Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday, 20 August 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; Ezra 8...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua
na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!



Neno la Mwenyezi-Mungu lililomjia Sefania mwana wa Kushi, mwana wa Gedalia, mwana wa Amenia, mwana wa Hezekia, wakati wa utawala wa mfalme Yosia mwana wa Amoni, mfalme wa Yuda: Mwenyezi-Mungu asema: “Nitavifagilia mbali viumbe vyote duniani: Wanadamu, wanyama, ndege wa angani na samaki wa baharini; vyote nitaviangamiza. Waovu nitawaangamiza kabisa; wanadamu nitawafagilia mbali duniani. Nitaunyosha mkono wangu dhidi ya nchi ya Yuda, kadhalika na wakazi wote wa mji wa Yerusalemu. Nitaangamiza mabaki yote ya Baali kutoka nchi hii, na hakuna atakayetambua jina lao. Nitawaangamiza wote wanaosujudu juu ya paa, wakiabudu jeshi la mbinguni. Nitawaangamiza wale wanaoniabudu na kuapa kwa jina langu, hali wanaapa pia kwa jina la mungu Milkomu. Nitawaangamiza wote walioniacha mimi Mwenyezi-Mungu wote walioacha kunitafuta na kuniuliza shauri.”


Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine
Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachiliaq mikononi mwako
 Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona
Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona...

Nyamazeni mbele ya Bwana Mwenyezi-Mungu, kwani siku ya Mwenyezi-Mungu iko karibu. Mwenyezi-Mungu ameandaa tambiko, nao aliowaalika amewateua. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Katika siku ile ya karamu yangu, nitawaadhibu viongozi wa watu hao, kadhalika na wana wa mfalme pamoja na wote wanaoiga desturi za kigeni. Siku hiyo nitawaadhibu wote: Wanaoruka kizingiti cha nyumba kama wapagani, wanaojaza nyumba ya bwana wao vitu vya dhuluma na wizi. “Siku hiyo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, Kutasikika kilio kutoka Lango la Samaki, maombolezo kutoka Mtaa wa Pili, na mlio mkubwa kutoka milimani. Lieni enyi wakazi wa Makteshi! Wafanyabiashara wote wameangamia, wote wapimao fedha wamefutiliwa mbali.



Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...




Wakati huo nitaupekua mji wa Yerusalemu kwa taa, nitawaadhibu wanaoishi wametulia kama machicha ya divai, wote ambao husema mioyoni mwao: ‘Mwenyezi-Mungu hatafanya kitu: Chema au kibaya.’ Utajiri wao utanyakuliwa, na nyumba zao zitaachwa tupu! Watajijengea nyumba, lakini hawataishi humo. Watapanda mizabibu, lakini hawatakunywa divai yake.” Ile siku kubwa ya Mwenyezi-Mungu imekaribia, iko karibu na inakuja mbio. Mlio wa siku ya Mwenyezi-Mungu ni wa uchungu; hapo, shujaa atalia kwa sauti. Siku hiyo itakuwa siku ya ghadhabu, ni siku ya dhiki na uchungu, siku ya giza na huzuni; siku ya uharibifu na maangamizi, siku ya mawingu na giza nene. Siku hiyo ni ya mlio wa tarumbeta ya vita, dhidi ya miji yenye ngome na kuta ndefu. Kwa kuwa watu wamemkosea Mwenyezi-Mungu, yeye atawaletea dhiki kubwa, hivyo kwamba watatembea kama vipofu. Damu yao itamwagwa kama vumbi, na miili yao kama mavi. Fedha yao wala dhahabu yao havitaweza kuwaokoa katika siku hiyo ya ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu. Kwa moto wa wivu wake dunia yote itateketezwa. Kwa ukamilifu na kwa namna ya kutisha atawafanya wakazi wote duniani watoweke.


Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopotia magumu/majaribu mbalimbali
watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Yahweh tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Jehovah tunaomba ukawaokoe,ukawavushe salama na  kuwalinda
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimaie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Baba wa Mbinguni ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.


Watu waliorudi kutoka uhamishoni

1Ifuatayo ni orodha ya viongozi wa koo za watu waliorudi pamoja nami Ezra8:1 Ezra: Jina Ezra limeongezwa halimo katika Kiebrania. kutoka Babuloni, wakati wa utawala wa mfalme Artashasta: 2Gershomu, wa ukoo wa Finehasi. Danieli, wa ukoo wa Ithamari. Hatushi, wa ukoo wa Daudi, 3aliyekuwa mwana wa Shekania. Zekaria, wa ukoo wa Paroshi, pamoja na wanaume 150 wa ukoo wake, walioandikishwa pamoja. 4Eliehoenai, mwana wa Zerahia, wa ukoo wa Pahath-moabu, pamoja na wanaume 200. 5Shekania, mwana wa Yahazieli, wa ukoo wa Zatu,8:5 Zatu: Makala ya Kiebrania haina jina hili (taz pia 2:8). pamoja na wanaume 300. 6Ebedi, mwana wa Yonathani, wa ukoo wa Adini, pamoja na wanaume 50. 7Yeshaya, mwana wa Athalia, wa ukoo wa Elamu, pamoja na wanaume 70. 8Zebadia, mwana wa Mikaeli, wa ukoo wa Shefatia, pamoja na wanaume 80. 9Obadia, mwana wa Yehieli, wa ukoo wa Yoabu, pamoja na wanaume 218. 10Shelomithi, mwana wa Yosifia, wa ukoo wa Bani,8:10 Bani: Jina hili halimo katika makala ya Kiebrania. pamoja na wanaume 160. 11Zekaria, mwana wa Bebai, wa ukoo wa Bebai, pamoja na wanaume 28. 12Yohanani, mwana wa Hakatani, wa ukoo wa Azgadi, pamoja na watu 110. 13Elifeleti, Yeueli na Shemaya, wa ukoo wa Adonikamu, pamoja na wanaume 60, (hawa walirudi baadaye). 14Uthai na Zakuri, wa ukoo wa Bigwai, pamoja na wanaume 70.

Ezra atafuta Walawi kwa ajili ya hekalu

15Niliwakusanya pamoja watu wote kando ya mto uelekeao mji wa Ahava. Huko, tulipiga kambi kwa muda wa siku tatu. Niliwakagua watu wote pamoja na makuhani, lakini sikupata Walawi miongoni mwao. 16Niliita waje kwangu viongozi tisa: Eliezeri, Arieli, Shemaya, Elnathani, Yaribu, Elnathani, Nathani, Zekaria na Meshulamu, pamoja na waalimu wawili, Yoyaribu na Elnathani. 17Nikawatuma kwa Ido, kiongozi wa jamii ya watu kule Kasifia, nikimwomba yeye pamoja na wenzake wahudumu wa nyumba ya Mungu, watuletee watu watakaohudumu katika nyumba ya Mungu. 18Kwa neema yake Mungu, walituletea Sherebia, mtu mwenye busara na Mlawi wa ukoo wa Mahli, pamoja na wanawe na ndugu zake kumi na wanane. 19Walituletea pia Hashabia na Yeshaya, wote wa ukoo wa Merari, pamoja na ndugu zao ishirini. 20Mbali na hao, kulikuwa na wahudumu wa hekalu 220 ambao babu zao walikuwa wamechaguliwa na mfalme Daudi na maofisa wake kuwasaidia Walawi. Majina ya watu wote hawa yaliorodheshwa.

Watu wanaomba na kufunga

21Kisha, nilitoa maagizo kuwa sote tufike karibu na mto Ahava ili tufunge na kujinyenyekeza mbele za Mungu wetu na kumwomba atulinde na kutuongoza katika safari yetu pamoja na watoto wetu. 22Ingekuwa aibu kubwa kwangu kumwomba mfalme kikosi cha askari na wapandafarasi wa kutulinda na adui njiani maana nilikuwa nimekwisha mwambia kuwa Mungu wetu huwabariki wote wanaomtafuta, lakini huwachukia na kuwaadhibu wote wanaomwacha. 23Kwa hiyo tulifunga na kumwomba Mungu atulinde, naye aliyasikia maombi yetu.

Zawadi kwa ajili ya hekalu

24Halafu kati ya makuhani waliokuwa viongozi nilichagua kumi na wawili: Sherebia, Hashabia pamoja na wenzao kumi. 25Hawa niliwapimia kwa mizani fedha, dhahabu na vyombo ambavyo mfalme, washauri wake, maofisa wake pamoja na watu wa Israeli walivyokuwa wamevitoa kwa ajili ya sadaka ya nyumba ya Mungu wetu. 26Hivi ndivyo vitu nilivyowapimia: Fedha tani 22, vyombo 100 vya fedha, uzito wake kilo 70, dhahabu kilo 3400, 27mabakuli 20 ya dhahabu, uzito wake kilo 8, vyombo viwili vya shaba nzuri iliyongaa yenye thamani kama ya dhahabu.
28Kisha nikawaambia, “Nyinyi ni wakfu kwa Mwenyezi-Mungu. Kadhalika vyombo ni wakfu na fedha na dhahabu ni matoleo ya hiari kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu. 29Tafadhali vilindeni na vitunzeni mpaka mtakapovipima mbele ya makuhani wakuu, Walawi na viongozi wa koo za Israeli, huko Yerusalemu katika vyumba vya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.” 30Basi, makuhani na Walawi wakachukua fedha, dhahabu na vyombo vyote walivyopimiwa, ili kuvipeleka mjini Yerusalemu katika nyumba ya Mungu wetu.

Kurudi Yerusalemu

31Mnamo siku ya kumi na mbili ya mwezi wa kwanza, tulisafiri kutoka mto Ahava, kwenda Yerusalemu. Mungu wetu alikuwa pamoja nasi, akatulinda na maadui na washambuliaji wa njiani. 32Tulipofika Yerusalemu, tulipumzika kwa muda wa siku tatu. 33Mnamo siku ya nne, tukiwa ndani ya nyumba ya Mungu wetu, tulipima ile fedha, dhahabu na vile vyombo, kisha tukamkabidhi kuhani Meremothi, mwana wa Uria. Meremothi alikuwa pamoja na Eleazari, mwana wa Finehasi, na Walawi wawili, Yozabadi, mwana wa Yeshua, na Noadia, mwana wa Binui. 34Kila kitu kilihesabiwa na kupimwa na wakati huo uzito wa kila kitu uliandikwa.
35Kisha, watu wote waliorudi kutoka uhamishoni walimtolea Mungu wa Israeli sadaka zao za kuteketezwa. Walitoa mafahali 12 kwa ajili ya Israeli yote, kondoo madume 96 na wanakondoo 77; pia walitoa mbuzi 12 kama sadaka ya kuondoa dhambi. Wanyama wote hawa walitolewa kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa Mwenyezi-Mungu. 36Aidha, waliwakabidhi manaibu wa mfalme na watawala wa mkoa wa magharibi ya Eufrate mwongozo waliopewa na mfalme, nao walitoa msaada kwa watu na kwa ajili ya nyumba ya Mungu.




Ezra8;1-36

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: