Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday, 21 June 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2Mambo ya Nyakati2...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote....

Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Sifa na Utukufu ni wako  ee Mungu wetu....!!



Mapendo yenu na yawe bila unafiki wowote. Chukieni jambo lolote ovu, zingatieni jema. Pendaneni kindugu; kila mmoja amfikirie kwanza mwenzake kwa heshima. Msilegee katika bidii, ila muwe wachangamfu rohoni katika kumtumikia Bwana. Tumaini lenu liwaweke daima wenye furaha; muwe na saburi katika shida, na kusali daima. Wasaidieni watu wa Mungu katika mahitaji yao; wapokeeni wageni kwa ukarimu. Watakieni baraka wote wanaowadhulumu nyinyi; naam, watakieni baraka na wala msiwalaani. Furahini pamoja na wenye kufurahi, lieni pamoja na wenye kulia. Ishini kwa kupatana vema nyinyi kwa nyinyi. Msijitakie makuu, bali jishughulisheni na madogo. Msijione kuwa wenye hekima sana. Msilipe ovu kwa ovu. Zingatieni mambo mema mbele ya wote. Kadiri inavyowezekana kwa upande wenu, muwe na amani na watu wote. Wapenzi wangu, msilipize kisasi, bali mwachieni Mungu jambo hilo; maana Maandiko Matakatifu yasema: “Kulipiza kisasi ni shauri langu; mimi nitalipiza, asema Bwana.” Zaidi ya hayo, Maandiko yasema: “Adui yako akiwa na njaa, mpe chakula; akiwa na kiu, mpe kinywaji. Maana kwa kufanya hivyo utamfanya apate aibu kali kama makaa ya moto juu ya kichwa chake.” Usikubali kushindwa na ubaya, bali ushinde ubaya kwa wema.


Tazama jana imepita Mungu wetu Leo ni siku
mpya Jehovah na Kesho ni siku nyingine  Yahweh..
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Kwakupigwa kwake sisi tumepona.....




Hii ndiyo amri yangu: Pendaneni; pendaneni kama nilivyowapenda nyinyi. Hakuna upendo mkuu zaidi kuliko upendo wa mtu atoaye uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Nyinyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru. Nyinyi siwaiti tena watumishi, maana mtumishi hajui anachofanya bwana wake. Lakini mimi nimewaita nyinyi rafiki, kwa sababu nimewajulisha yote ambayo nimeyasikia kutoka kwa Baba yangu. Nyinyi hamkunichagua mimi; mimi niliwachagueni na kuwatuma mwende mkazae matunda, matunda yadumuyo, naye Baba apate kuwapeni chochote mnachomwomba kwa jina langu. Basi, amri yangu kwenu ndiyo hii: Pendaneni.


Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji

Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni
tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe....




Yahweh  tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii 

Mungu wetu tunaomba ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu

Baba wa Mbinguni tukanene yaliyo yako
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi




Mwisho wa vitu vyote umekaribia. Kwa hiyo mnapaswa kuwa na utaratibu na kukesha ili muweze kusali. Zaidi ya yote pendaneni kwa moyo wote, maana upendo hufunika dhambi nyingi. Muwe na ukarimu nyinyi kwa nyinyi bila kunung'unika. Kila mmoja anapaswa kutumia kipaji alichojaliwa na Mungu kwa faida ya wengine kama wakili mwema wa zawadi mbalimbali za Mungu. Anayesema kitu, maneno yake na yawe kama maneno ya Mungu; anayetumikia anapaswa kutumikia kwa nguvu anayojaliwa na Mungu, ili katika mambo yote, Mungu atukuzwe kwa njia ya Yesu Kristo ambaye utukufu na nguvu ni vyake milele na milele! Amina.


Mungu Baba tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu
wote wanaopotia magumu/majaribu mbalimbali
watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Yahweh tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Jehovah tunaomba ukawaokoe,ukawavushe salama na  kuwalinda
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimaie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Baba wa Mbinguni ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee  kama inavyokupendeza wewe
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
sawasawa na mapenzi yake....

Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo 
wa Mungu Baba ukae nanyi daima....
Nawapenda.

Matayarisho ya kujenga Hekalu

(1Fal 5:1-18)

1Mfalme Solomoni alikata shauri kujenga nyumba ambamo Mwenyezi-Mungu ataabudiwa, na pia kujijengea yeye mwenyewe jumba la kifalme. 2Alipanga wanaume 70,000 wawe wachukuzi wa mizigo, 80,000 wawe wachonga mawe milimani na wengine 3,600 wawe wasimamizi wao.
3Kisha, Solomoni akatuma ujumbe kwa Hiramu, mfalme wa Tiro, akamwambia, “Nitendee na mimi kama ulivyomtendea baba yangu Daudi, ulipompelekea mierezi ya kujengea ikulu. 4Tazama, karibu nianze kujenga nyumba ya kumwabudia Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu. Nitaiweka wakfu, nayo itakuwa mahali pa kufukiza ubani wa harufu nzuri mbele yake, na mahali pa mikate ya kuwekwa mbele yake daima, na tambiko za kuteketezwa asubuhi na jioni na pia siku za Sabato, mwezi mwandamo, na sikukuu nyinginezo za Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kama alivyoiagiza Israeli milele. 5Nyumba ninayokusudia kujenga itakuwa kubwa sana, kwani Mungu wetu ni mkuu zaidi ya miungu yote. 6Lakini ni nani awezaye kumjengea nyumba ikiwa mbingu zenyewe hazimtoshi, wala mbingu za juu sana? Nami ni nani basi, hata nimjengee nyumba isipokuwa tu kama mahali pa kufukizia ubani mbele yake? 7Basi, sasa nitumie mtu mwenye ujuzi wa kutengeneza vyombo kwa dhahabu, fedha, shaba, na chuma, na nguo za rangi ya zambarau, za rangi nyekundu na ya samawati, ajuaye pia, kutia nakshi. Yeye atashirikiana katika kazi hiyo na mafundi walioko pamoja nami katika Yuda na Yerusalemu, ambao baba yangu Daudi aliwachagua. 8Tena nipelekee mierezi, miberoshi na misandali kutoka Lebanoni, kwa maana najua ya kwamba watumishi wako ni hodari sana wa kupasua mbao huko Lebanoni. Nao watumishi wangu watashirikiana na watumishi wako, 9ili wanipasulie mbao kwa wingi, maana nyumba ninayokusudia kujenga ni kubwa na ya ajabu. 10Kwa ajili ya watumishi wako, yaani maseremala watakaopasua mbao, nitatoa tani 2,000 za ngano iliyopondwa, tani 2,000 za shayiri, lita 400,000 za divai na lita 400,000 za mafuta.”
11Naye Hiramu, mfalme wa Tiro, alimjibu Solomoni kwa barua akisema:
“Kwa kuwa Mwenyezi-Mungu anawapenda watu wake, amekufanya uwe mfalme wao. 12Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, aliyeziumba mbingu na dunia! Amempa mfalme Daudi mwana mwenye hekima, busara na akili, atakayemjengea Mwenyezi-Mungu nyumba, na kujijengea ikulu. 13Sasa nakupelekea fundi stadi sana na mwenye akili, jina lake Huramu-abi, 14mwana wa mmoja wa wanawake wa kabila la Dani, na baba yake alikuwa mkazi wa Tiro. Yeye ana ujuzi mwingi wa kutumia dhahabu, fedha, shaba, chuma, mawe, miti, rangi ya zambarau, ya samawati, nyekundu na nguo za kitani safi. Tena ni hodari na anaweza kutia nakshi na kuchora michoro ya kila aina kufuatana na kielelezo chochote ambacho angepewa. Yeye atafanya kazi pamoja na mafundi wako, mafundi wa bwana wangu, Daudi, baba yako. 15Sasa basi, bwana wangu, vitu hivyo ulivyosema: Ngano, shayiri, mafuta na divai, tafadhali uvitume kwa watumishi wako, 16nasi tutapasua mbao kadiri ya mahitaji yako kutoka huko Lebanoni; kisha tutazifunga pamoja zielee majini mpaka Yopa. Kutoka huko utazipeleka Yerusalemu.”

Ujenzi wa Hekalu waanza

(1Fal 6:1-38)

17Mfalme Solomoni aliamuru sensa ifanywe ya wageni wote walioishi katika nchi ya Israeli. Sensa hii ni kama ile aliyoifanya Daudi, baba yake. Kulikuwa na wageni wapatao 153,600. 18Kati yao, 70,000 aliwapa kazi ya upagazi, 80,000 wakawa wachonga mawe milimani, na 3,600 wakawa wasimamizi ili wawahimize watu kufanya kazi.




2Mambo ya Nyakati2;1-17

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: