Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday, 23 April 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Wafalme 13......



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana
Ni siku nyingine tena Mungu wetu ametuchagua na kutupa 
kibali cha kuendelea kuiona leo hii...
Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zao kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Utukuzwe ee Mungu wetu ,Usifiwe Baba wa Mbinguni,Uhinidiwe  Yahweh,
Uabudiwe Jehova....
Unatosha ee Mungu wetu,Matendo yako ni makuu mno,Matendo yako
ni ya ajabu,Matendo yako yanatisha...
Sifa na utukufu tunakurudishia Mungu wetu...!!



Baadaye mwezi wa saba ulipofika, na watu wa Israeli wakiwa wamekwisha kaa katika miji yao, wote walikusanyika pamoja mjini Yerusalemu. Yeshua, mwana wa Yosadaki, pamoja na makuhani wenzake, na Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, pamoja na jamaa zake, waliijenga upya madhabahu ya Mungu wa Israeli, ili waweze kumtolea sadaka za kuteketezwa kama ilivyoandikwa katika sheria ya Mose, mtu wa Mungu. Waliijenga madhabahu hiyo mahali palepale ilipokuwa hapo zamani, kwa kuwa waliwaogopa watu waliokuwa wanaishi katika nchi hiyo. Kisha wakawa wanamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka za kuteketezwa juu yake kila siku asubuhi na jioni.


Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na
kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya muweza kuwasamehe wale
wote waliotukosea
Mungu wetu utuepushe katika majaribu Yahweh tunaomba utuokoe na 
yule mwovu na kazi zake zote
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Yahweh  utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo
wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona...


Waliiadhimisha sikukuu ya vibanda kama ilivyoandikwa katika sheria; kila siku walitoa sadaka za kuteketezwa zilizohitajika kwa ajili ya siku hiyo. Walitoa pia sadaka za kawaida ambazo ziliteketezwa nzima, sadaka zilizotolewa wakati wa sikukuu ya mwezi mpya na katika sikukuu nyingine zote alizoagiza Mwenyezi-Mungu. Pia, walitoa tambiko zote zilizotolewa kwa hiari. Ingawa msingi wa hekalu la Mwenyezi-Mungu ulikuwa bado kuwekwa, watu walianza kutoa sadaka za kuteketezwa tangu siku ya kwanza ya mwezi wa saba.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya muweza kuwabariki
 wenye kuhitaji....
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni ukatupe 
kama inavyokupendeza wewe....

Mfalme wa amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi
wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Baba wa Mbinguni tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote 
tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba utubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Mungu wetu tukawe salama rohoni Yahweh ukatupe macho ya kuona
na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii
Jehovah tunaomba ukatupe neema ya kutambua mema na mabaya
Yahweh ukatupe neema ya kufuata njia zako Mungu wetu tukasimamie
Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
amani yako ikatawale,neema yako ikawe nasi,Nuru yako ikaangaze
katika maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu Yahweh ukatamalaki
na kutuamia..
Ukatufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike kama 
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Watu walitoa fedha za kuwalipa maseremala na waashi, walitoa pia chakula, vinywaji na mafuta, ili vipelekwe katika miji ya Tiro na Sidoni kupata miti ya mierezi kutoka Lebanoni. Miti hiyo ililetwa kwa njia ya bahari hadi Yopa. Haya yote yalifanyika kwa msaada wa mfalme Koreshi wa Persia. Basi, watu walianza kazi mnamo mwezi wa pili wa mwaka wa pili baada ya kufikia nyumba ya Mungu mjini Yerusalemu. Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, Yeshua mwana wa Yosadaki, ndugu zao wengine, makuhani, Walawi na watu wengine wote waliorudi Yerusalemu kutoka uhamishoni, walijiunga nao katika kazi hiyo. Walawi wote waliokuwa na umri wa miaka ishirini au zaidi, waliteuliwa ili kusimamia kazi ya kuijenga upya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Yeshua, wanawe na jamaa yake, pamoja na Kadmieli na wanawe, (wa ukoo wa Yuda) walishirikiana kusimamia ujenzi wa nyumba ya Mungu. Walisaidiwa na wazawa wa Henadadi na ndugu zao Walawi. Wajenzi walipoanza kuweka msingi wa hekalu la Mwenyezi-Mungu, makuhani wakiwa wamevalia mavazi yao rasmi, walisimama mahali pao na tarumbeta mikononi, nao Walawi wa ukoo wa Asafu wakisimama na matoazi yao; basi, walimtukuza Mwenyezi-Mungu kufuatana na maagizo ya mfalme Daudi wa Israeli. Waliimba kwa kupokezana, wakimsifu na kumtukuza Mwenyezi-Mungu: “Kwa kuwa yu mwema, fadhili zake kwa Israeli zadumu milele.” Watu wote walipaza sauti kwa nguvu zao zote, wakamsifu Mwenyezi-Mungu kwa sababu ya kuanza kujengwa msingi wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Wengi wa makuhani, Walawi, na viongozi wa koo waliokuwa wazee na ambao walikuwa wameiona nyumba ya kwanza, walilia kwa sauti kubwa walipouona msingi wa nyumba hii mpya unawekwa, ingawa watu wengine wengi walipaza sauti kwa furaha. Watu hawakuweza kutofautisha kati ya sauti za furaha na za kilio kwa sababu zilikuwa nyingi na zilisikika mbali sana.

Yahweh  tazama watoto wako wanaokutafuta/kukuomba
kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Jehovah tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Mungu wetu tunaomba ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimamie Neno lako nalo likawaweke huru
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao,amani ikatawale na upendo
ukadumu kati yao...
Ee Baba tunaomba ukasikie kulia kwao Mungu wetu tunaomba 
ukawafute machozi yao....
Baba wa Mbinguni tunaomba ukasikie na ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!

Asanteni sana wapewndwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami/kunisoma
Baba wa Mbinguni aendelee kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye...
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo wa Mungu Baba 
ukawe nanyi daima.....
Nawapenda.



Mfalme Yehoahazi wa Israeli

1Katika mwaka wa ishirini na tatu wa enzi ya mfalme Yoashi wa Yuda, Yehoahazi mwana wa Yehu alianza kutawala Israeli, akaendelea kutawala huko Samaria muda wa miaka kumi na saba. 2Alitenda dhambi mbele ya Mwenyezi-Mungu kama vile mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati aliyewakosesha watu wa Israeli wakatenda dhambi. Yehoahazi hakuacha matendo hayo mabaya. 3Mwenyezi-Mungu alikasirika, akawafanya watu wa Israeli washindwe vitani mara kwa mara na mfalme Hazaeli wa Aramu na mwanawe Ben-hadadi. 4Yehoahazi akamsihi Mwenyezi-Mungu, naye Mwenyezi-Mungu alipoona jinsi mfalme wa Aramu alivyowadhulumu watu wa Israeli alisikia maombi yake. 5(Mwenyezi-Mungu akawapa watu wa Israeli kiongozi ambaye aliwakomboa kutoka kwa Washamu, ndipo wakakaa kwa amani kama vile walivyokuwa hapo awali. 6Hata hivyo hawakuacha kutenda dhambi ambazo mfalme Yeroboamu aliwakosesha watu wa Israeli; lakini waliendelea13:6 lakini waliendelea; Kiebrania: Yeye aliendelea. na dhambi zao na sanamu ya mungu wa kike Ashera ilihifadhiwa huko Samaria.)
7Yehoahazi hakuwa na majeshi, ila tu wapandafarasi hamsini, magari kumi na askari wa miguu 10,000. Hii ilikuwa ni kwa sababu mfalme wa Aramu alikuwa ameyaangamiza majeshi ya Israeli na kuyakanyaga chini kama mavumbi.
8Matendo mengine yote ya Yehoahazi na ushujaa wake yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli. 9Yehoahazi alifariki na kuzikwa huko Samaria, naye mwanawe Yehoashi akawa mfalme mahali pake.

Mfalme Yehoashi wa Israeli

10Katika mwaka wa thelathini na saba wa enzi ya mfalme Yoashi wa Yuda, Yehoashi mwanawe Yehoahazi, alianza kutawala Israeli huko Samaria, na enzi yake ikaendelea kwa miaka kumi na sita. 11Yehoashi pia alitenda dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu na kufuata mfano wa mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati ambaye aliwapotosha watu wa Israeli. 12Matendo mengine yote ya Yehoashi, ushujaa wake na vita alivyopigana na mfalme Amazia wa Yuda, yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli. 13Yehoashi alifariki na kuzikwa katika makaburi ya kifalme huko Samaria, naye mwanawe Yeroboamu wa pili akatawala mahali pake.

Kifo cha Elisha

14Nabii Elisha aliugua ugonjwa mbaya sana. Alipokuwa karibu kufa, mfalme Yehoashi wa Israeli alimtembelea. Alipomfikia Elisha, alilia, akisema, “Baba yangu, baba yangu! Magari ya Israeli na wapandafarasi wake!” 15Elisha akamwamuru, “Hebu lete upinde na mishale!” Yehoashi akavileta. 16Elisha akamwambia ajitayarishe kupiga mishale. Mfalme akajitayarisha na Elisha akaiweka mikono yake juu ya mikono ya mfalme. 17Mfalme alifuata maagizo ya nabii na kufungua dirisha ambalo lilielekea Aramu. Elisha akatoa amri “Tupa mshale!” Mara tu mfalme alipotupa mshale, nabii akasema, “Wewe ndio mshale wa Mwenyezi-Mungu, ambao kwao atapata ushindi juu ya Waaramu. Utapigana na Waaramu huko Afeka mpaka uwashinde.”
18Ndipo Elisha akamwambia mfalme achukue mishale mingine na kuipiga chini. Mfalme akapiga mishale chini mara tatu, kisha akaacha. 19Elisha alikasirika sana, akamwambia mfalme, “Mbona hukupiga mara tano au sita? Hivyo ungewaangamiza Waaramu kabisa. Lakini sasa utawashinda mara tatu tu.”
20Elisha alifariki, akazikwa.
Kila mwaka, makundi ya Wamoabu yalikuja kuishambulia nchi ya watu wa Israeli. 21Wakati mmoja, wakati wa mazishi, watu waliona kundi mojawapo la watu waliobeba maiti wakamtupa yule maiti kaburini mwa Elisha na kukimbia. Mara maiti huyo alipogusa mifupa ya Elisha, alifufuka na kusimama wima.

Vita kati ya Israeli na Aramu

22Mfalme Hazaeli wa Aramu aliwanyanyasa sana watu wa Israeli wakati wote wa enzi ya Yehoahazi. 23Lakini Mwenyezi-Mungu aliwarehemu na kuwaonea huruma. Aliwaangalia kwa wema kwa sababu ya agano lake na Abrahamu, Isaka na Yakobo. Hakuwaangamiza wala hajawaacha kamwe mpaka leo.
24Hazaeli mfalme wa Aramu alipofariki, Ben-hadadi mwanawe alitawala mahali pake. 25Mfalme Yehoashi alimshinda Ben-hadadi mara tatu na kuikomboa miji yote iliyotekwa wakati wa utawala wa Yehoahazi, baba yake Yehoashi.



2Wafalme13;1-25


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: