Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday, 2 March 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Samueli 24...Mwisho wa kitabu cha Samueli...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah  Mungu wetu yu mwema sana....

Tunamshukuru Mungu kwa kumaliza/kupitia kitabu hiki
cha "2 Swamuel" Natumai kupitia kitabu hiki na vingine
tulivyopitia kuna mengi tumejifunza...
Mungu wetu akatuongoze na kutupa neema ya kuendelea
kusoma zaidi na tukapate kuelewa...
Mungu akatupe macho ya rohoni katika kujifunza..
Akatupe shauku/kiu/hamu ya kujifunza zaidi na ikawe
faida kwetu na wengine pia...
ee Baba tunaomba utusikie....!!

Mwanangu, ukiyakubali maneno yangu, na kuyathamini maagizo yangu; ukitega sikio lako kusikiliza hekima, na kuuelekeza moyo wako upate ufahamu; naam, ukiomba upewe busara, ukisihi upewe ufahamu; ukiitafuta hekima kama fedha, na kuitaka kama hazina iliyofichika; hapo utaelewa ni nini kumcha Mwenyezi-Mungu, utafahamu maana ya kumjua Mungu.


Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu...
Utukuzwe ee Mungu wetu,wewe ni Mungu mwenye nguvu,
Mungu unayeponya,Mungu unayeokoa,Mungu unaye jibu,Mungu unayesikia,
Mungu unaye tenda sawasawa na mapenzi yako...
Unatosha ee Baba wa Mbinguni,Jehovah Jireh,Jehovah Nissi,
Jehovah Rapha,Jehovah Raah,Jehovah Shammah,Jehovah Shalom
Emanuel-Mungu pamoja nasi......!!

Maana Mwenyezi-Mungu huwapa watu hekima; kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu. Huwawekea wanyofu akiba ya hekima safi, yeye ni ngao kwa watu waishio kwa uaminifu. Huilinda mienendo ya watu watendao haki, na kuzihifadhi njia za waaminifu wake. Ukinisikiliza utafahamu uadilifu na haki, utajua jambo lililo sawa na jema. Maana hekima itaingia moyoni mwako, na maarifa yataipendeza nafsi yako.


Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachlia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
 wale wote waliotukosea
Yahweh tunaomba usitutie katika majaribu Mungu wetu
utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
nguvu za giza,nguvu za mapepo,nguvu za mizimu,
nguvu za mpinga Kristo zishindwe katika jina lililokuu jina la Bwana
na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza
ili sisi tupate kupona...

Busara itakulinda, ufahamu utakuhifadhi; vitakuepusha na njia ya uovu, na watu wa maneno mapotovu; watu waziachao njia nyofu, ili kuziendea njia za giza; watu wafurahiao kutenda maovu, na kupendezwa na upotovu wa maovu; watu ambao mienendo yao imepotoka, nazo njia zao haziaminiki.


Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Mungu wetu ukatupe maarifa na ubunifu katika utendeji
Yahweh nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji..
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu ukatupe
kama inavyokupendeza wewe...

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Jehovah tunaomba ukatamalaki na kutuatamia,Yahweh tunaomba
ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukabariki
vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni tunaomba
ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo...
Yahweh ukaonekane katika maisha yetu Mungu wetu popote
tupitapo na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni...
Neema yako na Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatuepushe na kiburi,majivuno,choyo,kisasi,unafiki,makwazo
na yote yanayokwenda kinyume nawe
Mungu wetu ukatupe neema ya kufuata njia zako Yahweh tukasimamie
Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Ukatufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike
 kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Hekima itakuwezesha kumkwepa mwanamke mwasherati, mwanamke malaya wa maneno matamu; mwanamke amwachaye mwenzi wa ujana wake, na kulisahau agano la Mungu wake. Nyumba yake yaelekea kuzimu, njia zake zinakwenda ahera. Yeyote amwendeaye kamwe harudi, wala hairudii tena njia ya uhai. Kwa hiyo utafuata mfano wa watu wema, na kuzingatia mienendo ya waadilifu. Maana wanyofu wataipata nchi, na waaminifu watadumu ndani yake. Lakini waovu wataondolewa nchini, na wenye hila watangolewa humo.


Yahweh tazama wenye shida/tabu Mungu wetu wagonjwa,wenye njaa
wanaopitia magumu/majaribu,Jehovah walio katika vifungo vya yule mwovu,Yahweh walio magerezani pasipo na hatia
wenye hofu na mashaka,walio kataliwa,walio kata tamaa na wote
wakutafuatao kwa bidii na imani...
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaponye kimwili na kiroho pia
Yahweh ukawape chakula na ukabariki mashamba/kazi zao
Jehovah ukawavushe salama na ukawaokoe Baba wa Mbinguni
ukaonekane katika maisha yao, Jehovah ukawafute machozi ya watoto
wako Yahweh ukawape neema ya kijiombea na kufuata njia zako
Mungu wetu tunaomba ukasikie na ukapokee sala/maombi yetu
Jehovah ukawatendee sawasawa na mapenzi yako..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina.....!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwa kuwa nami
Baba wa Mbinguni akawabariki na kuwatendea
 kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.



Daudi anawahesabu Waisraeli

(1Nya 21:1-27)

1Kwa mara nyingine, Mwenyezi-Mungu aliwakasirikia Waisraeli, akamchochea Daudi dhidi yao, akamwambia awahesabu watu wa Israeli na watu wa Yuda. 2Hivyo, mfalme akamwambia Yoabu, na makamanda wa jeshi waliokuwa pamoja naye, “Nendeni katika makabila yote ya Israeli kutoka Dani mpaka Beer-sheba, mkawahesabu watu ili nipate kujua idadi yao.” 3Lakini Yoabu akamwambia mfalme, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, na awaongeze Waisraeli mara mia kuliko walivyo sasa, nawe bwana wangu mfalme upate kuona ongezeko hilo kwa macho yako mwenyewe. Lakini, kwa nini wewe bwana wangu mfalme unapendezwa na jambo hili?” 4Lakini tamko la mfalme lilikuwa na nguvu zaidi dhidi ya Yoabu na makamanda wa jeshi! Basi, Yoabu na makamanda wa jeshi wakaondoka mbele ya mfalme, wakaenda kuwahesabu Waisraeli. 5Walivuka mto Yordani wakianzia kuhesabu watu tangu Aroeri na mto ulioko bondeni kuelekea Gadi24:5 Aroeri … Gadi: Makala ya Kiebrania si dhahiri. hadi Yazeri. 6Kisha, wakaenda Gileadi halafu Kadeshi katika nchi ya Wahiti,24:6 Kadeshi … Wahiti: Makala ya Kiebrania: Kwenye nchi ya Tahtimu, Hodshi. halafu wakawasili Dani na kutoka Dani wakazunguka kwenda24:6 na kutoka Dani wakazunguka kwenda: Makala ya Kiebrania si dhahiri. Sidoni, 7na kufika kwenye ngome ya mji wa Tiro, wakaingia kwenye miji yote ya Wahivi na Wakanaani. Kisha, walitoka wakaenda Negebu ya Yuda huko Beer-sheba. 8Walipokwisha pitia katika nchi yote, walirejea Yerusalemu baada ya miezi tisa na siku ishirini. 9Halafu Yoabu alimpelekea mfalme idadi ya watu. Katika Israeli kulikuwamo wanaume mashujaa 800,000 wenye ujuzi wa kutumia mapanga; na katika Yuda, kulikuwa na wanaume 500,000. 10Lakini Daudi alisumbuliwa sana rohoni mwake baada ya kuwahesabu watu. Kwa hiyo, Daudi akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Nimetenda dhambi kubwa kwa tendo nililolifanya. Lakini sasa, ee Mwenyezi-Mungu, nakusihi unisamehe mimi mtumishi wako, kwani nimefanya jambo la kipumbavu kabisa.” 11Daudi alipoamka kesho yake asubuhi, wakati huo Mwenyezi-Mungu alimpa ujumbe nabii Gadi mwonaji wa mfalme Daudi, akisema, 12“Nenda ukamwambie hivi Daudi: ‘Mwenyezi-Mungu asema hivi: Ninakupa mambo matatu, nawe ujichagulie mojawapo, nami nitakutendea.’” 13Hivyo, Gadi akamwendea Daudi na kumweleza, akisema, “Je, wapendelea njaa ya miaka saba iijie nchi yako? Au je, wewe uwakimbie adui zako kwa miezi mitatu wanapokufuatia? Au kuwe na siku tatu ambapo nchi yako itakuwa na maradhi mabaya? Fikiri unipe jibu nitakalompa yeye aliyenituma.” 14Daudi akamjibu Gadi, “Nina mashaka makubwa! Lakini afadhali niadhibiwe na Mwenyezi-Mungu, kuliko kutiwa mikononi mwa watu, maana yeye ana huruma sana.”
15Basi, Mwenyezi-Mungu akawaletea Waisraeli maradhi, tangu asubuhi hadi wakati uliopangwa. Watu 70,000 walikufa nchini kote kutoka Dani mpaka Beer-sheba. 16Lakini wakati malaika aliponyosha mkono wake kuelekea mji wa Yerusalemu ili kuuangamiza, Mwenyezi-Mungu alibadilisha nia yake. Mwenyezi-Mungu akamwambia huyo malaika aliyetekeleza maangamizi kwa watu, “Basi! Yatosha; rudisha mkono wako.” Malaika wa Mwenyezi-Mungu alikuwa amesimama karibu na uwanja wa kupuria nafaka wa Arauna, Myebusi. 17Daudi alipomwona huyo malaika aliyekuwa anawaua watu, alimwambia Mwenyezi-Mungu, “Tazama, Mimi ndiye niliye na hatia! Mimi mwenyewe nimekosa! Hawa watu wapole hawakufanya uovu. Nakusihi sana uniadhibu mimi na jamaa ya baba yangu.”
18Siku hiyohiyo Gadi akamwendea Daudi, akamwambia, “Panda juu, ukamjengee Mwenyezi-Mungu madhabahu, katika kiwanja cha kupuria nafaka cha Arauna, Myebusi.” 19Basi, Daudi akapanda juu kufuatana na neno la Gadi kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru. 20Arauna alipoangalia upande wa chini alimwona mfalme akimkaribia pamoja na watumishi wake, naye akatoka, akaenda na kumsujudia mfalme, akainama mpaka chini ardhini. 21Kisha Arauna akamwuliza mfalme, “Kwa nini bwana wangu mfalme amenijia mimi mtumishi wake?” Daudi akamjibu, “Nimekuja kununua uwanja wako wa kupuria nafaka ili nimjengee Mwenyezi-Mungu madhabahu ili tauni iliyowakumba watu ikome.” 22Naye Arauna akamwambia Daudi, “Bwana wangu mfalme, chukua chochote unachoona kinafaa na utolee sadaka. Mimi nawatoa fahali hawa kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa na vifaa hivi vya kupuria na nira za ng'ombe kuwa kuni. 23Hivi vyote, ee mfalme, nakupa.24:23 nakupa: Makala ya Kiebrania: Mfalme kwa mfalme. Natumaini Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, atapokea sadaka yako kwa wema.” 24Lakini mfalme akamwambia Arauna, “La! Wewe hutanipa chochote. Mimi nitavinunua kwako kwa thamani yake. Sitamtolea Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, sadaka za kuteketezwa ambazo hazijanigharimu kitu.”
Hivyo, mfalme Daudi alinunua uwanja wa kupuria na fahali kwa fedha shekeli hamsini. 25Kisha Daudi akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu mahali hapo na kumtolea sadaka za kuteketezwa na za amani. Basi, Mwenyezi-Mungu akayakubali maombi kwa ajili ya nchi, na ile tauni iliyowakumba Waisraeli ikakoma.



2Samweli24;1-25


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: