Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday, 26 April 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Wafalme 16......




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Haleluyah ni siku nyingine tena Mungu wetu ametuchagua
na  ametupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana,wala si kwamba sisi
ni wazuri mno,si kwa nguvu zetu wala si kwa uwezo wetu,
si kwa akili zetu wala si kwa utashi wetu sisi kuwa hivi
tulivyo leo hii...
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu ....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Utukuzwe ee Mungu wetu,Mungu mwenye nguvu,Mungu mwenye upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...!
Sifa na Utukufu tunakuridishia Baba wa Mbinguni....

Kulikuwa na mtu mmoja huko Kaisarea aitwaye Kornelio, jemadari wa kikosi kimoja kiitwacho “Kikosi cha Italia.” Alikuwa mtu mwema; naye pamoja na jamaa yake yote walimcha Mungu; alikuwa anafanya mengi kusaidia maskini wa Kiyahudi na alikuwa anasali daima. Yapata saa tisa alasiri, aliona dhahiri katika maono malaika wa Mungu akiingia ndani na kumwambia, “Kornelio!” Kornelio alimkodolea macho huyo malaika kwa hofu, akamwambia, “Kuna nini Mheshimiwa?” Huyo malaika akamwambia, “Mungu amezipokea sala na sadaka zako kwa maskini wala hatazisahau. Sasa, watume watu Yopa wakamwite mtu mmoja aitwaye Simoni, kwa jina lingine Petro. Yeye yumo nyumbani kwa Simoni mtengenezaji wa ngozi ambaye nyumba yake iko karibu na bahari.” Huyo malaika aliyesema hayo alipokwisha kwenda zake, Kornelio aliwaita watumishi wawili wa nyumbani na mmoja wa askari zake ambaye alikuwa mcha Mungu, akawaeleza yote yaliyotukia, akawatuma Yopa.


Tazama jana imepita Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku
nyingine..
Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha 
na kujiachilia mikononi mwako
Yahweh tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza 
kuwasamehe wale wote waliotukosea
Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu Yahweh utuokoe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu 
Yesu Kristo wa Nazareti,yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona


Kesho yake, hao watu watatu wakiwa bado safarini, lakini karibu kufika Yopa, Petro alipanda juu ya paa la nyumba yapata saa sita mchana ili kusali. Aliona njaa, akatamani kupata chakula. Chakula kilipokuwa kinatayarishwa, akaota ndoto. Aliona mbingu zimefunguliwa na kitu kama shuka kubwa inateremshwa chini ikiwa imeshikwa pembe zake nne. Ndani ya shuka hiyo kulikuwa na kila aina ya wanyama: Wanyama wenye miguu minne, wanyama watambaao na ndege wa angani. Akasikia sauti ikimwambia: “Petro, amka uchinje, ule!” Petro akajibu, “La, Bwana; mimi sijaonja kamwe chochote ambacho ni najisi au kichafu.” Ile sauti ikasikika tena ikimwambia: “Usiviite najisi vitu ambavyo Mungu amevitakasa!” Jambo hili lilifanyika mara tatu, kisha ile shuka ikarudishwa juu mbinguni.


Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Yahweh nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji
Yaweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu ukatupe
kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu
familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Jehovah ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Yahweh ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu
Kristo...
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia ,Jehovah ukaonekane
katika maisha yetu
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni Yahweh ukatupe macho
ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Mungu wetu ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako 
siku zote za maisha yetu...
neema yako na Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Mfalme wa amani amani ikatawale  na upendo ukadumu kati yetu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inayokupendeza wewe...
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Petro alipokuwa bado anashangaa juu ya maana ya hayo maono aliyokuwa ameyaona, wale watu waliotumwa na Kornelio, baada ya kuigundua nyumba ya Simoni, walifika mlangoni, wakaita kwa sauti: “Je, kuna mgeni humu aitwaye Simoni Petro?” Petro alikuwa bado anajaribu kuelewa yale maono, na hapo Roho akamwambia, “Sikiliza! Kuna watu watatu hapa, wanakutafuta. Shuka upesi na wala usisite kwenda pamoja nao kwa maana ni mimi niliyewatuma.” Basi, Petro akateremka chini, akawaambia hao watu, “Mimi ndiye mnayemtafuta. Kwa nini mmekuja?” Wao wakamjibu, “Jemadari Kornelio ambaye ni mtu mwema, mcha Mungu na mwenye kuheshimika mbele ya Wayahudi wote, ametutuma. Aliambiwa na malaika mtakatifu akualike nyumbani kwake ili asikilize chochote ulicho nacho cha kusema.” Petro akawakaribisha ndani, akawapa mahali pa kulala usiku ule. Kesho yake, Petro alianza safari pamoja nao, na baadhi ya ndugu wa huko Yopa walifuatana naye.


Yahweh tazama watoto wako wanaokutafuta/kukuomba kwa 
bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Jehovah tunaomba ukawatendee kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni ukaonekane katika maisha yao
Mungu wetu ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Yahweh ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao Baba wa Mbinguni
ukawafute machozi yao...
Jehovah tunaomba ukasikie na ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!

Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana kwakuwanami/kunisoma
Mungu wetu mwenye nguvu akawabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye...
Nawapenda.


Mfalme Ahazi wa Yuda

(2Nya 28:1-27)

1Katika mwaka wa kumi na saba wa enzi ya Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli, Ahazi mwana wa Yothamu mfalme wa Yuda alianza kutawala. 2Alikuwa na umri wa miaka ishirini alipoanza kutawala. Alitawala kwa muda wa miaka kumi na sita huko Yerusalemu. Hakufanya mema mbele ya Mwenyezi-Mungu kama Daudi babu yake alivyofanya, 3bali alifuata mienendo ya wafalme wa Israeli. Isitoshe, hata alimpitisha mwanawe motoni kuwa tambiko, akifuata desturi mbaya za mataifa ambayo yalifukuzwa na Mwenyezi-Mungu Waisraeli walipokuwa wanaingia nchini. 4Ahazi alitoa sadaka na kufukiza ubani mahali pa juu, vilimani na chini ya kila mti mbichi.
5Kisha Resini mfalme wa Aramu na Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli walitokea ili kupigana vita dhidi ya Yerusalemu, nao walimzingira Ahazi, lakini hawakuweza kumshinda. 6(Wakati huo, mfalme wa Edomu aliuteka akawarudishia Waedomu mji wa Elathi na kuwafukuza watu wa Yuda waliokaa humo. Nao Waedomu wakaingia Elathi na kufanya makao yao huko mpaka sasa.) 7Basi Ahazi akatuma watu kwa mfalme Tiglath-pileseri wa Ashuru wakiwa na ujumbe huu: “Mimi ni mtumishi wako mwaminifu. Njoo uniokoe kutoka kwa wafalme wa Aramu na Israeli ambao wananishambulia.” 8Ahazi akachukua fedha na dhahabu iliyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na hazina iliyokuwa katika nyumba ya mfalme na kumpelekea kama zawadi mfalme wa Ashuru. 9Tiglath-pileseri, akiitikia ombi la Ahazi, aliushambulia mji wa Damasko na kuuteka. Akamuua mfalme Resini na kuwapeleka mateka Kiri.
10Mfalme Ahazi alipokwenda Damasko kukutana na mfalme Tiglath-pileseri, aliona madhabahu huko. Basi, akamtumia kuhani Uria mfano kamili na mchoro wa madhabahu hiyo. 11Uria akajenga madhabahu hiyo kulingana na mfano huo na kuimaliza kabla ya Ahazi kurejea nyumbani. 12Ahazi aliporejea kutoka Damasko, aliiona hiyo madhabahu; basi akaikaribia madhabahu na kutoa sadaka juu yake. 13Alitoa sadaka yake ya kuteketezwa, ya nafaka, na ya kinywaji, akanyunyiza damu ya sadaka ya amani. 14Madhabahu ya shaba ambayo iliwekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu, aliiondoa mbele ya nyumba kutoka nafasi yake katikati ya madhabahu yake na nyumba ya Mwenyezi-Mungu, akaiweka kwenye nafasi iliyokuwa upande wa kaskazini wa madhabahu yake. 15Kisha alimwamuru Uria, “Tumia hii madhabahu yangu kubwa kwa kuteketeza sadaka za asubuhi na sadaka za nafaka za jioni, sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka za mfalme na za watu wote na pia sadaka za divai za watu. Irashie damu ya wanyama wote wa kuteketezwa ambao wametolewa sadaka. Lakini ile madhabahu ya shaba nitaitumia mimi kwa kuuliza kauli ya Mungu.” 16Naye Uria akafuata maagizo ya mfalme.
17Mfalme Ahazi aliziondoa papi zilizokuwa zimesimamishwa huko, akaondoa birika lililoitwa bahari ambalo lilikuwa juu ya wale fahali kumi na wawili wa shaba na kuliweka juu ya msingi wa mawe. 18Nalo jukwaa lililotumika siku ya Sabato lililokuwa limejengwa ndani ya nyumba pamoja na kivutio cha nje, mfalme alivihamisha kutoka katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu kwa ajili ya mfalme wa Ashuru.
19Matendo mengine yote ya mfalme Ahazi yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda. 20Ahazi akafa na kuzikwa katika makaburi ya kifalme katika mji wa Daudi, naye Hezekia mwanawe akatawala mahali pake.



2Wafalme16;1-20


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: