Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday, 24 May 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 1Mambo ya Nyakati 11...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluya Mungu wetu yu mwema sana
Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Mungu wetu Baba yetu Muumba wetu 
Muumba wa Mbingu na Nchi,Muumba wa vyote vilivyomo
Mungu mwenye nguvu,Mungu mwenye kuponya,Mungu mwenye huruma
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo
Baba wa Upendo,Baba wa Baraka,Baba  wa Uzima
Mwenyezi-Mungu wetu  Mungu wa walio hai
Yeye ni mwanzo na yeye ni mwisho,Alfa na Omega..!!

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha
kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudishia Baba wa Mbinguni...!!


1Mimi Yakobo, mtumishi wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo, nawaandikia nyinyi, makabila kumi na mawili, yaliyotawanyika ulimwenguni! Salamu!
Imani na hekima
2Ndugu zangu, muwe na furaha mnapopatwa na majaribu mbalimbali, 3kwani mwajua kwamba imani yenu ikisha stahimili, itawapatieni uvumilivu. 4Muwe na hakika kwamba uvumilivu wenu utawategemeza mpaka mwisho, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu, bila kupungukiwa chochote. 5Lakini kama mmoja wenu ametindikiwa hekima, basi, anapaswa kumwomba Mungu ambaye atampatia; kwani Mungu huwapa wote kwa wingi na kwa ukarimu.6Lakini anapaswa kuomba kwa imani bila mashaka yoyote. Mtu aliye na mashaka ni kama mawimbi ya bahari ambayo husukumwa na kutupwatupwa na upepo. 7,8Kwa hiyo mtu aliye na mashaka, mwenye nia mbili na asiye na msimamo katika mwenendo wake wote, asidhani ya kwamba atapata chochote kile kutoka kwa Bwana.

Yakobo 1:1-8



Mungu wetu tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale
wote waliotukosea
Jehovah utuepushe katika majaribu Baba wa Mbinguni utuokoe na
 yule mwovu na kazi zake zote
Mungu wetu ututakase miili yetu na akili zetu Yahweh utufunike kwa
Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Ndugu aliye maskini anapaswa kufurahi wakati Mungu anapomkweza, naye tajiri anapaswa kufurahi anaposhushwa na Mungu. Maana tajiri atatoweka kama ua la porini. Jua huchomoza na kwa joto lake kali hukausha mimea, nayo maua yake huanguka, na uzuri wake wote huharibika. Vivyo hivyo, tajiri ataangamizwa katika shughuli zake. Heri mtu anayebaki mwaminifu katika majaribu, kwani akisha stahimili, atapewa tuzo la uhai ambalo Mungu aliwaahidi wale wanaompenda. Kama mtu akijaribiwa, asiseme: “Ninajaribiwa na Mungu.” Maana Mungu hawezi kujaribiwa na uovu, wala yeye hamjaribu mtu yeyote. Lakini mtu hujaribiwa anapovutwa na kunaswa na tamaa zake mbaya. Tamaa ikiiva huzaa dhambi; nayo dhambi ikikomaa huzaa kifo. Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike! Kila kipaji chema na kila zawadi kamilifu hutoka mbinguni; hutoka kwa Baba, Muumba wa mianga, ambaye habadiliki wala hana alama yoyote ya ugeugeu. Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa kwa neno lake la ukweli, ili tuwe katika nafasi ya kwanza miongoni mwa viumbe vyake.

Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Mungu wetu tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Yahweh nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
 kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu ukatupe
kama inavyokupendeza wewe...

Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,
familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Baba wa Mbinguni tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote
tunavyovimiliki
Mungu wetu tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Jehovah tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Yahweh tunaomba ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya 
Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahweh tunaomba ukatupe macho ya kuona na masikio
ya kusikia sauti yako na kuitii
Jehovah ukatupe neema ya kiufuata njia zako
Mungu wetu tunakasimamie Neno lako amri na sheria zako
 siku zote za maisha yetu 
Baba wa Mbinguni ukaonekane katika maisha yetu
Mungu wetu ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Yahweh ukatupe neema ya kutambua mema na mabaya
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu
nasi tukatunmike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi.....


Ndugu zangu wapenzi, kumbukeni jambo hili! Kila mtu na awe mwepesi wa kusikia lakini si mwepesi wa kusema wala mwepesi wa kukasirika. Mwenye hasira hawezi kutimiza matakwa ya Mungu yaliyo ya haki. Kwa hiyo, tupilieni mbali mwenendo mchafu na tabia zote mbovu; jiwekeni chini ya Mungu na kupokea lile neno lililopandwa mioyoni mwenu, ambalo laweza kuziokoa nafsi zenu. Msijidanganye wenyewe kwa kusikiliza tu neno lake, bali litekelezeni kwa vitendo. Yeyote anayesikiliza hilo neno lakini halitekelezi, huyo ni kama mtu anayejiangalia sura yake mwenyewe katika kioo. Hujiangalia mwenyewe, kisha huenda zake, na mara husahau jinsi alivyo. Lakini mtu anayeangalia kwa makini sheria kamilifu ambayo huwapa watu uhuru, mtu anayeendelea kuizingatia, na si kuisikia tu na kuisahau baadaye, bali anaitekeleza, mtu huyo atabarikiwa katika kila kitu anachofanya. Kama mtu akijiona kuwa ni mtu mwenye dini, lakini hawezi kuutawala ulimi wake, dini yake haifai kitu, na anajidanganya mwenyewe. Dini iliyo safi na isiyo na hitilafu mbele ya Mungu Baba ni hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika shida zao, na kujilinda mwenyewe usichafuliwe na ulimwengu huu.

Yahweh tunawaweka mikononi mwako wote wenye shida/tabu,
wanaokutafuta kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kila mmoja na mahitajio yake
Baba wa Mbinguni wewe unajua haja zao na mahitaji yao
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Jehovah tunaomba ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
nazo zikawaweke huru
Yahweh tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Ukawape macho ya rohoni Mungu wetu na masikio ya kusikia sauti yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina.....!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba akawabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo wa Mungu Baba ukae nanyi
daima....
Nawapenda.


Daudi anakuwa mfalme

(2Sam 5:1-10)

1Kisha Waisraeli wote walikusanyika pamoja kwa Daudi huko Hebroni, wakamwambia: “Tazama, sisi ni mwili na damu yako. 2Hapo awali, Shauli alipokuwa mfalme wewe ndiwe uliyewaongoza Waisraeli vitani, na Mwenyezi-Mungu, Mungu wako alikuambia, ‘Utakuwa mchungaji wa watu wangu Israeli, na utakuwa mkuu wa watu wangu Israeli.’ 3Basi, wazee wote wa Israeli wakamwendea mfalme huko Hebroni; naye Daudi akafanya agano nao mbele ya Mwenyezi-Mungu, halafu wakampaka Daudi mafuta awe mfalme wa Waisraeli kulingana na neno la Mwenyezi-Mungu lililotolewa kwa njia ya Samueli.”
4Baadaye Daudi na Waisraeli wote walikwenda Yerusalemu uliojulikana kama Yebusi, na ambao wenyeji wake walikuwa Wayebusi. 5Wakazi wa Yebusi walimwambia Daudi, “Hutaingia katika mji huu.” Hata hivyo, Daudi aliiteka ngome ya Siyoni, yaani mji wa Daudi. 6Ndipo Daudi akasema, “Mtu atakayetangulia kuwapiga Wayebusi, atakuwa mkuu na kamanda jeshini.” Basi Yoabu, mwana wa Seruya, akawa wa kwanza kuwashambulia, hivyo akawa mkuu. 7Daudi alikaa katika ngome hiyo, na kwa hiyo, mji huo ukaitwa “Mji wa Daudi.” 8Aliujenga mji huo, akianzia Milo, na kuuzunguka wote, na Yoabu akautengeneza mji huo upya. 9Naye Daudi akazidi kuwa mkuu kwa sababu Mwenyezi-Mungu wa majeshi alikuwa pamoja naye.

Orodha ya mashujaa wa Daudi

(2Sam 23:8-39)

10Hii ndiyo orodha ya wakuu wa mashujaa wa Daudi, ambao pamoja na watu wengine wote wa Israeli, walimuunga mkono kwa pamoja ili awe mfalme, sawa na neno la Mwenyezi-Mungu alilotoa juu ya Waisraeli.
11Ifuatayo ni orodha ya mashujaa hao wa Daudi: Yashobeamu, Mhakmoni, aliyekuwa kiongozi wa “Wale thelathini.”11:11 “Wale thelathini” au wale watatu; tafsiri moja ya zamani (taz 2Sam 23:8). Yeye alipigana kwa mkuki wake akaua watu 300 kwa mara moja vitani. 12Halafu aliyefuata miongoni mwa wale mashujaa watatu alikuwa Eleazari mwana wa Dodo, Mwahohi. 13Siku moja Eleazari alikuwa pamoja na Daudi huko Pas-damimu, wakati Wafilisti walipokusanyika kupigana vita. Huko kulikuwa na shamba lenye shayiri tele, nao Waisraeli walikuwa wamewakimbia Wafilisti. 14Lakini Daudi na Eliazari walisimama imara katikati ya shamba hilo ili kulitetea, wakawaua Wafilisti; Mwenyezi-Mungu akawaokoa kwa kuwapa ushindi mkubwa.
15Kisha mashujaa watatu kati ya wakuu thelathini waliteremka hadi kwenye mwamba, wakamwendea Daudi kwenye pango huko Adulamu. Wakati huo jeshi la Wafilisti lilikuwa limepiga kambi katika bonde la Refaimu. 16Naye Daudi wakati huo alikuwa katika ngome, nalo jeshi la Wafilisti lilikuwa mjini Bethlehemu. 17Daudi akasema kwa hamu kubwa, “Laiti kama mtu angeweza kunipa maji ya kunywa kutoka katika kisima cha Bethlehemu kilicho karibu na lango la mji!” 18Wale mashujaa wake watatu walitoka, wakapenya katikati ya kambi ya jeshi la Wafilisti, wakaenda na kuchota maji katika kisima cha Bethlehemu, karibu na lango la mji, wakamletea Daudi. Lakini Daudi akakataa kuyanywa, na badala yake akayamwaga chini kama tambiko kwa Mwenyezi-Mungu 19akisema, “Tendo kama hili lipitishie mbali nami; siwezi kulifanya mbele ya Mungu wangu. Je, waweza kunywa damu ya maisha ya watu hawa? Maana kwa kuyahatarisha maisha yao walileta maji haya.” Kwa hiyo Daudi hakuyanywa maji hayo. Hayo ndio mambo waliyotenda wale mashujaa watatu.
20Abishai, nduguye Yoabu, alikuwa mkuu wa mashujaa thelathini. Yeye alipigana kwa mkuki wake dhidi ya watu 300, akawaua, akajipatia jina miongoni mwa wale mashujaa watatu. 21Basi, akawa mashuhuri zaidi miongoni mwa mashujaa thelathini, hata akawa kamanda wao, lakini hakuwa shujaa kama wale mashujaa watatu.
22Naye Benaya, mwana wa Yehoyada, kutoka Kabzeeli, alikuwa askari shujaa11:22 askari shujaa: Kiebrania: Mwana wa askari shujaa. ambaye alifanya mambo mengi ya ajabu. Aliwaua mashujaa wawili11:22 mashujaa wawili: Kiebrania si dhahiri. kutoka Moabu, na siku moja wakati wa barafu, alishuka na kuua simba shimoni. 23Vilevile, alimuua Mmisri mmoja, mtu mrefu sana, urefu wake kama mita mbili, naye mkononi mwake alikuwa amebeba mkuki mkubwa sana, kama mti wa mfumaji. Lakini Benaya alimwendea akiwa na fimbo tu, akamnyanganya mkuki huo, na kumuua Mmisri huyo kwa mkuki wake mwenyewe. 24Benaya, mwana wa Yehoyada alifanya mambo haya, akajipatia jina miongoni mwa wale mashujaa watatu. 25Basi, akawa mashuhuri kati ya wale mashujaa thelathini, ingawa hakuwa shujaa kama wale mashujaa watatu. Na Daudi akampa cheo cha mkuu wa walinzi wake binafsi.
26Wanajeshi mashujaa wa Daudi walikuwa: Asaheli nduguye Yoabu, Elhanani mwana wa Dodo wa Bethlehemu, 27Shamothi Mharodi, Helesi Mpeloni, 28Ira, mwana wa Ikeshi Mtekoa, Abiezeri Mwanathothi; 29Sibekai Mhushathi; Ilai Mwahohi; 30Maharai Mnetofathi; Heledi, mwana wa Baana Mnetofathi; 31Itai, mwana wa Ribai, kutoka Gibea, wa kabila la Benyamini; Benaya Mpirathoni; 32Hurai kutoka vijito vya Gaashi, Abieli Mwaibathi; 33Azmawethi Mbaharumu; Eliaba Mshaalboni; 34wana wa Yasheni Mgiloni; Yonathani, mwana wa Shagee Mharari, 35Ahiamu, mwana wa Sakari Mharari; Elifali, mwana wa Uri; 36Heferi Mmekerathi; Ahiya Mpeloni; 37Hezro Mkarmeli; Naarai, mwana wa Ezbai; 38Yoeli, nduguye Nathani; Mibhari, mwana wa Hagri; 39Zeleki Mwamoni; Naharai Mbeerothi, aliyekuwa mbeba silaha wa Yoabu, mwana wa Seruya; 40Ira na Garebu, waliokuwa Waithri, 41Uria, Mhiti; Zabadi, mwana wa Ahlai; 42Adina, mwana wa Shiza Mreubeni, mkuu wa Wareubeni, akiwa pamoja na watu thelathini; 43Hanani, mwana wa Maaka, Yoshafati Mmithni; 44Uzia Mwashterathi, Shama na Yeieli, wana wa Hothamu Mwaroeri; 45Yediaeli na Yoha nduguye, wana wa Shimri Mtizi; 46Elieli Mmahawi, Yeribai na Yoshavia wana wa Elnaamu; Ithma Mmoabu; 47Elieli, Obedi, na Yaasieli Mmesobai.




1Mambo ya Nyakati11;1-47


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: