Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday, 9 May 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Wafalme 25......




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana
Tumshukuru Mungu katika yote...

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Mungu mwenye nguvu,Mungu wa walio hai,Mungu mwenye huruma,
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Mungu mwenye kuponya,Mungu wetu si kiziwi anasikia,

Mungu wetu anajibu,Mungu wetu si mwadamu mpaka aseme uongo,
Mungu wetu akisema ndiyo hakuna wakupinga
yeye ni mwanzo na yeye ni mwisho,Alfa na Omega...!

Asante kwa wema na fadhili zako kwetu

Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha
kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...!!


Mfarisayo mmoja alimwalika Yesu kula chakula nyumbani kwake. Akaingia nyumbani kwa huyo Mfarisayo, akakaa kula chakula. Basi, katika mji ule kulikuwa na mama mmoja mwenye dhambi. Alipopata habari kwamba Yesu yuko nyumbani kwa huyo Mfarisayo, alichukua chupa ya alabasta yenye marashi. Akaja, akasimama karibu na miguu yake Yesu, akilia, na machozi yake yakamdondokea Yesu miguuni. Huyo mwanamke akaipangusa miguu ya Yesu kwa nywele zake. Kisha akaibusu na kuipaka yale marashi. Yule Mfarisayo aliyemwalika Yesu alipoona hayo, akawaza moyoni mwake, “Kama mtu huyu angekuwa kweli nabii angejua huyu mwanamke ni wa namna gani, ya kwamba ni mwenye dhambi.”


Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea
Yahweh usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuokoe na
yule mwovu na kazi zake zote
Nguvu za giza,nguvu za mapepo,nguvu za mizimu,nguvu za mpinga 
Kristo zishindwe katika jina lililo kuu jina la Bwana wetu Yesu Kristo
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi
wetu Yesu Kristo wa Nazareti,yeye aliteseka kwanza ili sisi
tupate kupona,kwakupigwa kwake sisi tumepona...


Yesu akamwambia huyo Mfarisayo, “Simoni, ninacho kitu cha kukuambia.” Naye Simoni akamwambia, “Ndio Mwalimu, sema.” Yesu akasema, “Watu wawili walikuwa wamemkopa mtu fedha: Mmoja alikuwa amekopa denari 500, na mwingine hamsini. Waliposhindwa kulipa madeni yao, huyo mtu aliwasamehe wote wawili. Sasa ni yupi kati ya hao wawili atampenda zaidi huyo bwana?” Simoni akamjibu, “Ni dhahiri kwamba yule aliyesamehewa deni kubwa zaidi atampenda zaidi yule bwana.” Yesu akamwambia, “Sawa.”


Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji
Baba wa Mbinguni tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Jehovah ukatupe kama inavyokupendeza wewe....

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu
Familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Yahweh tunaomba ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Baba wa Mbinguni ukatamalaki na kutuatamia
Jehovah tukawe salama rohoni
Yahweh tunaomba ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mungu wetu tunaomba ukatupe macho ya kuona na masikio ya 
kusikia sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Mungu wetu tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote
za maisha yetu
Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na 
ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni
Ukatupe hekima,busara na upendo ukadumu kati yetu
neema yako na Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke
kama inavyokupendeza wewe...
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Halafu akamgeukia yule mwanamke na kumwambia Simoni, “Unamwona huyu mwanamke, sivyo? Basi, mimi nilipoingia hapa nyumbani kwako hukunipa maji ya kunawa miguu yangu; lakini mwanamke huyu ameniosha miguu yangu kwa machozi yake na kunipangusa kwa nywele zake. Wewe hukunisalimu kwa kunibusu, lakini huyu mwanamke tangu nilipoingia hapa amekuwa akiibusu miguu yangu. Wewe hukunionesha ukarimu wako kwa kunipaka mafuta kichwani, lakini huyu mwanamke amefanya hivyo kwa kunipaka mafuta miguu yangu. Kwa hiyo nakuambia amesamehewa dhambi zake nyingi kwa kuwa ameonesha upendo mkubwa. Mwenye kusamehewa kidogo, hupenda kidogo.” Basi, Yesu akamwambia yule mwanamke, “Umesamehewa dhambi zako.” Ndipo wale waliokuwa pamoja naye mezani wakaulizana, “Ni mtu wa namna gani huyu awezaye kusamehe dhambi?” Naye Yesu akamwambia yule mwanamke, “Imani yako imekuokoa; nenda kwa amani.”

Mungu wetu tazama wenye shida/tabu,wagonjwa,wenye njaa,
wanaopitia  magumu/majaribu mbalimbali,walio katika vifungo
vya yule mwovu,walio magerezani pasipo na hatia,walio kataliwa,
walio kata tamaa,wenye hofu na mashaka,walio kwama kibiashara,
kielemu,wanaotafuta watoto,waliomumizwa/jeruhiwa rohoni,
wote walio elemewa na mizigo mizito,wafiwa ukawae mfariji wao
ee Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaponye kimwili na kiroho pia
Yahweh tunaomba ukabariki kazi/mashamba yao wakapate
mazao ya kutosha kuweka akiba na kusaidia wengine
Mungu wetu tunaomba ukawavushe salama, ukawafungue na 
kuwaokoa,Yahweh tunaomba ukawaweke huru na haki ikatendeke
Baba wa Mbinguni tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Jehovah tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea na kufuata njia zako
Yahweh ukawabariki na kuwatendea sawsaawa na mapenzi yako
Mungu wetu tunaomba ukasikie na ukapokee sala/maombi yetu
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo yesu kwakuwanami/kunisoma
Baba wa Mbinguni akawaguse kwa mkono wake wenye nguvu
Akawabariki na kuwatendea kama inayompendeza yeye..
Nawapenda.

Maangamizi ya Yerusalemu

(2Nya 36:13-21; Yer 52:3b-11)

1Katika siku ya kumi ya mwezi wa kumi wa mwaka wa tisa wa utawala wake Sedekia, Nebukadneza mfalme wa Babuloni alifika na jeshi lake, akaushambulia mji wa Yerusalemu, akauzingira na kujenga ngome kuuzunguka. 2Mji uliendelea kuzingirwa mpaka mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Sedekia. 3Katika siku ya tisa ya mwezi wa nne njaa ilikuwa kali sana mjini hata hapakuwapo chakula chochote kwa ajili ya wakazi wake. 4Basi, sehemu ya ukuta wa mji ilibomolewa, nao askari wote wakakimbia wakati wa usiku wakipitia katika bustani ya mfalme kwenye lango katikati ya kuta mbili, wakaenda upande wa Araba, ingawa Wababuloni walikuwa wameuzunguka mji. 5Lakini jeshi la Wakaldayo lilimfuatia mfalme na kumteka kwenye tambarare za Yeriko, nao askari wake wote walimwacha, wakatawanyika. 6Basi, Wakaldayo walimteka mfalme, wakampeleka kwa mfalme wa Babuloni huko Ribla, naye akamhukumu. 7Halafu waliwaua wanawe akiona kwa macho yake mwenyewe, kisha wakamngoa macho yake. Mwishowe walimfunga kwa pingu, wakampeleka Babuloni.

Hekalu lateketezwa

(Yer 52:12-23)

8Katika siku ya saba ya mwezi wa tano wa mwaka wa kumi na tisa wa utawala wa Nebukadneza mfalme wa Babuloni, Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, aliingia Yerusalemu. 9Aliichoma moto nyumba ya Mwenyezi-Mungu, ikulu na nyumba zote za Yerusalemu; kila nyumba kubwa aliichoma moto. 10Nao askari wote wa Wakaldayo waliokuwa pamoja na kapteni na walinzi wa mfalme walizibomoa kuta zilizouzunguka mji wa Yerusalemu. 11Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, aliwapeleka uhamishoni watu waliokuwa wamebakia mjini na wale wote waliokuwa wamejisalimisha kwa mfalme wa Babuloni pamoja na watu wengine wote. 12Lakini aliacha baadhi ya watu waliokuwa maskini kabisa nchini. Aliwaacha watunze mizabibu na kulima mashamba. 13Wakaldayo walivunja vipandevipande nguzo za shaba ambazo zilikuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, pamoja na vikalio vyake, birika kubwa la shaba nyeusi lililokuwamo katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, wakaichukua shaba nyeusi mpaka Babuloni. 14Vilevile walichukua vyungu, masepetu, makasi na miiko iliyotumiwa kuchomea ubani na vyombo vingine vyote vya shaba nyeusi vilivyotumiwa katika huduma ya hekalu, 15wakachukua na vyetezo na mabakuli. Kapteni wa walinzi wa mfalme alipeleka mbali kila chombo cha dhahabu na kila chombo cha fedha. 16Shaba yote nyeusi aliyotumia Solomoni kutengeneza zile nguzo mbili, birika lile kubwa na vikalio kwa ajili ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu haikuweza kupimwa kwa uzito. 17Kila nguzo ilikuwa na urefu wa mita 8, na juu yake kulikuwa na kichwa cha shaba nyeusi, urefu wa kila kichwa ulikuwa mita 1.25. Kila kichwa kilizungushiwa mapambo ya makomamanga, yote ya shaba nyeusi.

Watu wa Yuda wapelekwa Babuloni

18Kisha Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme alimchukua mateka Seraya kuhani mkuu, Sefania kuhani wa pili pamoja na maofisa walinda milango watatu; 19alimchukua towashi mmoja huko mjini ambaye alikuwa akiwaongoza askari vitani, pamoja na watu watano mashuhuri wa mfalme ambao aliwakuta huko. Vilevile, alimchukua katibu wa kamanda mkuu wa jeshi ambaye alitunza kumbukumbu za jeshi pamoja na watu sitini mashuhuri ambao aliwakuta mjini Yerusalemu. 20Nebuzaradani kapteni wa walinzi aliwachukua watu hao, akawapeleka kwa mfalme wa Babuloni huko Ribla. 21Mfalme Nebukadneza wa Babuloni aliwapiga na kuwaua watu hao huko Ribla katika nchi ya Hamathi. Hivyo watu wa Yuda walichukuliwa mateka nje ya nchi yao.

Gedalia, gavana wa Yuda

(Yer 40:7-9; 41:1-3)

22Mfalme Nebukadneza wa Babuloni alimteua Gedalia mwana wa Ahikamu, mjukuu wa Shafani, kuwa mtawala wa watu wote wa Yuda ambao hawakupelekwa Babuloni. 23Kisha makapteni wote wa majeshi pamoja na watu wao waliposikia kuwa mfalme wa Babuloni alimteua Gedalia kuwa mtawala, walimwendea Gedalia huko Mizpa. Watu hao walikuwa Ishmaeli mwana wa Nethania, Yohanani mwana wa Karea, Seraya mwana wa Tanhumethi Mnetofathi, na Yezania mwana wa Mmaaka. 24Naye Gedalia aliapa mbele yao na watu wao, akasema, “Msiogope kwa sababu ya maofisa wa Wakaldayo. Kaeni nchini mumtumikie mfalme wa Babuloni na mambo yote yatawaendea vema.” 25Mnamo mwezi wa saba, Ishmaeli mwana wa Nethania, mjukuu wa Elishama aliyekuwa wa ukoo wa kifalme, alifika kwa Gedalia akiandamana na watu kumi, akamshambulia Gedalia, akamuua. Vilevile, aliwaua Wayahudi na Wakaldayo waliokuwa naye. 26Halafu, Waisraeli wote, wadogo kwa wakubwa pamoja na maofisa wa majeshi, waliondoka, wakaenda Misri, kwa sababu waliwaogopa Wakaldayo.

Yehoyakini aachiliwa

(Yer 52:31-34)
27Mnamo mwaka wa thelathini na mbili, Evil-merodaki mfalme wa Babuloni, alipoanza kutawala, mwaka huohuo alimsamehe Yehoyakini mfalme wa Yuda, akamtoa gerezani. Hiyo ilikuwa siku ya ishirini na saba ya mwezi wa kumi na mbili, mwaka wa thelathini na saba tangu Yehoyakini alipochukuliwa mateka. 28Aliongea naye vizuri na kumpa nafasi ya heshima kuliko wafalme wengine waliokuwa pamoja naye huko Babuloni. 29Basi, Yehoyakini alibadili mavazi yake ya kifungoni. Kila siku alikuwa anapata daima chakula chake kwa mfalme. 30Alipatiwa na mfalme mahitaji yake siku kwa siku, maisha yake yote.



2Wafalme25;1-30


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: