Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday, 30 April 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Wafalme 18......



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki na ni mwisho wa mwezi huu wa 4
Mungu ametupa kibali cha kuendelea kuiona keo hii
Si kwamba sisi ni wema sana,si kwamba sisi ni wazuri mno
Si kwa uwezo wetu wala akili zetu si kwa nguvu zetu wala
utashi wetu ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake
Mungu wetu sisi kuwa hivi tuluvyo leo hii.....!!

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari
 kwa majukumu yetu..
Utukuzwe ee Mungu wetu,Unastahili sifa,unastahili kuabudiwa,
Unastahili kuhimidiwa....
Neema yako yatutosha Baba wa Mbinguni...!!


Nyamazeni mbele ya Bwana Mwenyezi-Mungu, kwani siku ya Mwenyezi-Mungu iko karibu. Mwenyezi-Mungu ameandaa tambiko, nao aliowaalika amewateua. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Katika siku ile ya karamu yangu, nitawaadhibu viongozi wa watu hao, kadhalika na wana wa mfalme pamoja na wote wanaoiga desturi za kigeni. Siku hiyo nitawaadhibu wote: Wanaoruka kizingiti cha nyumba kama wapagani, wanaojaza nyumba ya bwana wao vitu vya dhuluma na wizi. “Siku hiyo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, Kutasikika kilio kutoka Lango la Samaki, maombolezo kutoka Mtaa wa Pili, na mlio mkubwa kutoka milimani. Lieni enyi wakazi wa Makteshi! Wafanyabiashara wote wameangamia, wote wapimao fedha wamefutiliwa mbali. Wakati huo nitaupekua mji wa Yerusalemu kwa taa, nitawaadhibu wanaoishi wametulia kama machicha ya divai, wote ambao husema mioyoni mwao: ‘Mwenyezi-Mungu hatafanya kitu: Chema au kibaya.’
Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza
kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribuni Mungu wetu utuokoe na yule mwovu
na kazi zake zote
Ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni utufunike 
kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti 
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona...


Utajiri wao utanyakuliwa, na nyumba zao zitaachwa tupu! Watajijengea nyumba, lakini hawataishi humo. Watapanda mizabibu, lakini hawatakunywa divai yake.” Ile siku kubwa ya Mwenyezi-Mungu imekaribia, iko karibu na inakuja mbio. Mlio wa siku ya Mwenyezi-Mungu ni wa uchungu; hapo, shujaa atalia kwa sauti. Siku hiyo itakuwa siku ya ghadhabu, ni siku ya dhiki na uchungu, siku ya giza na huzuni; siku ya uharibifu na maangamizi, siku ya mawingu na giza nene. Siku hiyo ni ya mlio wa tarumbeta ya vita, dhidi ya miji yenye ngome na kuta ndefu. Kwa kuwa watu wamemkosea Mwenyezi-Mungu, yeye atawaletea dhiki kubwa, hivyo kwamba watatembea kama vipofu. Damu yao itamwagwa kama vumbi, na miili yao kama mavi. Fedha yao wala dhahabu yao havitaweza kuwaokoa katika siku hiyo ya ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu. Kwa moto wa wivu wake dunia yote itateketezwa. Kwa ukamilifu na kwa namna ya kutisha atawafanya wakazi wote duniani watoweke.

Jehovah tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Mungu wetu tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Yahweh nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Jehovah nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji
Mungu wetu  tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,
familia/ndungu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Jehovah tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki vyote tunavyoenda
kugusa/kutumia Mungu wetu ukavitakase na kuvifunika kwa Damu
ya Bwana wetu Yesu Kristo
Baba wa Mbinguni ukatamalaki na kutuatamia Yahweh tukawe 
salama rohoni Mungu wetu tunaomba ukatupe macho ya kuona na
masikio ya kusikia sauti yako na kuitii
Jehovah tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako Mungu wetu
tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
Baba wa Mbinguni ukatupe neema ya kutambua mema na mabaya
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na 
ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni
Neema yako na Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Kusanyikeni, kusanyikeni enyi taifa la watu wasio na aibu, kabla hamjapeperushwa mbali kama makapi, kabla haijawajia siku ya hasira kali ya Mwenyezi-Mungu, kabla haijawajia siku ya ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu. Mtafuteni Mwenyezi-Mungu enyi wanyenyekevu wote nchini, enyi mnaozitii amri zake. Tafuteni uadilifu, tafuteni unyenyekevu; labda mtaiepa siku ya ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu.

Yahweh tazama watoto wako wanaokutafuta/kukuomba kwa
bidii na imani,Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako
wenye nguvu,Jehovah tunaomba ukawatendee kila mmoja na mahitaji
yake,Mungu  wetu ukaonekane katika shida/tabu zao
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe,Jehovah tunaomba ukawape neema ya kujiombea,
Kufuata njia zako, waka simamie Neno lako nalo likawaweke huru
Yahweh tunaomba neema yako na Nuru ikaangze katika maisha yao
Jehovah ukasikie kulia kwao Mungu wetu ukawafute machozi yao
Baba wa Mbinguni tunaomba ukasikie na ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa waungwana kwakuwa nami/kunisoma
Baba wa Mbinguni aendelee kuwabariki katika maisha yenu
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukawe navyi daima....
Nawapenda.



Mfalme Hezekia wa Yuda

(2Nya 29:1-2; 31:1)

1Katika mwaka wa tatu wa enzi ya Hoshea mwana wa Ela, mfalme wa Israeli, Hezekia mwana wa Ahazi, mfalme wa Yuda, alianza kutawala; 2alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala. Alitawala miaka ishirini na tisa huko Yerusalemu. Mama yake alikuwa Abi, binti wa Zekaria. 3Alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu, kama alivyofanya Daudi babu yake. 4Aliharibu mahali pote pa juu pa kuabudia miungu ya uongo na kuvunja nguzo za kutambikia na za mungu Ashera. Kadhalika, alivunja nyoka wa shaba ambaye Mose alimtengeneza, aliyeitwa Nehushtani. Mpaka wakati huo, watu wa Israeli walikuwa wakiitambikia. 5Hezekia alimtegemea Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli; hakuna aliyekuwa kama yeye kati ya wafalme wa Yuda waliomfuata au waliomtangulia. 6Yeye hakumwasi Mwenyezi-Mungu wala hakuacha kumfuata, bali alishika amri za Mwenyezi-Mungu alizomwamuru Mose. 7Basi, Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja naye, na alimfanya kufaulu kwa kila alilotenda. Alimwasi mfalme wa Ashuru na kukataa kumtumikia. 8Aliwapiga Wafilisti mpaka mji wa Gaza na nchi iliyouzunguka, kuanzia mnara wa walinzi mpaka mji wenye ngome.
9Katika mwaka wa nne wa enzi ya Hezekia, ambao pia ulikuwa mwaka wa saba wa enzi ya Hoshea mwana wa Ela mfalme wa Israeli, Shalmanesa mfalme wa Ashuru alishambulia mji wa Samaria na kuuzingira. 10Mwishoni mwa mwaka wa tatu Waashuru waliuteka Samaria. Ilikuwa katika mwaka wa sita wa enzi ya Hezekia na pia mwaka wa tisa wa enzi ya Hoshea mfalme wa Israeli, Samaria ulipotekwa. 11Mfalme wa Ashuru aliwachukua watu wa Israeli mateka mpaka Ashuru na kuwaweka wengine wao katika mji wa Hala, na karibu ya Habori, mji wa Gozani, pia na wengine katika miji ya Media, 12kwa sababu Waisraeli hawakutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, bali walivunja agano lake, hata hawakusikia wala kutii yote Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, aliyowaamuru.

Waashuru watishia Yerusalemu

(2Nya 32:1-19; Isa36:1-22)

13Mnamo mwaka wa kumi na nne wa utawala wa mfalme Hezekia, mfalme Senakeribu wa Ashuru aliishambulia miji yote yenye ngome ya Yuda na kuiteka. 14Hezekia akatuma ujumbe kwa Senakeribu huko Lakishi na kumwambia, “Nimefanya makosa. Tafadhali, komesha mashambulio yako kwangu; nami nitalipa chochote utakacho.” Mfalme wa Ashuru akaagiza Hezekia amletee tani kumi za fedha na tani moja ya dhahabu. 15Hezekia akampelekea fedha yote iliyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na katika hazina za nyumba ya mfalme; 16kadhalika, alingoa dhahabu kutoka katika milango ya hekalu la Mwenyezi-Mungu na ile dhahabu ambayo yeye mwenyewe aliiweka kwenye mihimili ya mlango; yote akampelekea Senakeribu. 17Kisha mfalme wa Ashuru alimtuma jemadari mkuu, amiri mkuu, mkuu wa matowashi pamoja na jeshi kubwa kutoka Lakishi kwenda kwa mfalme Hezekia huko Yerusalemu. Walisafiri na kufika Yerusalemu. Nao walipowasili waliingia na kusimama karibu na mfereji wa bwawa lililoko upande wa juu katika barabara kuu inayoelekea Uwanda wa Dobi. 18Walipomwita mfalme Hezekia walilakiwa na Eliakimu mwana wa Hilkia, ambaye alikuwa msimamizi wa ikulu; Shebna, aliyekuwa katibu na Yoa mwana wa Asafu, mwandishi wa kumbukumbu za mfalme. 19Ndipo jemadari mkuu alipowaambia, “Mwambieni Hezekia, hivi ndivyo anavyosema mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru: Ni ujasiri wa namna gani huu unaouwekea matumaini? 20Je, unadhani kuwa maneno matupu ndiyo maarifa na nguvu katika vita? Ni nani unayemtegemea hata ukaniasi? 21Angalia, sasa, unategemea Misri, utete uliovunjika ambao utamchoma mkono yeyote atakayeutegemea. Hivyo ndivyo Farao mfalme wa Misri alivyo kwa wote wale wanaomtegemea.”
22“Lakini hata kama mkiniambia: ‘Tunamtegemea Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu’, Jueni kwamba ni Mungu huyohuyo ambaye Hezekia alipaharibu mahali pake pa juu na madhabahu zake, akawaambia watu wa Yuda na watu wa Yerusalemu waabudu tu mbele ya madhabahu iliyoko Yerusalemu. 23Basi, fanyeni mkataba na bwana wangu mfalme wa Ashuru, nami nitawapa farasi 2,000 kama mtaweza kupata wapandafarasi. 24Mwawezaje kumrudisha nyuma ofisa mmoja kati ya watumishi wa bwana wangu walio na cheo cha chini kabisa, wakati mnategemea Misri iwaletee magari na wapandafarasi?” 25Zaidi ya hayo, je, mnafikiri nimekuja bila amri ya Mwenyezi-Mungu ili kuishambulia na kuiangamiza nchi hii? Mwenyezi-Mungu ndiye aliyeniambia, “Ishambulie nchi hii na kuiangamiza!”
26Basi, Eliakimu mwana wa Hilkia, Shebna na Yoa wakamwambia huyo jemadari mkuu, “Tafadhali, sema nasi kwa lugha ya Kiaramu, maana tunaielewa; usiseme nasi kwa lugha ya Kiebrania; kwa kuwa watu walioko ukutani wanasikiliza.”
27Yule jemadari mkuu akawaambia, “Je, bwana wangu amenituma kutoa ujumbe huu kwa bwana wenu na kwenu tu? Je, hakunituma pia kwa watu wanaokaa ukutani ambao wamehukumiwa pamoja nanyi kula mavi yao wenyewe na kunywa mikojo yao wenyewe?” 28Kisha huyo mkuu wa matowashi akasimama, akapaza sauti na kusema kwa lugha ya Kiebrania, “Sikilizeni maneno ya mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru! 29Hivi ndivyo anavyosema mfalme: Msikubali Hezekia awadanganye, kwa sababu hataweza kuwaokoa mikononi mwa mfalme. 30Msikubali awashawishi ili mumtegemee Mwenyezi-Mungu akisema, ‘Mwenyezi-Mungu atatuokoa na mji huu hautatiwa mikononi mwa mfalme wa Ashuru.’ 31Msimsikilize Hezekia, maana mfalme wa Ashuru anasema, ‘Muwe na amani nami, na jisalimisheni kwangu. Hapo kila mmoja wenu ataweza kula matunda ya mzabibu wake mwenyewe, matunda ya mtini wake mwenyewe, na kunywa maji ya kisima chake mwenyewe, 32mpaka baadaye nitakapokuja na kuwapeleka mbali katika nchi kama hii yenu, nchi yenye nafaka na divai, nchi yenye mikate na mashamba ya mizabibu; nchi yenye mizeituni na asali, ili mpate kuishi, msije mkafa.’ Msimsikilize Hezekia anapowahadaa akisema, ‘Mwenyezi-Mungu atatuokoa.’ 33Je, kuna yeyote kati ya miungu ya mataifa aliyeokoa nchi yake kutoka mikononi mwa mfalme wa Ashuru? 34Je, iko wapi miungu ya Hamathi na Arpadi. Iko wapi miungu ya Sefarvaimu, Hena na Iva? Je, imeokoa Samaria mikononi mwangu? 35Ni nani miongoni mwa miungu ya nchi hizi aliyeokoa nchi zao mikononi mwangu hata Mwenyezi-Mungu aweze kuukoa mji wa Yerusalemu?”
36Lakini watu wote walinyamaza kimya, wala hawakumjibu neno, kama walivyoamriwa na mfalme Hezekia, akisema, “Msimjibu.” 37Kisha Eliakimu mwana wa Hilkia, Shebna katibu na Yoa mwana wa Asafu, mwandishi, wakamwendea Hezekia huku mavazi yao yakiwa yameraruka, wakamweleza maneno ya jemadari mkuu.



2Wafalme18;1-37


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: