Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday, 8 May 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Wafalme 24......




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Mungu mwenye nguvu,Mungu wa walio hai,Mungu mwenye huruma,
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Mungu mwenye kuponya,Mungu wetu hasemi uongo..
Baba wa Upendo,Baba wa Yatima,Baba wa Baraka,Mume wa wajane
yeye ni mwanzo na yeye ni mwisho,Alfa na Omega...!

Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha
kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudishia ee Mungu wetu...!!



Wanafunzi wa Yohane walimhabarisha Yohane juu ya mambo hayo yote. Naye Yohane, baada ya kuwaita wawili kati ya wanafunzi wake, aliwatuma kwa Bwana wamwulize: “Wewe ndiye yule anayekuja, au tumngoje mwingine?” Wale wanafunzi walipomfikia Yesu wakamwambia, “Yohane Mbatizaji ametutuma kwako tukuulize: ‘Wewe ndiye yule anayekuja, au tumngoje mwingine?’” Wakati huohuo, Yesu alikuwa anawaponya watu wengi waliokuwa wanateseka kwa magonjwa na waliopagawa na pepo wabaya na kuwawezesha vipofu wengi kuona. Basi, Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie Yohane yale mliyojionea na kuyasikia: Vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa Habari Njema. Heri mtu yule ambaye hana mashaka nami!”

Mungu wetu tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
Kwakuwaza,Kwakunena,Kwakutenda,Kwakujua/Kutojua
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale
wote waliotukosea
Yahweh utuepushe katika majaribu Mungu wetu tunaomba
utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
Baba wa Mbinguni ututakase miili yetu na akili zetu
Jehovah tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi
wetu Yesu Kristo wa Nazareti,yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona



Hapo wajumbe wa Yohane walipokwisha kwenda zao, Yesu alianza kuyaambia makundi ya watu juu ya Yohane: “Mlikwenda kutazama nini kule jangwani? Je, mlitaka kuona mwanzi unaotikiswa na upepo? Basi, mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona mtu aliyevaa mavazi maridadi? Wanaovaa mavazi maridadi na kuishi maisha ya anasa, hukaa katika majumba ya wafalme! Basi, niambieni, mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona nabii? Naam, hakika ni zaidi ya nabii. Huyu Yohane ndiye anayesemwa katika Maandiko Matakatifu: ‘Tazama mimi namtuma mtumishi wangu akutangulie; ambaye atakutayarishia njia yako.’”

Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Mungu wetu tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji
Baba wa Mbinguni tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Jehovah ukatupe kama inavyokupendeza wewe...



Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu
Familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Baba wa Mbinguni tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote
tunavyovimiliki
Mungu wetu tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Jehovah tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Yahweh tunaomba ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana
wetu Yesu Kristo
Baba wa Mbinguni ukatamalaki  na kutuatamia
Mungu wetu tukawe salama rohoni
Jehovah tunaomba ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia
sauti yako na kuitii
Mungu wetu tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Baba wa Mbinguni tukasimamie Neno lako amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu
Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika
maisha yetu,upendo ukadumu kati yetu
Neema yako na Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Tukanene yaliyo yako ee Mungu wetu
Ukatufanye chombo chema Baba wa Mbinguni nasi tukatumike
kama inavyo kupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi




Yesu akamalizia kwa kusema, “Nawaambieni, kati ya binadamu wote hakuna aliye mkubwa zaidi kuliko Yohane Mbatizaji. Hata hivyo, yule aliye mdogo kabisa katika ufalme wa Mungu ni mkubwa kuliko yeye.” Waliposikia hayo watu wote na watozaushuru waliusifu wema wa Mungu; hao ndio wale waliokuwa wameupokea ubatizo wa Yohane. Lakini Mafarisayo na waalimu wa sheria walikataa mpango wa Mungu uliowahusu, wakakataa kubatizwa na Yohane. Yesu akaendelea kusema, “Basi, nitawafananisha watu wa kizazi hiki na kitu gani? Ni watu wa namna gani? Ni kama vijana waliokuwa wamekaa sokoni na kuambiana, kikundi kimoja na kingine: ‘Tumewapigieni ngoma, lakini hamkucheza! Tumeimba nyimbo za huzuni lakini hamkulia!’ Kwa maana Yohane alikuja, akawa anafunga na hakunywa divai, nanyi mkasema: ‘Amepagawa na pepo!’ Naye Mwana wa Mtu amekuja, anakula na kunywa, nanyi mkasema: ‘Mwangalieni mlafi huyu na mlevi; rafiki ya watozaushuru na wenye dhambi!’ Hata hivyo, hekima ya Mungu imethibitishwa kuwa njema na wote wale wanaoikubali.”

Baba wa Mbinguni tunawaweka mikononi mwako
wenye shida/tabu,wagonjwa,wenye njaa,wanaopitia magumu/majaribu

mbalimbali,walio katika vifungo vya yule mwovu,walio magerezani pasipo na hatia,walio kata tamaa,walio kataliwa,wenye hofu na mashaka,waliokwama kibiashara,kimasomo,walioumizwa rohoni,walio kwenda kinyume nawe,na wote wanaokutafuta  kwa bidii na imani,
wafiwa ukawe mfariji wao..
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Jehovah tunaomba ukawaponye kimwili na kiroho pia
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawavushe salama na ukawaokoe
Yahweh ukawaweke huru na haki ikatendeke
Mungu wetu tunaomba ukabariki mashamba yao/kazi zao
Jehovah ukawape ubunifu na maarifa katika utendaji
Baba wa Mbinguni tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe na ukawape neema ya kujiombea,
kufuata njia zako nazo zikawaweke huru
Jehovah ukasikie kulia kwao Mungu wetu tunaomba ukawafute
machozi yao,Baba wa Mbinguni ukawatendee kila mmoja na mahitaji yake
Yahweh tunaomba ukasikie kuomba kwetu Mungu wetu 
ukapokee sala/maombi yetu
Baba wa Mbinguni ukatende sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!



Asanteni sana wapendwa katika Yesu Kristo kwakuwa nami/kunisoma
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea sawasawa na mapenzi yake
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukawe nanyi daima....
Nawapenda.
1Nebukadneza mfalme wa Babuloni aliishambulia Yuda. Yehoyakimu, alimtumikia kwa miaka mitatu halafu aliacha kumtii, akamwasi. 2Basi, Mwenyezi-Mungu akampelekea makundi ya Wababuloni, Waaramu, Wamoabu na Waamoni washambulie nchi ya Yuda na kuiharibu, kulingana na neno la Mwenyezi-Mungu alilolisema kwa watumishi wake manabii. 3Hakika mambo haya yaliikumba nchi ya Yuda kwa amri ya Mwenyezi-Mungu, ili kuwahamisha kutoka mbele yake, kwa sababu ya dhambi za mfalme Manase na yote aliyoyatenda, 4na kwa sababu ya damu isiyo na hatia aliyoimwaga. Mwenyezi-Mungu hakumsamehe makosa hayo.
5Basi matendo mengine ya Yehoyakimu na yote aliyoyafanya yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Yuda. 6Yehoyakimu akafariki, na mwanawe Yehoyakini akatawala mahali pake.
7Mfalme wa Misri hakutoka tena nchini kwake, kwa sababu mfalme wa Babuloni aliitwaa na kuimiliki nchi yote iliyokuwa chini ya mfalme wa Misri hapo awali tangu kijito cha Misri mpaka mto Eufrate.

Mfalme Yehoyakini wa Yuda

(2Nya 36:9-10)

8Yehoyakini alikuwa na umri wa miaka kumi na minane alipoanza kutawala; alitawala huko Yerusalemu kwa muda wa miezi mitatu. Mama yake alikuwa Nehushta binti Elnathani, mkazi wa Yerusalemu. 9Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kama aliyoyafanya baba yake.
10Wakati huo jeshi la Nebukadneza mfalme wa Babuloni, lilishambulia mji wa Yerusalemu na kuuzingira. 11Wakati majeshi yalipokuwa yanauzingira mji, Nebukadneza mwenyewe alikuja Yerusalemu, 12na Yehoyakini mfalme wa Yuda alijisalimisha kwa mfalme wa Babuloni, yeye mwenyewe pamoja na mama yake, watumishi wake, maofisa na maakida wake. Mfalme wa Babuloni alimchukua mateka katika mwaka wa nane wa kutawala kwake. 13Vilevile, pia kama Mwenyezi-Mungu alivyosema, Nebukadneza alichukua mali yote iliyokuwa ndani ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, na ndani ya ikulu. Alikatakata vyombo vyote vya dhahabu ambavyo Solomoni mfalme wa Israeli alitengeneza. Vyombo hivyo vilikuwa ndani ya hekalu la Mwenyezi-Mungu. 14Alichukua watu wote wa Yerusalemu: Wakuu wote, watu wote waliokuwa mashujaa, mateka 10,000, na mafundi wote na wahunzi. Hakuna aliyebaki isipokuwa waliokuwa maskini kabisa nchini. 15Alimchukua Yehoyakini mpaka Babuloni pamoja na mama yake mfalme, wake za mfalme, maofisa wake na wakuu wa nchi; wote hao aliwatoa Yerusalemu, akawapeleka Babuloni. 16Nebukadneza alichukua watu mashujaa wa Yuda jumla yao watu 7,000 pamoja na mafundi hodari na wahunzi 1,000; wote hawa wakiwa watu wenye nguvu na wa kuweza kupigana vitani.
17Nebukadneza akamtawaza Matania, mjomba wake Yehoyakini, kuwa mfalme badala yake, akalibadilisha jina lake kuwa Sedekia.

Mfalme Sedekia wa Yuda

(2Nya 36:11-12; Yer 52:1-3a)

18Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja alipoanza kutawala; alitawala kwa muda wa miaka kumi na mmoja huko Yerusalemu. Mama yake aliitwa Hamutali binti Yeremia, mkazi wa mji wa Libna. 19Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kama vile alivyofanya mfalme Yehoyakimu. 20Mwenyezi-Mungu aliwakasirikia sana watu wa Yerusalemu na Yuda, hata akawafukuza mbali naye. Sedekia alimwasi mfalme wa Babuloni.



2Wafalme24;1-20


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: