Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday, 19 June 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 1Mambo ya Nyakati 29...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?


Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana

Tumshukuru Mungu wetu kila wakati
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni
Uabudiwe Jehovah,Uhimidiwe Yahweh,Matendo yako ni makuu mno,
Matendo yako ni ya ajabu,Matendo yako yanatisha
Hakuna kama wewe ee Mungu wetu,Neema yako yatutosha
Baba wa Mbinguni...!!





Hapo mwanzo, Neno alikuwako; naye alikuwa na Mungu, naye alikuwa Mungu. Tangu mwanzo Neno alikuwa na Mungu. Kwa njia yake vitu vyote viliumbwa; hakuna hata kiumbe kimoja kilichoumbwa pasipo yeye. Yeye alikuwa chanzo cha uhai na uhai huo ulikuwa mwanga wa watu. Na mwanga huo huangaza gizani, nalo giza halikuweza kuushinda.



Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona...




Mungu alimtuma mtu mmoja jina lake Yohane, ambaye alikuja kuwaambia watu juu ya huo mwanga. Alikuja ili kwa ujumbe wake watu wote wapate kuamini. Yeye hakuwa huo mwanga, ila alikuja tu kuwaambia watu juu ya huo mwanga. Huu ndio mwanga halisi, mwanga unaokuja ulimwenguni, na kuwaangazia watu wote. Basi, Neno alikuwako ulimwenguni, na kwa njia yake ulimwengu uliumbwa, lakini ulimwengu haukumtambua. Alikuja katika nchi yake mwenyewe, nao walio wake hawakumpokea. Lakini wale waliompokea, wale waliomwamini, aliwapa uwezo wa kuwa watoto wa Mungu, ambao walizaliwa si kwa maumbile ya kibinadamu, wala kwa nguvu za kimwili, wala mapenzi ya mtu, bali kutokana na Mungu mwenyewe.



Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii

 Mungu wetu ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...




Naye Neno akawa mwanadamu, akakaa kwetu. Nasi tumeuona utukufu wake, utukufu wake yeye aliye Mwana wa pekee wa Baba; amejaa neema na ukweli. Yohane aliwaambia watu habari zake, akasema kwa sauti, “Huyu ndiye niliyemtaja wakati niliposema: ‘Anakuja mtu mmoja baada yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa.’” Kutokana na ukamilifu wake sisi sote tumepokea neema kupita neema. Maana Mungu alitoa sheria kwa njia ya Mose, nayo neema na kweli vimetujia kwa njia ya Yesu Kristo. Hakuna mtu aliyemwona Mungu kamwe. Mwana wa pekee aliye sawa na Mungu ambaye ameungana na Baba, ndiye aliyetujulisha habari za Mungu.



Baba wa Mbinguni tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopotia magumu/majaribu mbalimbali
watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Yahweh tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Jehovah tunaomba ukawaokoe,ukawavushe salama na  kuwalinda
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimaie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Baba wa Mbinguni ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.



Matoleo ya kujengea hekalu

1Mfalme Daudi akaumbia ule mkutano wote uliojumuika, “Solomoni, mwanangu, ambaye peke yake amechaguliwa na Mungu, bado yungali mdogo, na hana uzoefu mwingi, na kazi hii ni kubwa. Nyumba atakayoijenga si ya mwanadamu, bali ni ya Mungu, Mwenyezi-Mungu. 2Basi, nimejitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu wote kuiwekea nyumba ya Mungu wangu, akiba ya dhahabu ya kutengenezea vitu vya dhahabu, fedha ya kutengenezea vitu vya fedha, shaba ya kutengenezea vitu vya shaba, chuma cha kutengenezea vitu vya chuma, na miti ya kutengenezea vitu vya miti. Zaidi ya hayo, nimevitayarisha kwa wingi vito vya rangi na mawe ya kujazia vito vya njumu, mawe ya rangi, mawe ya thamani ya kila namna na marumaru. 3Tena, zaidi ya vyote nilivyotoa kwa ajili ya nyumba takatifu, ninayo hazina yangu binafsi ya dhahabu na fedha, na kwa sababu naipenda nyumba ya Mungu wangu, naitoa kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu: 4Tani 3,000 za dhahabu kutoka Ofiri, talanta 700 za fedha safi ya kuzifunikia kuta za nyumba, 5na kwa ajili ya kutengenezea vitu vya kila aina vitakavyotengenezwa na mafundi kwa mikono. Nimeweka dhahabu kwa ajili ya vyombo vya dhahabu, na fedha kwa ajili ya vyombo vya fedha. Ni nani basi atakayemtolea Mwenyezi-Mungu kwa hiari ili ajiweke wakfu hivi leo kwa Mwenyezi-Mungu?”
6Ndipo wakuu wa koo, viongozi wa makabila ya Israeli, makamanda wa maelfu na wa mamia; pia na maofisa wasimamizi wa kazi za mfalme walipotoa kwa hiari yao. 7Walitoa kwa ajili ya huduma za nyumba ya Mungu: Tani 170 za dhahabu, tani 340 za fedha, tani 620 za shaba na tani 3,400 za chuma. 8Wale ambao walikuwa na vito vya thamani walivitoa vitiwe katika hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, chini ya uangalizi wa Yehieli, Mgershoni. 9Ndipo watu wakafurahi kwa sababu walitoa kwa hiari, maana kwa moyo wao wote walimtolea Mwenyezi-Mungu kwa hiari, naye mfalme Daudi alifurahi sana.

Daudi amsifu Mungu

10Ndipo Daudi akamtukuza Mwenyezi-Mungu mbele ya mkutano wote, akisema: “Utukuzwe milele na milele, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa baba yetu Israeli. 11Ukuu ni wako, ee Mwenyezi-Mungu, una nguvu, utukufu, ushindi na enzi. Vyote vilivyoko mbinguni na duniani ni vyako. Ee Mwenyezi-Mungu, ufalme ni wako, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote. 12Utajiri na heshima hutoka kwako, vyote wavitawala. Uwezo na nguvu vimo mkononi mwako, nawe wawakuza uwapendao, na huwaimarisha wote. 13Sasa ee Mungu wetu, tunakushukuru na kulisifu jina lako tukufu.
14“Lakini, mimi ni nani, na watu wangu ni nani, hata tuweze kukupa kitu? Kwa maana vitu vyote vyatoka kwako, tumekutolea vilivyo vyako wewe mwenyewe. 15Sisi tu wageni mbele yako, na wasafiri kama walivyokuwa babu zetu wote. Siku zetu duniani ni kama kivuli kipitacho, hapa hakuna tumaini la kukaa. 16Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, wingi wote huu tuliotoa ili kukujengea nyumba kwa ajili ya utukufu wa jina lako takatifu, watoka mkononi mwako na yote ni yako. 17Ninajua Mungu wangu, kwamba wewe waujaribu moyo, nawe unapendezwa na unyofu. Nami, katika unyofu wa moyo wangu nimetoa vitu hivi vyote kwa hiari yangu, na sasa ninaona watu wako walioko hapa, wakikutolea kwa hiari na furaha. 18Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Israeli, babu zetu, dumisha maazimio ya namna hiyo na fikira za namna hiyo mioyoni mwa watu wako, na ielekeze mioyo ya watu wako kwako. 19Mjalie Solomoni mwanangu ili kwa moyo wote ashike amri zako, maamuzi na maagizo yako, atekeleze yote ili aweze kuijenga nyumba hii ya enzi niliyoifanyia matayarisho.”
20Kisha, mfalme Daudi aliwaambia wote waliokusanyika, “Msifuni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.” Na wote waliokusanyika wakamtukuza Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao, wakamsujudia na kumwabudu Mwenyezi-Mungu na kumtolea mfalme Daudi heshima. 21Wakamtolea tambiko Mwenyezi-Mungu. Siku ya pili yake wakamtolea sadaka za kuteketezwa: Mafahali 1,000, wanakondoo 1,000, pamoja na sadaka zao za vinywaji na tambiko nyingi kwa ajili ya Waisraeli wote. 22Basi siku hiyo walikula na kunywa kwa furaha kuu mbele ya Mwenyezi-Mungu.
Wakamtawaza Solomoni mwana wa Daudi, mara ya pili. Wakampaka mafuta awe mtawala kwa jina la Mwenyezi-Mungu, na Sadoki awe kuhani. 23Ndipo Solomoni akaketi katika kiti cha enzi cha Mwenyezi-Mungu, badala ya Daudi baba yake. Naye akafanikiwa, na taifa lote la Israeli likamtii. 24Viongozi wote, mashujaa na wana wote wa Daudi wakajiweka chini ya mfalme Solomoni. 25Mwenyezi-Mungu akampa Solomoni sifa nzuri machoni pa Waisraeli wote, akampa fahari ya kifalme ipitayo fahari ya mfalme awaye yote aliyeitawala Israeli kabla yake.

Muhtasari wa utawala wa Daudi

26Basi Daudi, mwana wa Yese, akawa mfalme juu ya Israeli yote. 27Na muda aliotawala juu ya Israeli ulikuwa miaka arubaini; miaka saba alitawala huko Hebroni na miaka thelathini na mitatu alitawala huko Yerusalemu. 28Alikufa akiwa mzee mwenye miaka mingi, ameshiba siku, akiwa na mali na heshima. Solomoni mwanawe, akawa mfalme badala yake. 29Habari za mfalme Daudi toka mwanzo hadi mwisho, zimeandikwa katika kumbukumbu za Samueli mwonaji, katika kumbukumbu za nabii Nathani na katika kumbukumbu za Gadi mwonaji. 30Hizo zasema pamoja na mambo ya utawala wake, uwezo wake, na mambo yaliyompata yeye, Waisraeli, na falme zote nchini.






1Mambo ya Nyakati29;1-30

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: