Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday, 7 May 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Wafalme 23......



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana..
Ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua
na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Tumshukuru Mungu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari
 kwa majukumu yetu
Utukuzwe ee Mungu wetu,Unastahili sifa Baba wa Mbinguni,
Unastahili kuabudiwa Yahweh,unastahili kuhimidiwa Jehovah..
Matendo yako ni makuu mno,Matendo yako ni ya ajabu,
Mtendo yako  yanatisha,Neema yako yatutosha ee Mungu wetu
Sifa na utukufu tunakurudishia wewe Baba wa Mbinguni...

Baada ya kusema yale aliyotaka watu wasikie, Yesu alikwenda Kafarnaumu. Huko kulikuwa na jemadari mmoja ambaye alikuwa na mtumishi wake aliyempenda sana. Huyu mtumishi alikuwa mgonjwa karibu na kufa. Yule jemadari aliposikia habari za Yesu, aliwatuma wazee fulani Wayahudi waende kumwomba aje kumponya mtumishi wake. Walipofika kwa Yesu, walimsihi sana, wakasema: “Huyu anastahili afanyiwe jambo hilo, kwa maana yeye analipenda taifa letu, na ndiye aliyetujengea lile sunagogi.”
Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na
kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya
kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba
utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi
wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Basi, Yesu akaenda pamoja nao. Alipokuwa karibu na kufika nyumbani kwa yule jemadari, yule jemadari aliwatuma marafiki zake wamwambie Yesu: “Bwana, usijisumbue zaidi, maana mimi sistahili uingie nyumbani mwangu. Ndio maana sikujiona nastahili hata kuja kwako. Lakini sema tu neno, na mtumishi wangu atapona. Kwa maana mimi pia ni mtu niliye chini ya mamlaka, na ninao askari chini yangu. Namwambia mmoja, ‘Nenda!’ Naye huenda; namwambia mwingine, ‘Njoo!’ Naye huja; na mtumishi wangu, ‘Fanya kitu hiki!’ Naye hufanya.” Yesu aliposikia hayo, alishangaa, halafu akauelekea ule umati wa watu uliokuwa unamfuata, akasema, “Sijaona mwenye imani kama hii hata katika Israeli!” Wale watu walipowasili nyumbani walimkuta yule mtumishi hajambo kabisa.
Jehovah tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Mungu wetu nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Yahweh tunaomba ukatupe nasi neema ya kuweza kuwabariki
 wenye kuhitaji
Jehovah tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni  ukatupe kama inavyokupendeza wewe


Mungu wetu tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Jehovah tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Mungu wetu tunaomba ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya
 Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote
tunavyo vimiliki
Baba wa Mbinguni ukatamalaki na kutuatamia
Yahweh ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia
sauti yako na kuitii
Mungu wetu tunaomba ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Jehovah tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Mungu wetu tukasimamie Neno lako amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu
Baba wa Mbinguni ukaonekane katika maisha yetu
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Upendo ukadumu kati yetu,utu wema na fadhili,hekima na busara....
Tukanene yaliyo yako ee Mungu wetu
Ukatufanye chombo chema Baba wa Mbinguni nasi tukatumike
kama inavyokupendeza wewe...
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi


Baadaye kidogo, Yesu alikwenda katika mji mmoja uitwao Naini, na wafuasi wake na kundi kubwa la watu waliandamana naye. Basi, alipokuwa anakaribia lango la mji, walitokea watu wamebeba maiti ya mwanamume mmoja, mtoto wa pekee wa mama mjane. Watu wengi wa mji ule walikuwa pamoja na huyo mama. Bwana alipomwona mama huyo akamwonea huruma, akamwambia, “Usilie.” Kisha, akaenda akaligusa lile jeneza, na wale waliokuwa wamelichukua wakasimama. Halafu akasema, “Kijana! Nakuamuru, amka!” Yule aliyekufa akaketi, akaanza kuongea. Na Yesu akamkabidhi kwa mama yake. Watu wote walishikwa na hofu, wakawa wanamtukuza Mungu wakisema, “Nabii mkuu ametokea kati yetu. Mungu amekuja kuwakomboa watu wake.” Habari hizo zikaenea kote katika Yudea na katika nchi za jirani.
Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye
nguvu wote wanaokutafuta kwa bidii na imani
Yahweh tunaomba ukawaponye kimwili na kiroho pia
Jehovah tunaomba ukawatendee kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukaonekane katika maisha yao
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
nazo zikawaweke huru
Yahweh tunaomba ukasikie kulia kwao Mungu wetu
tunaomba ukawafute machozi yao
Baba wa Mbinguni tunaomba ukasikie na
 ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Miele
Amina....!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukawe nanyi daima....
Nawapenda.







Mfalme Yosia aondoa ibada za miungu

(2Nya 34:3-7,29-33)

1Kisha mfalme alituma wajumbe, nao wakamkusanyia viongozi wote wa Yuda na wa Yerusalemu. 2Naye mfalme akaenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu akifuatana na watu wote wa Yuda na wakazi wote wa Yerusalemu, na makuhani pamoja na manabii, watu wote wadogo kwa wakubwa. Basi, akawasomea maneno ya kitabu cha agano kilichopatikana katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 3Halafu mfalme akasimama karibu na nguzo na kufanya agano mbele ya Mwenyezi-Mungu, kumfuata Mwenyezi-Mungu, kushika amri zake, maamuzi na masharti yake kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote, kutenda maneno yote ya agano yaliyoandikwa katika kitabu hicho cha agano. Watu wote wakaungana katika kufanya agano.
4Kisha Yosia akaamuru kuhani mkuu Hilkia na makuhani wasaidizi wake na mabawabu watoe katika hekalu la Mwenyezi-Mungu vitu vilivyotengenezwa kwa ajili ya Baali, Ashera na kwa ajili ya sayari; aliviteketeza nje ya Yerusalemu katika bonde la Kidroni na kupeleka majivu yake huko Betheli. 5Kisha akawaondoa makuhani wote waliobarikiwa na wafalme wa Yuda ili kufukiza ubani katika mahali pa kuabudia katika miji ya Yuda na kuzunguka Yerusalemu; pia na wale waliofukiza ubani kwa Baali, jua, mwezi, nyota na sayari katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 6Aliondoa Ashera kutoka katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, nje ya Yerusalemu, akaipeleka mpaka kijito cha Kidroni. Huko akaiteketeza na kuisaga mpaka ikawa mavumbi, nayo mavumbi yake akayatawanya juu ya makaburi ya watu. 7Alibomoa nyumba za mahanithi zilizokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, mahali ambamo wanawake walifuma mapazia ya Ashera. 8Akakusanya makuhani wote kutoka miji ya Yuda na akapatia najisi mahali pa juu makuhani walikofukiza ubani, kutoka Geba mpaka Beer-sheba; naye akabomoa mahali pa juu palipokuwa upande wa kushoto wa lango la mji penye malango yaliyokuwa kwenye njia ya kuingilia lango la Yoshua mtawala wa mji. 9Makuhani hao hawakufikia madhabahu ya Mwenyezi-Mungu katika Yerusalemu, lakini walikula mikate isiyotiwa chachu waliyopewa na jamaa zao.
10Mfalme Yosia pia alipatia najisi mahali pa kuabudia miungu ya uongo palipoitwa Tofethi katika bonde la wana wa Hinomu, ili mtu yeyote asimchome mwanawe au bintiye kuwa tambiko kwa Moleki. 11Kadhalika aliondoa farasi waliotengwa na wafalme wa Yuda kwa ajili ya jua, kwenye njia ya kuingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, karibu na chumba cha Nathan-meleki, kilichokuwa kiungani; naye alichoma kwa moto magari ya jua. 12Madhabahu ambayo wafalme wa Yuda walijenga paani kwenye chumba cha juu cha Ahazi, pamoja na madhabahu ambayo Manase alijenga katika nyua mbili za nyumba ya Mwenyezi-Mungu aliyabomoa na kuyapondaponda, kisha alitupa mavumbi yake katika kijito cha Kidroni. 13Mfalme pia alipatia unajisi mahali pa kuabudia palipokuwa upande wa mashariki ya Yerusalemu na kuelekea upande wa mlima wa Ufisadi, mahali mfalme wa Israeli alipopajenga kwa ajili ya Ashtarothi chukizo la Wasidoni, Kemoshi chukizo la Moabu na pia kwa ajili ya Milkomu chukizo la Waamoni. 14Alivunja nguzo katika vipandevipande; pia alikatakata sanamu za Ashera, na mahali zilipokuwa zinasimama alipajaza mifupa ya watu.
15Zaidi ya hayo aliharibu huko Betheli mahali pa kuabudia palipojengwa na mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati, aliyewafanya watu wa Israeli watende dhambi; aliharibu madhabahu hayo na kuvunja mawe yake katika vipandevipande, na kisha akaviponda mpaka vikawa vumbi; pia akachoma sanamu ya Ashera. 16Kisha Yosia alipogeuka aliona makaburi juu ya kilima; aliagiza mifupa ifukuliwe kutoka makaburini na kuichoma juu ya madhabahu; basi akayatia unajisi madhabahu sawasawa na neno la Mwenyezi-Mungu ambalo mtu wa Mungu alilitangaza, nabii ambaye alitabiri matukio haya. 17Halafu mfalme aliuliza, “Mnara ninaouona kule ni wa nini?” Nao watu wa mji wakamjibu, “Ni kaburi la mtu wa Mungu ambaye alikuja kutoka Yuda na kutabiri mambo ambayo umeyafanya dhidi ya madhabahu pale Betheli.”
18Naye akaagiza, “Mwacheni hapo, mtu yeyote asiondoe mifupa yake.” Kwa hiyo waliiacha mifupa yake, pamoja na mifupa ya nabii aliyetoka Samaria.
19Katika kila mji wa Samaria mfalme Yosia aliharibu mahali pa kuabudia miungu ya uongo palipojengwa na wafalme wa Israeli, ili kumkashifu Mwenyezi-Mungu. Madhabahu hayo yote aliyaharibu kama vile alivyofanya huko Betheli. 20Aliwaua makuhani wote wa miungu ya uongo juu ya madhabahu ambapo walitumikia na kuchoma mifupa yao juu ya madhabahu hayo. Kisha alirudi Yerusalemu.

Yosia asherehekea Pasaka

(2Nya 35:1-19)

21Kisha mfalme aliwaamuru watu wote, akisema, “Mfanyieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, Pasaka, kama ilivyoandikwa katika kitabu hiki cha agano.” 22Hakuna Pasaka iliyosherehekewa kama hii tangu wakati wa waamuzi waliowaamua Waisraeli wala wakati wa ufalme wa Israeli au wa Yuda. 23Lakini, katika mwaka wa kumi na nane wa enzi ya Yosia, Pasaka ilisherehekewa kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu katika Yerusalemu.

Mabadiliko mengine yaliyofanywa na Yosia

24Tena, ili mfalme Yosia atekeleze sheria zote zilizoandikwa katika kitabu alichokipata kuhani mkuu Hilkia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, aliondoa katika nchi ya Yuda na Yerusalemu, wachawi, watabiri, vinyago vya miungu, sanamu za miungu pamoja na vitu vyote vya kuchukiza. 25Kabla ya Yosia au baada yake hakuna mfalme yeyote aliyekuwa kama yeye, ambaye alimtumikia Mwenyezi-Mungu kwa moyo wake wote, kwa nguvu zake zote na kwa roho yake yote kulingana na sheria ya Mose.
26Hata hivyo, Mwenyezi-Mungu hakuacha ukali wa ghadhabu yake nyingi, kwa sababu hasira yake iliwaka dhidi ya Yuda kwa ajili ya vitendo vya kukasirisha, ambavyo Manase alifanya dhidi yake. 27Naye Mwenyezi-Mungu alisema, “Nitawafukuza watu wa Yuda kutoka mbele yangu kama vile nilivyofanya kwa watu wa Israeli; nitaukataa mji wa Yerusalemu ambao niliuchagua niliposema, ‘Jina langu litakuwa humo.’”

Mwisho wa enzi ya Yosia

(2Nya 35:20–36:1)

28Matendo mengine ya Yosia na yale yote aliyofanya yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda. 29Wakati wa kutawala kwake, Farao Neko wa Misri alikwenda mpaka mto Eufrate ili kukutana na mfalme wa Ashuru. Naye mfalme Yosia akaondoka ili kupambana naye; lakini Farao Neko alipomwona alimuua kule Megido. 30Maofisa wake wakaibeba maiti yake katika gari na kuirejesha Yerusalemu walikomzika katika kaburi lake mwenyewe. Kisha watu wa Yuda wakamchukua Yehoahazi mwana wa Yosia wakampaka mafuta na kumtawaza kuwa mfalme mahali pa baba yake.

Mfalme Yohoahazi wa Yuda

(2Nya 36:2-4)

31Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitatu alipoanza kutawala, akatawala kwa miezi mitatu huko Yerusalemu. Mama yake alikuwa Hamutali binti Yeremia wa Libna. 32Yehoahazi alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kama babu zake walivyofanya. 33Ili asiendelee kutawala huko Yerusalemu, Farao Neko alimtia nguvuni huko Ribla katika nchi ya Hamathi, akaitoza nchi kodi ya kilo 3,400 za madini ya fedha na kilo 34 za dhahabu. 34Farao Neko akamtawaza Eliakimu mwana wa mfalme Yosia mahali pa baba yake Yosia, akabadilisha jina lake kuwa Yehoyakimu. Lakini alimchukua Yehoahazi mbali mpaka Misri na kufia huko.

Mfalme Yehoyakimu wa Yuda

(2Nya 36:5-8)

35Mfalme Yehoyakimu alimpa Farao fedha na dhahabu, lakini aliitoza nchi kodi ili aweze kutekeleza matakwa ya Farao ya kupewa fedha. Aliwatoza wananchi fedha na dhahabu. Kila mmoja alitoa kiasi alichokadiria mfalme, naye akampa Farao Neko.
36Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, na alitawala huko Yerusalemu kwa muda wa miaka kumi na mmoja. Jina la mama yake lilikuwa Zebida binti Pedaya wa Ruma. 37Yehoyakimu alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, kama waliyoyafanya babu zake wote.



2Wafalme23;1-37


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: