Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday, 24 April 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Wafalme 14......




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana..
Tumshukuru Mungu wetu katika yote...!!

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu,Muumba wa Mbingu na Nchi
Mfalme wa amani,Mungu mwenye nguvu,Mungu wa walio hai,
Mungu wa Abrahamu ,Isaka na Yakobo...
Baba wa huruma,Baba wa baraka,Baba wa upendo..
Muweza wa yote Alfa na Omega...!!

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha
kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...
Sifa na Utukufu tunakurudishia wewe ee Mungu wetu...!!


Siku moja, saa tisa alasiri, Petro na Yohane walikuwa wakienda hekaluni, wakati wa sala. Wakati huo watu walikuwa wanambeba mtu mmoja kiwete tangu kuzaliwa. Watu hao walikuwa wakimweka huyo mtu kila siku kwenye mlango wa hekalu uitwao “Mlango Mzuri,” ili aombe chochote kwa wale waliokuwa wakiingia hekaluni. Alipowaona Petro na Yohane wakiingia hekaluni, aliwaomba wampe chochote. Petro na Yohane walimkodolea macho, naye Petro akamwambia, “Tutazame!” Naye akawageukia, akitazamia kupata kitu kutoka kwao. Kisha Petro akamwambia, “Sina fedha wala dhahabu, lakini kile nilicho nacho nitakupa. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, tembea!” Halafu, akamshika mkono wa kulia, akamwinua. Papo hapo miguu na magoti yake yakapata nguvu. Akaruka, akasimama na kuanza kutembea. Halafu akaingia pamoja nao hekaluni, akitembea na kurukaruka huku akimtukuza Mungu. Watu wote waliokuwa hapo walimwona akitembea na kumsifu Mungu. Walipomtambua kuwa ndiye yule aliyekuwa anaombaomba karibu na ule “Mlango Mzuri” wa hekalu, wakashangaa mno hata wasiweze kuelewa yaliyompata.
Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na 
kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza
 kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah tunaomba utuepushe katika majaribu Mungu wetu
utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni
tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona...


Watu wote, wakiwa na mshangao mkubwa, wakaanza kukimbilia mahali palipoitwa “Ukumbi wa Solomoni,” ambapo yule mtu alikuwa bado anaandamana na Petro na Yohane. Basi, Petro alipowaona watu hao akawaambia, “Wananchi wa Israeli, kwa nini mnashangazwa na jambo hili? Mbona mnatukodolea macho kana kwamba ni kwa nguvu zetu au utakatifu wetu sisi wenyewe tumemfanya mtu huyu aweze kutembea? Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo, Mungu wa babu zetu amemtukuza mtumishi wake Yesu. Yeye ndiye yuleyule mliyemtia mikononi mwa wakuu na kumkataa mbele ya Pilato hata baada ya Pilato kuamua kumwacha huru. Alikuwa mtakatifu na mwema; lakini nyinyi mlimkataa, mkataka mtu mwingine aliyekuwa muuaji afunguliwe. Basi, mlimuua yule ambaye ni chanzo cha uhai. Lakini Mungu alimfufua, na sisi ni mashahidi wa tukio hilo. Jina la Yesu na imani katika jina hilo ndivyo vilivyompa nguvu mtu huyu mnayemwona na kumfahamu. Imani kwa Yesu ndiyo iliyomponya kabisa mtu huyu kama mnavyoona nyote. “Sasa ndugu zangu, mnafahamu kwamba nyinyi na wakuu wenu mlitenda hayo kwa sababu ya kutokujua kwenu. Lakini ndivyo Mungu alivyotimiza yale aliyotangaza zamani kwa njia ya manabii wote, kwamba ilikuwa lazima Kristo wake ateseke. Basi, tubuni, mkamrudie Mungu ili yeye afute dhambi zenu. Fanyeni hivyo ili Bwana awape nyakati za kuburudika rohoni na kuwaletea yule Kristo aliyemteua ambaye ndiye Yesu.

Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Mungu wetu nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu ukatupe kama
inavyokupendeza wewe...

Mungu wetu tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo
vimiliki,Mungu wetu  tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Yahweh tunaomba ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana
wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Yahweh tukawe salama rohoni
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kutambua mema na mabaya,Jehovah ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti
yako na kuitii,Yahweh tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Baba wa Mbinguni tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku 
zote za maisha yetu,Jehovah ukaonekane katika maisha yetu
Mungu wetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Baba wa
Mbinguni,Neema yako na Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Upendo ukadumnu kati yetu,Utu wema na fadhili vikawe nasi..
Mungu wetu ukatufanye chombo chema Yahweh nasi tukatumike
kama inavyokupendeza wewe...
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Ni lazima yeye abaki huko mbinguni mpaka utakapofika wakati wa kurekebishwa vitu vyote, kama Mungu alivyosema kwa njia ya manabii wake watakatifu wa tangu zamani. Kwa maana Mose alisema, ‘Bwana Mungu wenu atawapelekeeni nabii kama mimi kutoka kati yenu nyinyi wenyewe. Yeyote yule ambaye hatamsikiliza nabii huyo atatengwa mbali na watu wa Mungu na kuangamizwa.’ Manabii wote, kuanzia Samueli na wale waliomfuata, walitangaza habari za mambo haya ambayo yamekuwa yakitendeka siku hizi. Ahadi zile Mungu alizotoa kwa njia ya manabii ni kwa ajili yenu; na mnashiriki lile agano Mungu alilofanya na babu zenu, kama alivyomwambia Abrahamu: ‘Kwa njia ya wazawa wako, jamaa zote za dunia zitabarikiwa.’ Basi, Mungu alimfufua mtumishi wake kwa faida yenu kwanza, akamtuma awaleteeni baraka kwa kumfanya kila mmoja wenu aachane kabisa na maovu yake.”

Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako watoto wako
wanaokutafuta/kukuomba kwa bidii na imani
Yahweh tunaomba ukawaguse kwa mkmono wako wenye nguvu
Jehovah ukawatendee kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao Baba wa Mbinguni
tunaomba ukawafute machozi yao
Jehovah ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
Mungu wetu wakasimamie Neno lako nalo likawaweke huru
Yahweh tunaomba ukasikie na ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na utukufu hata Milele
Amina..!!

Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana kwakunisoma
Mungu Baba akawabariki na kuwatendea sawasawa na 
mapenzi yake....
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo wa Mungu Baba
Ukae nanyi Daima...
Nawapenda.

Mfalme Amazia wa Yuda

(2Nya 25:1-24)

1Katika mwaka wa pili wa enzi ya Yehoashi mwana wa Yehoahazi huko Israeli, Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda alianza kutawala. 2Alipoanza kutawala alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano, naye alitawala katika Yerusalemu kwa muda wa miaka ishirini na tisa. Mama yake aliitwa Yehoadani wa Yerusalemu. 3Alitenda yaliyo mema mbele ya Mwenyezi-Mungu, lakini hakuwa kama babu yake Daudi. Bali alifanya mambo yote kama Yoashi baba yake; 4isipokuwa mahali pa ibada milimani hapakuharibiwa na watu waliendelea kutambika na kufukiza ubani mahali hapo.
5Mara tu Amazia alipojiimarisha mamlakani, aliwaua watumishi waliomuua mfalme, baba yake. 6Lakini hakuwaua watoto wa wauaji; kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Sheria za Mose, Mwenyezi-Mungu anapotoa amri akisema, “Wazazi hawatauawa kwa ajili ya watoto wao, wala watoto hawatauawa kwa ajili ya wazazi wao; bali kila mtu atauawa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe.”
7Amazia aliwaua Waedomu 10,000 katika Bonde la Chumvi; aliutwaa kwa nguvu mji wa Sela na kuuita Yoktheeli, na hivi ndivyo unavyoitwa mpaka sasa.
8Kisha Amazia akatuma wajumbe kwa Yehoashi mwana wa Yehoahazi, mwana wa Yehu mfalme wa Israeli akisema, “Njoo tupambane.” 9Lakini Yehoashi mfalme wa Israeli alimpelekea ujumbe Amazia mfalme wa Israeli, akisema, “Siku moja mbaruti wa Lebanoni uliuambia mwerezi, wa huko Lebanoni pia, ‘Mwoze binti yako kwa mwanangu.’ Lakini mnyama wa mwituni akapita hapo na kuukanyagakanyaga mbaruti huo. 10Sasa wewe Amazia umewashinda kabisa Waedomu, na moyo wako unakufanya ujivune. Ridhika na utukufu wako, ukakae nyumbani; ya nini kujitafutia taabu zitakazokuangamiza wewe mwenyewe pamoja na watu wako wa Yuda?”
11Lakini Amazia hakujali. Kwa hiyo Yehoashi mfalme wa Israeli alitoka akakabiliana uso kwa uso na Amazia huko vitani Beth-shemeshi, nchini Yuda. 12Watu wa Yuda walishindwa na watu wa Israeli na kila mmoja alirudi kwake. 13Yehoashi mfalme wa Israeli alimteka Amazia mfalme wa Yuda, mwana wa Yehoashi, mwana wa Ahazia huko Beth-shemeshi; halafu akauendea Yerusalemu na kuubomoa ukuta wake kutoka Lango la Efraimu mpaka Lango la Pembeni, umbali wa karibu mita 200. 14Alichukua dhahabu yote na fedha, hata na vifaa vyote vilivyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na katika hazina ya ikulu; pia alichukua mateka,14:14 mateka: Kiebrania “wana wa dhamana”. kisha akarudi Samaria. 15Matendo mengine yote ya Yehoashi, ushujaa wake na vita alivyopigana na mfalme Amazia wa Yuda yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli. 16Yehoashi alifariki, akazikwa katika makaburi ya kifalme huko Samaria. Mwanae, Yeroboamu akatawala mahali pake.

Kifo cha mfalme Amazia wa Yuda

(2Nya 25:25-28)

17Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda aliishi miaka kumi na mitano baada ya mfalme Yehoashi wa Israeli kufariki. 18Matendo mengine yote ya Amazia yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda.
19Njama za kumwua Amazia zilifanywa Yerusalemu, kwa hiyo alikimbilia Lakishi, lakini maadui walituma watu wa kumwua huko. 20Maiti yake ililetwa juu ya farasi na kuzikwa katika makaburi ya kifalme katika Yerusalemu katika mji wa Daudi. 21Kisha watu wote wa Yuda wakamchukua Azaria14:21 Azariya: Au Uzia. akiwa na umri wa miaka kumi na sita, wakamtawaza mahali pa Amazia baba yake. 22Azaria, baada ya kifo cha baba yake, aliujenga upya mji wa Elathi na kuurudisha kwa Yuda.

Mfalme Yeroboamu wa pili wa Israeli

23Katika mwaka wa kumi na tano wa enzi ya Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda, Yeroboamu mwana wa Yehoashi mfalme wa Israeli alianza kutawala huko Samaria, akatawala kwa muda wa miaka arubaini na mmoja. 24Alimwasi Mwenyezi-Mungu akafuata mfano wa mtangulizi wake mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati, aliyewapotosha watu wa Israeli wakatenda dhambi. 25Aliikomboa nchi yote iliyokuwa mali ya Israeli, kutoka Pito la Hamathi mpaka Bahari ya Araba. Hivi ndivyo alivyoahidi Mwenyezi-Mungu kwa njia ya mtumishi wake Yona mwana wa Amitai, nabii, kutoka Gath-heferi. 26Maana Mwenyezi-Mungu aliona taabu kubwa kwa waliyopata Waisraeli kwani hapakuwa na mtu yeyote wa kuwasaidia. 27Lakini Mwenyezi-Mungu hakuwa amesema ya kwamba ataangamiza Israeli kabisa, hivyo aliwaokoa kwa njia ya mfalme Yeroboamu mwana wa Yehoashi.
28Matendo mengine yote ya Yeroboamu, vita alivyopigana kwa ushujaa, na jinsi alivyoikomboa Damasko na Hamathi na kuifanya mali ya Israeli, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli. 29Yeroboamu alifariki na kuzikwa katika makaburi ya kifalme na mwanawe Zekaria akatawala mahali pake.


2Wafalme14;1-29


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.


No comments: