Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday, 2 May 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Wafalme 20......




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu
na Nchi,Muumba wa vyote vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu mwenye nguvu,Mungu wa walio hai,Mungu wa Abrahamu,
Isaka na Yakobo..
Jehovah Jireh ..!Jehovah Nissi..!Jehovah Shammah,Jehovah Raah..!Jehovah Rapha..!
Jehovah Shalom..!Emanuel-Mungu pamoja nasi...!!

Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudishia ee Mungu wetu...



Siku moja ya Sabato, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano, na wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke ya ngano, wakaondoa punje zake kwa mikono, wakala. Baadhi ya Mafarisayo wakawauliza, “Mbona mnafanya jambo ambalo si halali siku ya Sabato?” Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma jinsi alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati walipokuwa na njaa? Yeye aliingia katika nyumba ya Mungu, akachukua ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu, akala na kuwapa wenzake. Haikuruhusiwa mtu kula mikate hiyo isipokuwa tu makuhani.” Hivyo akawaambia, “Mwana wa Mtu ana uwezo juu ya Sabato.”

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Jehovah nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea
Yahweh usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuokoe na yule
mwovu na kazi zake zote
Baba wa Mbinguni ututakase na kutufunika kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Siku nyingine ya Sabato, Yesu aliingia katika sunagogi, akafundisha. Mle ndani kulikuwa na mtu ambaye mkono wake wa kulia ulikuwa umepooza. Waalimu wa sheria na Mafarisayo walitaka kupata kisa cha kumshtaki Yesu na hivyo wakawa wanangojea waone kama angemponya mtu siku ya Sabato. Lakini Yesu alijua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Inuka, simama katikati.” Yule mtu akaenda kusimama katikati. Kisha Yesu akawaambia, “Nawaulizeni, je, ni halali siku ya Sabato kutenda jambo jema au kutenda jambo baya; kuokoa maisha au kuyaangamiza?” Baada ya kuwatazama wote waliokuwa pale, akamwambia yule mtu, “Nyosha mkono wako.” Naye akafanya hivyo, na mkono wake ukawa mzima tena. Lakini wao wakakasirika sana, wakajadiliana jinsi ya kumtendea Yesu maovu.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji
Baba wa Mbinguni tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe...

Mungu wetu tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu ukatubariki tuingiapo/tutokapo Yahweh tunaomba
ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Jehovah tunaomba
ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Baba wa Mbinguni ukatamalaki na kutuatamia
Mungu wetu tukawe salama rohoni
Jehovah tunaomba ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia
sauti yako na kuitii
Yahweh tunaomba ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mungu wetu tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Baba wa Mbinguni tukasimamie Neno lako amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu
Yahweh ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na 
ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni
Neema na Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Upendo ukadumu kati yetu...
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke 
kama inavyokupendeza wewe...
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Siku moja Yesu alikwenda mlimani kusali, akakesha huko usiku kucha akisali. Kesho yake aliwaita wanafunzi wake, na miongoni mwao akawachagua watu kumi na wawili ambao aliwaita mitume: Simoni (ambaye Yesu alimpa jina Petro) na Andrea ndugu yake, Yakobo na Yohane, Filipo na Bartholomayo, Mathayo na Thoma, Yakobo wa Alfayo na Simoni (aliyeitwa Zelote), Yuda wa Yakobo na Yuda Iskarioti ambaye baadaye alikuwa msaliti. Baada ya kushuka mlimani pamoja nao, Yesu alisimama mahali palipokuwa tambarare. Hapo kulikuwa na kundi kubwa la wanafunzi wake na umati wa watu waliotoka pande zote za Yudea na Yerusalemu na pwani ya Tiro na Sidoni. Wote walifika kumsikiliza Yesu na kuponywa magonjwa yao. Aliwaponya pia wote waliokuwa wanasumbuliwa na pepo wachafu. Watu wote walitaka kumgusa, kwa maana nguvu ilikuwa inatoka ndani yake na kuwaponya wote.

Baba wa Mbinguni tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,
Wagonjwa,wenye njaa,walio katika magumu/majaribu mbalimbali,
waliokataliwa,waliokata tamaa,wenye hofu na mashaka,
waliokatika vifungo vya yule mwovu,walio magerezani pasipo na hatia,
waliojeruhiwa/umizwa rohoni,waliokwenda kinyume nawe/walipotea
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Jehovah tunaomba ukawaponye kimwili na kiroho pia
Baba wa Mbinguni ukaonekane katika maisha yao
Jehovah ukabariki mashamba/kazi zao
Mungu wetu ukawasamehe na kuwaokoa
Mungu wetu ukawaweke huru na haki ikatendeke..
Ee Baba tunaomba ukasikie kuomba kwetu na ukapokee sala/maombi yetu
Jehovah ukawatendee sawasawa na mapenzi yako..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina...!!

Asanteni sana Wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwanami/kunisoma
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
 kama inavyompendeza yeye..
Nawapenda.



Kuugua na kupona kwa mfalme Hezekia

(Isa 38:1-8,21-22; 2Nya 32:24-26)

1Wakati huo Hezekia aliugua sana karibu na kufa. Ndipo nabii Isaya, mwana wa Amozi alipomwendea na kumwambia, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu; ‘Panga mambo yako sawasawa katika nyumba yako kwa kuwa utakufa, hutapona.’”
2Hezekia akageukia upande wa ukuta na kumwomba Mwenyezi-Mungu akisema, 3“Ee Mwenyezi-Mungu, nakusihi ukumbuke jinsi nilivyokutumikia kwa uaminifu na kwa moyo wangu wote na kutenda yaliyo sawa mbele yako.” Hezekia akalia kwa uchungu sana.
4Lakini kabla Isaya hajapita ua wa katikati, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia, kusema, 5“Rudi ukamwambie Hezekia, mkuu wa watu wa Mwenyezi-Mungu: Mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu yako Daudi, nimesikia ombi lako na nimeona machozi yako. Nitakuponya na baada ya siku tatu utakwenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 6Nitakuongezea miaka kumi na mitano ya kuishi. Nitakuokoa wewe pamoja na mji huu mikononi mwa mfalme wa Ashuru. Nitaulinda mji huu kwa ajili ya heshima yangu mimi na kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi.”
7Basi Isaya akasema, “Leteni andazi la tini mliweke kwenye jipu lake, ili apate kupona.” 8Hezekia akamwuliza Isaya, “Ni ishara gani ambayo itanionesha kwamba kweli Mwenyezi-Mungu ataniponya na katika siku ya tatu nitaweza kwenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu?”
9Isaya akamjibu, “Hii itakuwa ishara kwako kutoka kwa Mwenyezi-Mungu, kwamba Mwenyezi-Mungu atafanya kama alivyoahidi: Je, kivuli kiende hatua kumi mbele au nyuma?”
10Hezekia akamjibu, “Ni rahisi zaidi kivuli kwenda mbele hatua kumi! Hebu kirudi nyuma hatua kumi.”
11Isaya akamwomba Mwenyezi-Mungu, naye Mwenyezi-Mungu akafanya kivuli kirudi hatua kumi kwenye ngazi iliyojengwa na Ahazi.

Wajumbe kutoka Babuloni

(Isa 39:1-8)

12Wakati huo, mfalme Merodak-baladani mwana wa Baladani mfalme wa Babuloni alisikia kuwa Hezekia alikuwa ameugua na sasa amepona, akamtumia ujumbe pamoja na zawadi. 13Basi, Hezekia akawakaribisha na kuwaonesha mali yake: Nyumba yake ya hazina, fedha, dhahabu, viungo vya kukolezea chakula, mafuta ya thamani na nyumba ya vifaa vyake vyote vya kijeshi na vitu vyote vilivyokuwamo katika bohari zake. Hakukuwa chochote katika ikulu yake, au nchi yake ambacho hakuwaonesha. 14Ndipo nabii Isaya alipomwendea mfalme Hezekia na kumwuliza, “Watu hawa wamesema nini? Na, wamekujia kutoka wapi?” Naye Hezekia akamjibu, “Wamenijia kutoka nchi ya mbali.” 15Halafu akamwuliza, “Wameona nini katika ikulu yako?” Hezekia akamjibu, “Wameona yote yaliyomo katika ikulu yangu. Hakuna chochote katika bohari zangu ambacho sikuwaonesha.”
16Ndipo Isaya akamwambia Hezekia, “Sikia neno la Mwenyezi-Mungu: 17Tazama, siku zinakuja ambapo vyote vilivyomo nyumbani mwako na vitu vyote walivyokusanya baba zako mpaka wakati huu vitapelekwa mpaka Babuloni. Hakuna kitu chochote kitakachobaki; ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu. 18Tena baadhi ya watoto wako wa kiume watapelekwa mateka, nao watakuwa matowashi katika ikulu ya mfalme wa Babuloni.”
19Naye Hezekia akamwambia Isaya, “Neno la Mwenyezi-Mungu kama ulivyolisema ni sawa.” Alisema hivyo kwani alifikiri, “Kwa nini isiwe hivyo, ikiwa kutakuwapo amani na ulinzi katika siku za utawala wangu.”

Mwisho wa enzi ya Hezekia

(2Nya 32:32-33)

20Matendo mengine ya Hezekia, ushujaa wake na maelezo juu ya jinsi alivyojenga bwawa na kuchimba mfereji wa kuleta maji mjini, yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda. 21Hezekia alifariki, naye Manase mwanawe akatawala mahali pake.




2Wafalme20;1-21


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: