Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday, 21 August 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; Ezra 9...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?


Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana
Tumshukuru Mungu wetu kila wakati
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni
Uabudiwe Jehovah,Uhimidiwe Yahweh,Matendo yako ni makuu mno,
Matendo yako ni ya ajabu,Matendo yako yanatisha
Hakuna kama wewe ee Mungu wetu..

Neema yako yatutosha Baba wa Mbinguni...!!



Anayekaa chini ya ulinzi wa Mungu Mkuu, anayeishi chini ya kivuli cha Mungu Mwenye Nguvu, ataweza kumwambia Mwenyezi-Mungu: “Wewe ni kimbilio langu na ngome yangu; Mungu wangu, ninayekutumainia!” Hakika Mungu atakuokoa katika mtego; atakukinga na maradhi mabaya. Atakufunika kwa mabawa yake, utapata usalama kwake; mkono wake utakulinda na kukukinga.


Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona...



Huna haja ya kuogopa vitisho vya usiku, wala shambulio la ghafla mchana; huna haja ya kuogopa baa lizukalo usiku, wala maafa yanayotokea mchana. Hata watu elfu wakianguka karibu nawe, naam, elfu kumi kuliani mwako, lakini wewe baa halitakukaribia. Kwa macho yako mwenyewe utaangalia, na kuona jinsi watu waovu wanavyoadhibiwa. Wewe umemfanya Mwenyezi-Mungu kuwa kimbilio lako; naam, Mungu aliye juu kuwa kinga yako. Kwa hiyo, hutapatwa na maafa yoyote; nyumba yako haitakaribiwa na baa lolote.


Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii

 Mungu wetu ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye barua  njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...



Maana Mungu atawaamuru malaika zake, wakulinde popote uendapo. Watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa kwenye jiwe. Utakanyaga simba na nyoka, utawaponda wana simba na majoka. Mungu asema: “Nitamwokoa yule anipendaye; nitamlinda anayenitambua! Akiniita, mimi nitamwitikia; akiwa taabuni nitakuwa naye; nitamwokoa na kumpa heshima. Nitamridhisha kwa maisha marefu, nitamjalia wokovu wangu.”


Baba wa Mbinguni tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu
wote wanaopotia magumu/majaribu mbalimbali
watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Yahweh tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Jehovah tunaomba ukawaokoe,ukawavushe salama na  kuwalinda
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimaie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Baba wa Mbinguni ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee  kama inavyokupendeza wewe
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
sawasawa na mapenzi yake....

Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo 
wa Mungu Baba ukae nanyi daima....
Nawapenda.


Waisraeli wanaoa wanawake wa kigeni

1Baada ya mambo haya yote kutendeka, viongozi walinijia na kunipa taarifa ifuatayo: “Watu wa Israeli, makuhani na Walawi hawajajitenga na wakazi wa nchi ambao wanatenda machukizo: Waamoni, Wamoabu na Wamisri, Wakanaani, Wahiti, Waperizi, Wayebusi na Waamori. 2Wayahudi wanaoa wanawake wa kigeni na kuwaoza wavulana wao pia. Hivyo, taifa takatifu la Mungu limechanganyika na watu wa mataifa mengine Isitoshe, maofisa na wakuu ndio wa kwanza kutenda maovu hayo.”
3Nilipoyasikia maelezo hayo, nilizirarua nguo zangu na joho langu, nikazingoa nywele zangu na ndevu zangu kwa huzuni kubwa na kuketi chini kwa hofu. 4Ndipo watu wote walioshikwa na hofu kwa sababu ya maneno aliyosema Mungu wa Israeli kuhusu makosa ya wale waliorudi kutoka uhamishoni walipoanza kukusanyika karibu nami hali nikikaa katika hofu hadi jioni, wakati wa kutoa tambiko.
5Jioni, wakati wa kutoa tambiko ulipofika, niliinuka mahali hapo nilipokuwa nimekaa kwa huzuni huku nguo zangu zimeraruka pamoja na joho, nikapiga magoti na kumnyoshea mikono yangu Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, na kuomba, 6nikisema, “Ee Mungu wangu, naona aibu kubwa sana kukiinua kichwa changu mbele yako. Dhambi zetu zimerundikana kupita hata vichwa vyetu; naam, makosa yetu yanafika hata mbinguni. 7Tangu nyakati za babu zetu hadi sasa, sisi watu wako tumekukosea sana. Na kwa sababu ya dhambi zetu, sisi, wafalme wetu na makuhani wetu tumetiwa mikononi mwa wafalme wa nchi za kigeni, tukauawa, tukachukuliwa mateka na kunyanganywa mali zetu. Na hadi hivi leo, tumetiwa haya kupita kiasi. 8Lakini sasa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kwa muda mfupi umetuonesha huruma yako na kuwawezesha baadhi yetu kuponyoka kutoka utumwani na kuishi kwa usalama mahali hapa patakatifu. Badala ya utumwa, umetupa furaha na maisha mapya. 9Hukutuacha tuishi utumwani ingawa tulikuwa tu watumwa Uliwafanya wafalme wa Persia wawe wema kwetu na kuturuhusu tuishi na kuijenga nyumba yako iliyokuwa imebomoka, ukatufanya tukae salama hapa Yuda na Yerusalemu.
10“Lakini sasa, ee Mungu wetu, tuseme nini baada ya hayo yote? Maana, tumeziasi amri zako 11ulizotupa kwa njia ya watumishi wako manabii ukisema: ‘Nchi mnayoiendea na ambayo itakuwa mali yenu ni nchi iliyo najisi yenye uchafu wa wakazi toka nchi mbalimbali, kwa machukizo yao, wameijaza unajisi tele kila mahali. 12Taz Kut 13:21-22 Kwa hiyo, msiwaoze watu hao binti zenu, wala msiwaruhusu wavulana wenu kuwaoa binti zao. Pia, msishughulikie usalama au mafanikio yao, ili nyinyi wenyewe muweze kuwa na nguvu, na mfaidi mema ya nchi hiyo na kuwaachia watoto wenu kama urithi milele.’ 13Taz Kut 19:18–23:33 Hata baada ya yote yaliyotupata kwa sababu ya maovu yetu na makosa yetu mengi, tunajua kwamba adhabu uliyotupa, ee Mungu wetu, ni ndogo ikilinganishwa na makosa yetu, na umewaacha baadhi yetu hai. 14Je, tutavunja amri zako tena na kuoana na watu hawa watendao maovu haya? Je, hutatukasirikia na kutuangamiza kabisa, asibaki hata mmoja wetu hai wala yeyote wa kutoroka? 15Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, wewe ni mwenye haki na umetuacha tubaki kama tulivyo hivi leo. Tunaungama makosa yetu mbele yako, tukijua kuwa hakuna aliye na haki yoyote ya kuja mbele yako kwa ajili ya makosa haya.”




Ezra9;1-15

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: