Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday, 5 April 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;Tumemaliza Kitabu cha 1 Wafalme ,Leo tunaanza 2 Wafalem 1......



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana ..
Tunamshukuru Mungu wetu kwa neema aliyotupa ya kusoma/kupitia
kitabu cha "1Wafalme" na kukimaliza  natumaini wengi tumepata kujifunza zaidi na leo tunaanza kitabu cha "2Wafalme" tunamuomba Mungu wetu 
akatuongoze,akatupe macho,akatupe ufahamu,kuelewa,tusomapo na
tukahifadhi na ikawe faida kwetu na kwa wengine pia....
Ee Mungu tunaomba utusaidie....!!

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii
Si kwa nguvu zetu wala si kwa uwezo wetu si kwamba sisi tumetenda
mema sana wala si kwa akili zetu au utashi wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo
Ni kwa neema/rehema zako ni  kwa mapenzi yako Mungu wetu sisi kuwa
hivi tulivyo leo hii....
Sifa na Utukufu tunakurudishia wewe Jehovah....!!

Mwenyezi-Mungu anatawala, mataifa yanatetemeka! Ameketi juu ya viumbe vyenye mabawa, nayo dunia inatikisika! Mwenyezi-Mungu ni mkuu katika Siyoni; ametukuka juu ya mataifa yote. Wote na walisifu jina lake kuu la kutisha. Mtakatifu ndiye yeye! Ee mfalme mkuu, mpenda uadilifu! Umethibitisha haki katika Israeli; umeleta uadilifu na haki.

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
Kwakuwaza,kwakutenda,kwakunena,kwakujua/kutojua
Yahweh tunaomba nasi utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote
waliotukosea
Jehovah usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuoke na yule
mwovu na kazi zake zote,Nguvu za giza,nguvu za mapepo,nguvu za
mizimu,nguvu za mpinga Kristo zishindwe katika jina la Bwana wetu
Yesu Kristo...
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Mungu wetu utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Msifuni Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu; angukeni kifudifudi mbele zake. Mtakatifu ndiye yeye! Mose na Aroni walikuwa makuhani wake; Samueli alikuwa miongoni mwa waliomlilia. Walimlilia Mwenyezi-Mungu naye akawasikiliza. Alisema nao katika mnara wa wingu; waliyazingatia matakwa yake na amri alizowapa. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, wewe uliwasikiliza; kwao ulikuwa Mungu mwenye kusamehe, ingawa uliwaadhibu kwa makosa yao. Msifuni Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu; abuduni katika mlima wake mtakatifu! Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ni mtakatifu.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye
kuhitaji..
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni ukatupe
kama inavyokupendeza wewe.....

Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu  wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,
familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu  wetu tunaomba
ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Jehovah tunaomba 
ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo..
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatamalaki na kutuatamia Mungu wetu tukawe
salama rohoni Baba wa Mbinguni ukatupe macho ya kuona na masikio
ya kusikia sauti yako na kuitii
Jehovah tukanene yaliyo yako Mungu wetu tunaomba ukatupe neema
ya kufuata njia zako Baba wa Mbinguni tukasimamie Neno lako amri
na sheria zako siku zote za maisha yetu
Yahweh ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane
kwamba upo Baba wa Mbinguni,Ukatupe neema ya kutambua mema na mabaya  
Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu furaha na amani vikatawale
 upendo ukadumu kati yetu..
Mungu nwetu tunayaweka haya yote mikononi mwako Yahweh tukiamini
kwako wewe yote yanawezaka....
UKatufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe...
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Mshangilieni Mwenyezi-Mungu, enyi nchi zote! Mwabuduni Mwenyezi-Mungu kwa furaha, nendeni kwake mkiimba kwa shangwe! Jueni kwamba Mwenyezi-Mungu ni Mungu. Yeye ndiye aliyetuumba, nasi ni mali yake; sisi ni watu wake, ni kondoo wa malisho yake. Pitieni milango ya hekalu lake kwa shukrani, ingieni katika nyua zake kwa sifa. Mshukuruni na kulisifu jina lake. Mwenyezi-Mungu ni mwema; fadhili zake zadumu milele, na uaminifu wake katika vizazi vyote.
Jehovah tunawaweka mikononi mwako wote wenye shida/tabu,
wagonjwa,wenye njaa,wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
waliokataliwa,waliokata tamaa,wenye hofu na mashaka,walioumizwa
rohoni,wenye kiburi na kisasi,waliokwama kibiashara,waliokwama
kimasomo,walio katika vifungo vya yule mwovu,walio magerezani pasipo na hatia,wafiwa ukawe mfariji wao,waliokwenda kinyume nawe na 
kila mmoja kwa mahitaji yake....
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaponye kimwili na kiroho pia
Yahweh tunaomba ukawafungue na kuwaokoa,Jehovah tunaomba
haki ikatendeke,Mungu wetu tunaomba ukawape chakula na ukabariki
mashamaba yao/kazi zao na ukawape ubunifu na maaarifa
Yahweh tunaomba ukawasamehe na ukawape neema ya kujiombea
kufuata njia zako nazo ziwaweke huru,Mungu wetu ukaonekane katika
maisha yao amani ikatawale neema na Nuru yako ikaangaze katika 
maisha yao,Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao Jehovah
tunaomba ukawafute machozi ya watoto wako Yahweh tunaomba
ukasikie na ukapokee sala/maombi yetu Mungu wetu ukawatendee 
sawasawa na mapenzi yako..
Kwakuwa ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina....!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwanami
Mungu baba aendelee kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye,Amani ya kristo Yesu ikawe nanyi  daima..
Nawapenda.

Elia na mfalme Ahazia

1Baada ya kifo cha Ahabu, watu wa Moabu waliasi wasitawaliwe na Israeli.
2Mfalme Ahazia alipokuwa Samaria alianguka kutoka chumba kilichokuwa paani mwa nyumba yake, akaumia vibaya. Kwa hiyo akawatuma wajumbe, akawaambia, “Nendeni kwa Baal-zebubu, mungu wa mji wa Ekroni, mkamwulize kama nitapona ugonjwa huu.” 3Lakini malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia nabii Elia kutoka Tishbe, aende kukutana na wajumbe hao na kuwauliza, “Kwa nini mnakwenda kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni? Je, hakuna Mungu nchini Israeli? 4Mwambieni mfalme kwamba Mwenyezi-Mungu amesema hivi: ‘Hutashuka katika kitanda ulichokipanda; hakika utakufa!’” 5Basi, Elia akawaendea. Wale wajumbe wakarudi kwa mfalme, naye akawauliza, “Mbona mmerudi?” 6Wakamjibu, “Tumekutana na mtu ambaye alitutuma turudi kukuambia kwamba Mwenyezi-Mungu amesema hivi: ‘Kwa nini unatuma wajumbe kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni? Je, hakuna Mungu nchini Israeli? Hutashuka katika kitanda ulichokipanda; bali hakika utakufa!’” 7Mfalme akauliza, “Ni mtu gani huyo aliyekutana nanyi na kuwaambieni mambo hayo?” 8Wao wakamjibu, “Alikuwa amevaa vazi la manyoya1:8 au Mtu mwenye nywele nyingi mwilini. na mshipi wa ngozi kiunoni.” Mfalme akasema, “Huyo ni Elia kutoka Tishbe!”
9Hapo mfalme akamtuma kapteni mmoja na watu wake hamsini wamlete Elia. Kapteni huyo akamkuta Elia ameketi mlimani, akamwambia, “Ewe mtu wa Mungu, mfalme anakuamuru ushuke.” 10Elia akamjibu huyo kapteni wa watu hamsini, “Kama mimi ni mtu wa Mungu, moto na ushuke kutoka mbinguni na kukuteketeza wewe pamoja na watu wako!” Mara moto ukashuka kutoka mbinguni, ukamteketeza pamoja na watu wake hamsini.
11Mfalme akamtuma kapteni mwingine na watu wake hamsini wamlete Elia. Naye akapanda1:11 akapanda juu: Kiebrania: Akajibu. juu akamwambia Elia, “Ewe mtu wa Mungu, mfalme anakuamuru ushuke mara moja!” 12Elia akamjibu, “Kama kweli mimi ni mtu wa Mungu, moto na ushuke kutoka mbinguni, ukuteketeze wewe pamoja na watu wako!” Papo hapo moto wa Mungu ukashuka kutoka mbinguni, ukamteketeza pamoja na watu wake hamsini.
13Kwa mara nyingine tena, mfalme akatuma kapteni mwingine na watu wake hamsini. Kapteni wa tatu akapanda mlimani, akapiga magoti mbele ya Elia na kumsihi akisema, “Ewe mtu wa Mungu, nakusihi uyathamini maisha yangu, na ya watu wako hawa, usituangamize! 14Maofisa wawili waliotangulia na watu wao, wameteketezwa na moto ulioshuka kutoka mbinguni; lakini sasa nakuomba uyahurumie maisha yangu.” 15Hapo malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Elia, “Shuka pamoja naye, wala usimwogope.” Basi, Elia akainuka, akashuka pamoja naye mpaka kwa mfalme, 16akamwambia, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Kwa sababu ulituma wajumbe kumtaka shauri Baal-zebubu, mungu wa Ekroni – kana kwamba hapakuwa na Mungu katika Israeli ambaye ungemwomba shauri – basi, hutashuka katika kitanda ulichopanda; hakika utakufa.’”
17Baadaye Ahazia akafariki kama Mwenyezi-Mungu alivyomwambia nabii wake Elia. Na, kwa kuwa Ahazia hakuwa na mtoto wa kiume, Yoramu1:17 Yoramu: Au Yehoramu. akawa mfalme mahali pake, katika mwaka wa pili wa utawala wa Yehoramu mwana wa Yehoshafati, mfalme wa Yuda.
18Mambo mengine aliyoyatenda mfalme Ahazia, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli.




2Wafalme1;1-18


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: