Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday, 16 April 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Wafalme 8......




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana..
Ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua
na kutupa kibali cha kuendelea kuina leo hii...

Tumshukuru Mungu wetu katika yote....

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa uwepo,pumzi/uzima na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Utukuzwe ee Mungu wetu,Unastahili sifa Baba wa Mbinguni,
Unastahili kuabudiwa Yahweh,Unastahili kuhimidiwa Jehovah..
Matendo yako ni makuu mno,Matendo yako niya ajabu,Matendo yako yanatisha...
Neema yako yatutosha ee Mungun wetu...!!


Usihangaike kwa sababu ya waovu; usiwaonee wivu watendao mabaya. Maana hao watatoweka mara kama nyasi; watanyauka kama mimea mibichi. Mtumainie Mwenyezi-Mungu na kutenda mema, upate kuishi katika nchi na kuwa salama. Uitafute furaha yako kwa Mwenyezi-Mungu, naye atakujalia unayotamani moyoni. Mkabidhi Mwenyezi-Mungu maisha yako; mtumainie yeye naye atafanya kitu. Ataufanya wema wako ungae kama mwanga, na uadilifu wako kama jua la adhuhuri. Tulia mbele ya Mwenyezi-Mungu, mngojee kwa saburi; usihangaike juu ya wale wanaofanikiwa, watu wanaofaulu katika mipango yao mibaya.


Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
Kwakuwaza,Kwakunena,Kwakutenda,kwakujua/Kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie katika majaribu Baba wa Mbinguni tunaomba utuokoe
na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa mbinguni
utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona...


Epuka hasira wala usiwe na ghadhabu; usihangaike maana hiyo huzidisha ubaya. Watu watendao mabaya wataangamizwa, bali wanaomtumaini Mwenyezi-Mungu wataimiliki nchi. Bado kitambo kidogo, naye mwovu atatoweka; utamtafuta pale alipokuwa, wala hutamwona. Lakini wapole wataimiliki nchi, hao watafurahia wingi wa fanaka. Mwovu hula njama dhidi ya mwadilifu, na kumsagia meno kwa chuki. Lakini Mwenyezi-Mungu humcheka mwovu, kwani ajua mwisho wake u karibu. Waovu huchomoa panga na kuvuta pinde zao, wapate kuwaua maskini na fukara; wawachinje watu waishio kwa unyofu. Lakini panga zao zitawapenya wao wenyewe, na pinde zao zitavunjwavunjwa. Afadhali mali kidogo ya mtu mwadilifu kuliko utajiri wa watu waovu wengi. Maana nguvu za waovu zitavunjwa, lakini Mwenyezi-Mungu huwategemeza waadilifu. Mwenyezi-Mungu hutunza maisha ya watu waaminifu, na urithi wao utadumu milele. Hawataaibika zikifika nyakati mbaya; siku za njaa watakuwa na chakula tele. Lakini waovu wataangamia, maadui za Mwenyezi-Mungu watanyauka kama maua nyikani; naam, watatoweka kama moshi.


Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika
utendaji Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji,Jehovah tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu 
wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu
Familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Yahweh tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Jehovah ukavifunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo...
Baba wa Mbinguni ukatamalaki na kutuatamia Mungu wetu tukawe salama
rohoni Yahweh ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako
na kuitii,Mungu wetu tunaomba ukatupe neema ya kutamnbua mema na mabaya,Yahweh ukatupe neema ya kufuata njia zako Mungu wetu
tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zotye za maisha yetu..
Jehovah ukaonekane katika maisha yetu Mungu wetu popote
tupitapo na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni...
Ukatufanye chombo chema Jehovah nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe...
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Mtu mwovu hukopa bila kurudisha; lakini mwadilifu hutoa kwa ukarimu. Waliobarikiwa na Mwenyezi-Mungu wataimiliki nchi, lakini waliolaaniwa naye watafutiliwa mbali. Mwenyezi-Mungu huziongoza nyayo za mtu, humlinda yule ampendezaye. Ajapoanguka, haanguki akabaki chini, kwa sababu Mwenyezi-Mungu humtegemeza. Nilikuwa kijana na sasa ni mzee; kamwe sijaona mwadilifu ameachwa na Mungu, au watoto wake wakiombaomba chakula. Daima huwapa wengine kwa furaha na kukopesha, na watoto wake ni baraka. Achana na uovu, utende mema, nawe utaishi nchini daima; maana Mwenyezi-Mungu hupenda uadilifu, wala hawaachi waaminifu wake. Huwalinda hao milele; lakini wazawa wa waovu wataangamizwa. Waadilifu wataimiliki nchi, na wataishi humo milele. Mtu mwadilifu husema maneno ya hekima, kwa ulimi wake hunena yaliyo ya haki. Huizingatia moyoni mwake sheria ya Mungu wake; naye hatetereki katika mwenendo wake. Mtu mwovu humvizia mtu mwema na kujaribu kumuua; lakini Mwenyezi-Mungu hatamtia mtu mwema makuchani mwake, wala kumwacha apatilizwe akishtakiwa. Mtumainie Mwenyezi-Mungu na kushika njia yake, naye atakukuza uimiliki nchi, na kuwaona waovu wakiangamizwa. Nilimwona mwovu mdhalimu sana, alijiweka juu ya wote kama mierezi ya Lebanoni! Baadaye nikapita hapo, naye hakuwapo tena; nikamtafuta, lakini hakuonekana tena. Mwangalie mtu mwema, mtu mwadilifu; mtu anayependa amani hujaliwa wazawa. Lakini wakosefu wote wataangamizwa; na wazawa wao watafutiliwa mbali. Mwenyezi-Mungu huwaokoa waadilifu, na kuwalinda wakati wa taabu. Mwenyezi-Mungu huwasaidia na kuwaokoa; huwatoa makuchani mwa waovu na kuwaokoa, maana wanakimbilia usalama kwake.

Yahweh tazama watoto wako wanaokutafuta kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Jehovah tunaomba ukawaponye na kuwatendea kila mmoja na 
mahitaji yake Baba wa Mbinguni ukaonekane katika maisha yao
Jehovah ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Mungu wetu tunaomba ukawape neema ya kujiombea,kufuata
njia zako wakasimamie Neno lako nalo likawaweke huru
Yahweh nuru yako ikaangaze katika maisha yao Baba wa Mbinguni
ukasikie kulia kwao Mungu wetu tunaomba ukawafute machozi yao
Jehovah tunaomba ukasikie na ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami/kunisoma
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea sawasawa na mapenzi
yake,Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba ukawe nanyi Daima....
Nawapenda.

Mwanamke wa Shunemu arudi

1Elisha alikuwa amemwambia mwanamke aliyeishi Shunemu ambaye alikuwa amemfufua mwanawe, “Ondoka, na jamaa yako, uhamie ugenini kwa sababu Mwenyezi-Mungu ameleta njaa itakayokuwamo nchini kwa muda wa miaka saba.” Akamshauri ahame aende mahali pengine. 2Huyo mwanamke akaondoka akafanya kama mtu wa Mungu alivyosema akaenda pamoja na jamaa yake na kukaa kama mgeni katika nchi ya Filistia kwa miaka saba.
3Miaka saba ilipokwisha, alitoka Filistia akarudi Israeli na kwenda kwa mfalme kuomba arudishiwe nyumba yake na shamba lake. 4Akamkuta mfalme anaongea na Gehazi, akisema, “Tafadhali nieleze miujiza ambayo hutendwa na Elisha.” 5Gehazi alipokuwa anamweleza mfalme jinsi Elisha alivyofufua mtu aliyekufa, mwanamke huyo alitoa ombi lake kwa mfalme. Gehazi akasema, “Ee mfalme; huyu ndiye mwanamke ambaye Elisha alimfufua mwanawe!” 6Mfalme alipomwuliza mwanamke huyo, yeye alimweleza. Mfalme akamwita ofisa wake na kumwamuru amrudishie mwanamke huyo mali yake yote, pamoja na mapato yote ya mashamba yake katika muda huo wote wa miaka saba.

Elisha na mfalme Ben-hadadi wa Aramu

7Baadaye Elisha alikwenda Damasko. Wakati huo mfalme Ben-hadadi alikuwa mgonjwa na alipoambiwa kwamba Elisha alikuwa Damasko, 8alimwambia ofisa wake Hazaeli, “Mpelekee mtu wa Mungu zawadi umwambie atafute shauri kwa Mwenyezi-Mungu kama nitapona au la.” 9Hazaeli akapakia zawadi za kila aina ya mazao ya Damasko kiasi cha mizigo ya ngamia arubaini na kumpelekea Elisha. Alipofika kwa Elisha alimwambia, “Mtumishi wako, Ben-hadadi, mfalme wa Aramu amenituma kwako; yeye anauliza, ‘Nitapona ugonjwa huu?’” 10Basi Elisha akamjibu, “Atapona; lakini Mwenyezi-Mungu amenionesha kwamba atakufa.” 11Ndipo Elisha akamkazia macho akiwa na hofu hata Hazaeli akashikwa na wasiwasi. Ghafla, Elisha mtu wa Mungu, akaanza kulia. 12Hazaeli akamwuliza, “Bwana wangu, mbona unalia?” Elisha akamjibu, “Kwa sababu ninajua maovu ambayo utawatendea watu wa Israeli. Utateketeza ngome zao kwa moto, na kuwaua vijana wao, utawapondaponda watoto wao na kuwararua wanawake waja wazito.” 13Hazaeli akauliza, “Lakini mimi mtumishi wako ni kitu kweli? Mimi niliye mbwa tu nitawezaje kutenda mambo hayo makubwa?” Elisha akamjibu, “Mwenyezi-Mungu amenionesha kwamba utakuwa mfalme wa Aramu.” 14Ndipo Hazaeli alipotoka kwa Elisha, akarudi kwa bwana wake. Mfalme Ben-hadadi akamwuliza, “Elisha alikuambia nini?” Hazaeli akamjibu, “Aliniambia ya kwamba hakika utapona.” 15Lakini kesho yake Hazaeli akachukua blanketi akalilowesha majini, kisha akamfunika nalo usoni mpaka akafa. Hazaeli akatawala Aramu mahali pake.

Mfalme Yehoramu wa Yuda

(2Nya 21:1-20)

16Mnamo mwaka wa tano wa utawala wa Yoramu mwana wa Ahabu, mfalme wa Israeli,8:16 Israeli: Makala ya Kiebrania: Israeli Yehoshafati alipokuwa mfalme wa Yuda. Yehoramu mwana wa Yehoshafati, mfalme wa Yuda alianza kutawala. 17Alianza kutawala akiwa na umri wa miaka thelathini na miwili. Alitawala huko Yerusalemu miaka minane. 18Alizifuata njia mbaya za wafalme wengine wa Israeli, kama jamaa ya Ahabu ilivyofanya, kwa sababu mkewe alikuwa binti Ahabu. Akatenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, 19lakini Mwenyezi-Mungu hakutaka kuangamiza Yuda, kwa sababu ya Daudi mtumishi wake, kwani aliahidi kwamba wazawa wake wataendelea kutawala milele. 20Wakati wa enzi ya Yehoramu, watu wa Edomu waliasi utawala wa Yuda, wakamtawaza mfalme wao.
21Kwa hiyo Yoramu aliondoka na magari yake yote kwenda Zairi. Wakati wa usiku alitoka na makamanda wake wa magari akawashambulia Waedomu waliokuwa wamemzunguka; lakini jeshi lake lilikimbia nyumbani. 22Hivyo watu wa Edomu wakauasi utawala wa Yuda mpaka sasa. Wakati huohuo, wakazi wa Libna nao wakaasi.
23Matendo mengine yote ya mfalme Yehoramu yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda. 24Yehoramu akafa na kuzikwa katika makaburi ya kifalme katika mji wa Daudi, naye Ahazi, mwanawe Yehoramu, akatawala mahali pake.

Mfalme Ahazia wa Yuda

(2Nya 22:1-6)

25Katika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wa Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli, Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda, alianza kutawala. 26Ahazia alianza kutawala akiwa na umri wa miaka ishirini na miwili, akatawala kutoka Yerusalemu kwa muda wa mwaka mmoja. Mama yake aliitwa Athalia, mjukuu wa mfalme Omri mfalme wa Israeli. 27Kwa sababu Ahazia alikuwa mkwe wa jamaa ya Ahabu, naye alifuata mwenendo wa jamaa hiyo ya Ahabu, alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, kama vile jamaa ya Ahabu walivyofanya.
28Mfalme Ahazia akaenda na Yoramu mwana wa Ahabu kupigana vita dhidi ya Hazaeli mfalme wa Aramu huko Ramoth-gileadi mahali Waaramu walipomjeruhi Yoramu. 29Kisha mfalme Yoramu akarudi mjini Yezreeli ili apate kutibiwa majeraha aliyoyapata huko Rama, alipopigana na Hazaeli mfalme wa Aramu. Naye Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda alimwendea Yoramu mwana wa Ahabu huko Yezreeli, kwa sababu alikuwa mgonjwa.



2Wafalme8;1-29


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: