Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday, 27 April 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Wafalme 17......




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana...
Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo,vinavyoonekana na visivyoonekana..
Mungu mwenye nguvu,Mungu mwenye huruma,Mungu wa wote walio hai,
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Baba wa Upendo,Baba wa Baraka,Baba wa uzima,Baba wa yote..
Wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho,Alfa na Omega....

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha 
kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu
Neema yako yatutosha ee Mungu wetu
Sifa na Utukufu tunakurudishia Baba wa Mbinguni...!!


Siku ya pili yake walifika Kaisarea na huko Kornelio alikuwa anawangojea pamoja na jamaa na marafiki aliokuwa amewaalika. Petro alipokuwa anaingia, Kornelio alitoka nje kumlaki, akapiga magoti mbele yake na kuinama chini kabisa. Lakini Petro alimwinua, akamwambia, “Simama, kwa maana mimi ni binadamu tu.” Petro aliendelea kuongea na Kornelio wakiwa wanaingia nyumbani ambamo aliwakuta watu wengi wamekusanyika. Petro akawaambia, “Nyinyi wenyewe mnajua kwamba Myahudi yeyote amekatazwa na sheria yake ya dini kushirikiana na watu wa mataifa mengine. Lakini Mungu amenijulisha nisimfikirie mtu yeyote kuwa najisi au mchafu. Kwa sababu hiyo, mliponiita nimekuja bila kusita. Basi, nawaulizeni: Kwa nini mmeniita?” Kornelio akasema, “Siku tatu zilizopita saa kama hii, saa tisa alasiri, nilikuwa nikisali chumbani mwangu. Ghafla, mtu aliyekuwa amevaa mavazi yenye kungaa alisimama mbele yangu, akasema: ‘Kornelio! Sala yako na sadaka zako kwa maskini zimekubaliwa na Mungu. Mtume mtu Yopa akamwite mtu mmoja aitwaye Simoni, kwa jina lingine Petro; yuko nyumbani kwa Simoni mtengenezaji wa ngozi karibu na bahari.’ Kwa hiyo nilikutumia ujumbe bila kuchelewa, nawe umefanya vyema kuja. Sasa, sisi tuko mbele ya Mungu, kusikiliza chochote ambacho Bwana amekuamuru kusema.”


Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na
kujiachilia mikononi mwako
Yahweh tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea
Baba wa Mbinguni usitutie katika majaribu Mungu wetu tunaomba
utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Jehovah utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona


Hapo Petro akaanza kusema: “Sasa nimetambua kwamba hakika Mungu hana ubaguzi. Mtu wa taifa lolote anayemcha Mungu na kutenda yaliyo sawa anapokelewa naye. Huu ndio ule ujumbe Mungu alioupeleka kwa watu wa Israeli, akitangaza Habari Njema iletayo amani kwa njia ya Yesu Kristo ambaye ni Bwana wa wote. Nyinyi mnajua jambo lililotukia katika nchi yote ya Wayahudi kuanzia Galilaya baada ya ule ubatizo aliohubiri Yohane. Mnamjua Yesu wa Nazareti na jinsi Mungu alivyomteua kwa kummiminia Roho Mtakatifu na nguvu. Mungu alikuwa pamoja naye; yeye alikwenda huko na huko akitenda mema na kuwaponya wote waliokuwa wamevamiwa na Ibilisi. Sisi ni mashahidi wa mambo yote aliyotenda katika nchi ya Wayahudi na katika Yerusalemu. Walimuua kwa kumtundika msalabani; lakini Mungu alimfufua siku ya tatu, akamfanya aonekane, si kwa watu wote, ila kwa wale Mungu aliokwisha wachagua wawe mashahidi wake, yaani sisi tuliokula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu. Alituamuru kuihubiri Habari Njema kwa watu wote na kushuhudia kwamba yeye ndiye aliyeteuliwa na Mungu awe Mwamuzi wa walio hai na wafu. Manabii wote waliongea juu yake kwamba kila mtu atakayemwamini atasamehewa dhambi zake zote kwa jina lake.”


Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Mungu wetu tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu
ukatupe kama inavyokupendeza wewe....


Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Jehovah tunaomba ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinmguni tukawe salama rohoni
Yahweh ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako
na kuitii,Mungu wetu tunaomba ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya,Yahweh tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Mungu wetu tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu,Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu,Baba wa Mbinguni ukaonekane katika maisha yetu Yahweh popote
tupitapo na ikajulikane kwamba upo Mungu wetu
Neema yako na Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu..
Baba wa Mbinguni ukatufanye chombo chema Jehovah nasi tukatumike
kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Wakati Petro alipokuwa bado anasema maneno hayo, Roho Mtakatifu aliwashukia wote waliokuwa wanasikiliza ujumbe huo. Wale Wayahudi waumini waliokuja pamoja na Petro kutoka Yopa walishangaa kuona kuwa Mungu aliwamiminia kipawa cha Roho Mtakatifu watu wa mataifa mengine pia; maana waliwasikia wakiongea kwa lugha mbalimbali wakimtukuza Mungu. Hapo Petro akasema, “Watu hawa wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi wenyewe tulivyompokea. Je, kuna yeyote atakayeweza kuwazuia wasibatizwe kwa maji?” Basi, akaamuru wabatizwe kwa jina la Yesu Kristo. Kisha wakamwomba akae nao kwa siku chache.
Yahweh tazama watoto wako wanaokutafuta/kukuomba 
kwa bidii na imani Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono
wako wenye nguvu,Jehovah ukaonekane katika shida/mahitaji yao
kila mmoja na haja zake,Baba wa Mbinguni tuomba ukasikie kulia
kwao Mungu wetu tunaomba ukawafute machozi yao
Yahweh ukawasamehe pale walikwenda kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako
na kusimamia Neno lako nalo likawaweke huru
Ee Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu Baba wa Mbinguni
ukapokee sala/maombi yetu Jehovah ukawatendee sawasawa na 
mapenzi yako...
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina...!

Wapendwa/waungwana asanteni sana kwakuwanami/kunisoma
Mungu wetu mwenye nguvu akawatendee sawasawa na mapenzi yake
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba ukawe
nanyi daima..

Nawapenda.

Mfalme Hoshea wa Israeli

1Katika mwaka wa kumi na mbili wa enzi ya mfalme Ahazi wa Yuda, Hoshea mwana wa Ela alianza kutawala Israeli, akatawala huko Samaria kwa miaka tisa. 2Alitenda dhambi mbele ya Mwenyezi-Mungu ingawa siyo kama wafalme wa Israeli waliomtangulia. 3Mfalme Shalmanesa wa Ashuru alimshambulia; naye Hoshea akawa mtumishi wake na kumlipa ushuru. 4Lakini wakati mmoja Hoshea alituma wajumbe kwa mfalme wa Misri akiomba msaada; ndipo akaacha kulipa ushuru kwa mfalme Shalmanesa wa Ashuru kama alivyozoea kufanya kila mwaka. Shalmanesa alipoona hivi alimfunga Hoshea kwa minyororo na kumweka gerezani.

Kushindwa kwa Samaria

5Kisha mfalme wa Ashuru akaivamia nchi nzima na kuufikia mji wa Samaria na kuuzingira kwa muda wa miaka mitatu. 6Katika mwaka wa tisa wa utawala wa Hoshea, mfalme wa Ashuru aliuteka Samaria, na kuwachukua watu wa Israeli mateka mpaka Ashuru, baadhi yao akawaweka katika mji wa Hala, wengine karibu na mto Habori, mto Gozani na wengine katika miji ya Media.
7Haya yote yalitendeka kwa sababu watu wa Israeli walimwasi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, ambaye aliwatoa kutoka mikononi mwa mfalme wa Misri, pia waliabudu miungu mingine, 8na kufuata njia za mataifa ambayo Mwenyezi-Mungu aliyafukuza mbele ya Waisraeli, na kufanya matendo ya wafalme wa Israeli waliyoyaingiza nchini. 9Watu wa Israeli walitenda kwa siri mambo yasiyokuwa mema mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. Walijenga mahali pa juu pa kuabudia miungu ya uongo katika kila mji, kuanzia mnara wa walinzi mashambani hadi katika mji wenye ngome. 10Juu ya kila kilima na chini ya kila mti wenye majani mabichi, walijenga nguzo za mawe na sanamu za mungu wa kike Ashera, 11na wakafukiza ubani kwenye madhabahu zote za miungu ya uongo kufuatia desturi za mataifa ambayo yalifukuzwa na Mwenyezi-Mungu. Walimkasirisha Mwenyezi-Mungu kwa matendo yao maovu, 12na walitumikia sanamu ambazo Mwenyezi-Mungu alikuwa amewakataza, akisema, “Msifanye hivyo.”
13Mwenyezi-Mungu alituma manabii na waonaji kuionya Israeli na Yuda akisema, “Acheni njia zenu mbaya mkatii amri zangu na maagizo yangu kufuatana na sheria nilizowapa babu zenu, na ambazo niliwapeni kupitia kwa watumishi wangu manabii.” 14Lakini wao hawakutii; walikuwa wagumu kama babu zao ambao hawakumwamini Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. 15Walikataa kutii maagizo yake; hawakushika agano alilofanya na babu zao; licha ya kupuuza maonyo yake, waliabudu sanamu zisizokuwa na maana mpaka hata wao wenyewe hawakuwa na maana tena; walifuata desturi za mataifa yaliyowazunguka: Walipuuza amri za Mwenyezi-Mungu; wala hawakuzizingatia. 16Walivunja amri zote za Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, wakatengeneza sanamu za miungu ya ndama wawili wa kusubu; vilevile wakatengeneza sanamu za mungu wa kike Ashera wakaabudu na vitu vyote vya angani na wakamtumikia Baali. 17Waliwatambika watoto wao wa kiume na wa kike kwa miungu ya uongo; wakataka shauri kwa watabiri na wachawi. Walinuia kabisa kutenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, wakamkasirisha sana. 18Basi, Mwenyezi-Mungu akawakasirikia sana watu wa Israeli na kuwafukuza kabisa mbele yake; hakuacha mtu isipokuwa kabila la Yuda peke yake.
19Lakini hata watu wa Yuda hawakutii amri za Mwenyezi-Mungu, Mungu wao; bali walifuata desturi zilizoletwa na watu wa Israeli. 20Mwenyezi-Mungu aliwakataa Waisraeli wote; akawaadhibu na kuwaacha mikononi mwa adui wakali, na kisha akawafukuza mbele yake. 21Baada ya Mwenyezi-Mungu kutenga watu wa Israeli kutoka ukoo wa Daudi, walimtawaza Yeroboamu mwana wa Nebati kuwa mfalme. Naye Yeroboamu aliwafanya watu wa Israeli kumwacha Mwenyezi-Mungu na kutenda dhambi kubwa sana. 22Waisraeli walitenda dhambi alizotenda Yeroboamu; hawakuweza kuziacha, 23hadi hatimaye Mwenyezi-Mungu akawafukuza kutoka mbele yake, kama vile alivyokuwa amesema kupitia kwa watumishi wake wote manabii. Kwa hiyo watu wa Israeli walichukuliwa mateka kutoka nchi yao wenyewe mpaka Ashuru ambako wanakaa hata sasa.

Waashuru wafanya makao yao Israeli

24Kisha mfalme wa Ashuru akachukua watu kutoka Babuloni, Kutha, Ava, Hamathi na Sefarvaimu na kuwaweka katika miji ya Samaria mahali pa watu wa Israeli waliopelekwa uhamishoni. Wakaitwaa miji hiyo na kukaa humo. 25Basi ilitokea kwamba walipoanza kukaa humo, hawakumwabudu Mwenyezi-Mungu, kwa hiyo Mwenyezi-Mungu akatuma simba miongoni mwao, nao wakawaua baadhi yao. 26Halafu watu walimwambia mfalme wa Ashuru, “Mataifa uliyochukua na kuyaweka katika miji ya Samaria hayakujua hukumu za Mungu wa nchi hiyo, kwa hiyo Mungu huyo alituma simba ambao wanawaua.” 27Ndipo mfalme wa Ashuru akaamuru, “Mrudishe kuhani mmoja kati ya wale tuliowaleta mateka; mrudishe aende na kukaa huko, ili awafundishe watu sheria ya Mungu wa nchi hiyo.” 28Kwa hiyo mmoja wa makuhani waliotekwa nyara toka Samaria alikwenda na kukaa Betheli, na huko aliwafundisha watu jinsi ya kumwabudu Mwenyezi-Mungu.
29Lakini mataifa yote katika miji yalimoishi yalijitengenezea miungu yao na kuiweka mahali pa juu ambako watu wa Samaria walikuwa wametengeneza. 30Watu wa Babuloni walitengeneza vinyago vya Sukoth-benothi; Wakuthi vinyago vya Nergali; Wahamathi vinyago vya Ashima; 31Waiva vinyago vya Nibhazi na Tartaki; na Wasefarvaimu walitoa watoto wao kuwa sadaka za kuteketezwa kwa miungu yao Adrameleki na Anameleki. 32Watu hawa vilevile walimwabudu Mwenyezi-Mungu. Waliteua kutoka kati yao watu wa kila aina na kuwafanya makuhani kutumika katika mahali pa juu na kutoa sadaka huko kwa niaba yao. 33Hivi walimwabudu Mwenyezi-Mungu, lakini wakati huohuo waliwaabudu pia miungu yao waliyoichukua kutoka nchi zao.
34Hata sasa wanatenda kama walivyofanya hapo awali. Hawamwabudu Mwenyezi-Mungu, na wala hawafuati masharti, maagizo, sheria au amri ambazo yeye Mwenyezi-Mungu aliwaamuru wana wa Yakobo; ambaye alimpa jina Israeli. 35Mwenyezi-Mungu alikuwa amefanya agano nao na kuwaamuru, “Msiabudu miungu mingine; msiisujudie, msiitumikie wala msiitambikie. 36Mtaniabudu mimi Mwenyezi-Mungu, ambaye niliwatoa huko Misri kwa uwezo na nguvu nyingi. Mtanisujudia mimi na kunitolea sadaka. 37Wakati wote mtatii masharti, maongozi, sheria na amri ambazo niliandika kwa ajili yenu, siku zote mtakuwa waangalifu kuzitenda. Msiiabudu miungu mingine, 38wala msisahau agano nililofanya nanyi; msiiabudu miungu mingine, bali 39mtaniabudu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nami nitawaokoa kutoka mikononi mwa adui zenu.” 40Lakini watu hao hawakusikiliza, bali waliendelea kutenda kama walivyofanya hapo awali.
41Basi mataifa haya yalimwabudu Mwenyezi-Mungu, lakini pia yalitumikia sanamu zao za kusubu; na mpaka sasa hivi, wazawa wao wanaendelea kutenda hivyo kama walivyotenda babu zao.



2Wafalme17;1-41


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: