigana kwa mkuki wake,23:8 yeye … wake: Makala ya Kiebrania si dhahiri. akaua watu 800 wakati mmoja.
9Halafu aliyefuata miongoni mwa wale mashujaa watatu alikuwa Eleazari mwana wa Dodo, wa ukoo wa Mwahohi. Siku moja, Eleazari alikuwa pamoja na Daudi walipowatukana Wafilisti waliokuwa wamekusanyika kupigana vita. Waisraeli waliwakimbia Wafilisti. 10Lakini Eleazari alisimama imara na kupigana na Wafilisti mpaka mkono wake uliposhindwa kupinda, ukabaki umeshikilia upanga wake. Siku hiyo, Mwenyezi-Mungu alijipatia ushindi mkubwa. Baada ya ushindi huo, Waisraeli walirudi mahali alipokuwa Eleazari na kujipatia nyara za bure kutoka kwa Wafilisti waliouawa.
11Shujaa wa tatu alikuwa Shama mwana wa Agee, Mharari. Wafilisti walikusanyika huko Lehi, mahali palipokuwa na shamba la dengu nyingi, nao Waisraeli waliwakimbia Wafilisti. 12Lakini alisimama imara katikati ya shamba hilo ili kulitetea, naye akawaua Wafilisti. Mwenyezi-Mungu alijipatia ushindi mkubwa.
13Kisha, mashujaa watatu kati ya wakuu thelathini waliteremka wakati wa mavuno23:13 wakati … mavuno: Makala ya Kiebrania si dhahiri. wakamfikia Daudi kwenye pango huko Adulamu. Wakati huo jeshi la Wafilisti lilikuwa limepiga kambi katika bonde la Refaimu. 14Naye Daudi wakati huo alikuwa katika ngome, nalo jeshi la Wafilisti lilikuwa mjini Bethlehemu. 15Daudi akasema kwa hamu kubwa, “Laiti mtu angeweza kunipa maji ya kunywa kutoka katika kisima cha Bethlehemu, kilicho karibu na lango la mji!” 16Wale mashujaa wake watatu walitoka, wakapenya katikati ya kambi ya jeshi la Wafilisti, wakaenda na kuchota maji katika kisima cha Bethlehemu, karibu na lango la mji, wakamletea Daudi. Lakini Daudi alikataa kuyanywa, na badala yake, akayamwaga chini kama tambiko kwa Mwenyezi-Mungu, 17akisema, “Kamwe, sina haki ya kunywa maji haya, ee Mwenyezi-Mungu; je, haya si kama damu ya wale walioyahatarisha maisha yao kuyaleta maji haya?” Kwa hiyo, Daudi hakuyanywa maji hayo. Hayo ndiyo mambo waliyotenda wale mashujaa watatu.
18Abishai nduguye Yoabu, mwana wa Seruya, alikuwa mkuu wa mashujaa thelathini.23:18 thelathini: Makala ya Kiebrania: Watatu. Yeye alipigana kwa mkuki wake dhidi ya watu 300, akawaua, akajipatia jina miongoni mwa wale mashujaa watatu. 19Je, huyo hakuwa mashuhuri zaidi miongoni mwa mashujaa watatu? Kwa hiyo akawa kamanda wao, lakini hakuwa shujaa kama wale mashujaa watatu. 20Naye Benaya mwana wa Yehoyada, kutoka Kabzeeli, alikuwa askari shujaa23:20 askari shujaa: Kiebrania: Mwana wa askari shujaa. ambaye alifanya mambo mengi ya ajabu. Aliwaua mashujaa wawili23:20 mashujaa: Kiebrania si dhahiri. kutoka Moabu, na siku moja wakati wa theluji, alishuka shimoni na kuua simba. 21Vilevile, aliliua jitu la Misri. Mmisri huyo alikuwa na mkuki, lakini Benaya alimwendea akiwa na fimbo tu, akamnyanganya mkuki huo, na kumwua Mmisri huyo kwa mkuki wake mwenyewe. 22Benaya, mwana wa Yehoyada alifanya mambo haya, akajipatia jina miongoni mwa wale mashujaa watatu. 23Basi, akawa mashuhuri kati ya wale mashujaa thelathini, ingawa hakuwa kama wale mashujaa watatu. Na Daudi akampa cheo cha mkuu wa walinzi wake binafsi. 24Asaheli, nduguye Yoabu, alikuwa mmoja wa mashujaa thelathini. Mashujaa wengine wa Daudi walikuwa: Elhanani, mwana wa Dodo wa Bethlehemu; 25Shama, Mharodi; Elika, Mharodi; 26Helesi, Mpalti; Ira, mwana wa Ikeshi, Mtekoa; 27Abiezeri, Mwanathothi; Mebunai, Mhushathi; 28Salmoni, Mwahohi; Maharai, Mnetofathi; 29Helebu mwana wa Baana, Mnetofathi; Itai mwana wa Ribai, toka Gibea katika Benyamini; 30Benaya, Mpirathoni; Hidai, wa vijito vya Gaashi; 31Abialboni, Mwarbathi; Azmawethi, Mbahurimu; 32Eliaba, Mshaalboni; wana wa Yasheni; Yonathani; 33Shama, Mharari; Ahimu mwana wa Sharari, Mharari; 34Elifeleti mwana wa Ahasbai, Mmaaka; Eliamu mwana wa Ahithofeli, Mgiloni; 35Hesrawi, Mkarmeli; Paarai, Mwarbi; 36Igali mwana wa Nathani, Msoba; Bani, Mgadi; 37Seleki, Mwamoni; Naharai, Mbeerothi aliyekuwa mbeba silaha wa Yoabu mwana wa Seruya; 38Ira na Garebu, Waithri; 39na Uria, Mhiti. Wote pamoja walikuwa mashujaa thelathini na saba.



2Samweli23;1-39

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: