|
Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Haleluyah ni siku/wiki/mwezi mwingine tena Mungu wetu ametuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....
Tumshukuru Mungu wetu katika yote...
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!
Ndugu zangu, napenda mfahamu kwamba mambo yote yaliyonipata yamesaidia sana kuieneza Injili. Kutokana na hayo, walinzi wote wa ikulu pamoja na wengine wote hapa wanafahamu kwamba niko kifungoni kwa sababu mimi namtumikia Kristo. Na huku kuweko kwangu kifungoni kumewafanya ndugu wengi kuwa na imani kwa Bwana, hata wanazidi kuwa hodari katika kuutangaza ujumbe wa Mungu bila hofu. Kweli, baadhi yao wanamhubiri Kristo kwa sababu wana wivu na ni watu wagomvi; lakini wengine wanamhubiri Kristo kwa nia nzuri. Hawa wanafanya hivyo kwa upendo, kwani wanajua kwamba Mungu amenipa jukumu hili la kuitetea Injili. Hao wengine wanamtangaza Kristo kwa mashindano na si kwa moyo mnyofu, wakidhani kwamba wataniongezea mateso yangu kifungoni.
|
Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine
Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea Jehovah usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona
Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona...
Haidhuru! Mimi nafurahi ikiwa tu watu wanamhubiri Kristo kwa kila njia, iwe ni kwa nia nzuri au kwa nia mbaya. Tena nitaendelea kufurahi, kwani najua kwamba kwa sala zenu na kwa msaada wa Roho wa Yesu Kristo, nitakombolewa. Hamu yangu kubwa na tumaini langu ni kwamba kwa vyovyote sitashindwa katika kutimiza wajibu wangu, bali nitakuwa na moyo thabiti kila wakati na hasa wakati huu, ili kwa maisha yangu yote, niwapo hai au nikifa, nimpatie Kristo heshima. Kwangu, kuishi ni Kristo, na kufa ni faida zaidi. Lakini, kama kwa kuishi nitaweza kufanya kazi yenye faida zaidi, basi, sijui nichague lipi! Nakabiliwa na haya mawili yaliyo sawa. Natamani kuyaacha maisha haya nikakae pamoja na Kristo, jambo ambalo ni bora zaidi; lakini ni jambo la maana zaidi kwenu kama nikiendelea kuishi. Nina hakika ya jambo hili, na hivyo najua kwamba nitaendelea kuishi pamoja nanyi nyote, ili nipate kuongeza maendeleo yenu na furaha katika imani.
Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe
Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu, watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...
Basi, jambo muhimu ni kwamba mwenendo wenu uambatane na matakwa ya Injili ya Kristo, ili kama nikiweza kuja kwenu au nisipoweza, nipate walau kusikia kwamba mnasimama imara mkiwa na lengo moja, na kwamba mnapigana vita kwa pamoja na mnayo nia moja kwa ajili ya imani ya Injili. Msiwaogope maadui zenu, bali muwe hodari daima, na hiyo itawathibitishia kwamba wao watashindwa, nanyi mtashinda kwani Mungu mwenyewe ndiye anayewapeni ushindi. Maana nyinyi mmepewa fadhili ya kumtumikia Kristo si tu kwa kumwamini bali pia kwa kuteswa kwa ajili yake. Sasa mwaweza kushirikiana nami katika kupigana vita. Vita hivi ni vile mlivyoona nikipigana pale awali na ambavyo bado napigana sasa kama mnavyosikia.
Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopotia magumu/majaribu mbalimbali watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu kila mmoja na mahitaji yake Yahweh tunaomba ukaonekane katika maisha yao Jehovah tunaomba ukawaokoe,ukawavushe salama na kuwalinda Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako wakasimaie Neno lako nalo likaweke huru Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu Baba wa Mbinguni ukapokee sala/maombi yetu Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele Amina...!!
Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye.... Nawapenda.
|
Ezra anawasomea watu sheria
1Kisha watu wote, kwa nia moja, wakakusanyika mjini Yerusalemu kwenye uwanja ulio karibu na Lango la Maji. Wakamwambia Ezra, mwandishi, kukileta kitabu cha sheria ya Mose ambayo Mwenyezi-Mungu aliwapa watu wa Israeli. 2Ezra, ambaye alikuwa kuhani, akaenda na kukileta kitabu cha sheria ya Mose mbele ya mkutano mzima, wanaume kwa wanawake na yeyote aliyeweza kuielewa hiyo sheria aliposikia. Siku hiyo ilikuwa ni siku ya kwanza ya mwezi wa saba. 3Kisha watu wote wanaume kwa wanawake na yeyote aliyeweza kuelewa, Ezra aliwasomea sheria ya Mose akiwa mbele ya Lango la Maji tangu asubuhi hadi adhuhuri. Watu wote wakatega masikio yao kusikiliza kwa makini kitabu cha sheria.
4Ezra, mwandishi, alikuwa amesimama kwenye mimbari ya mbao iliyotengenezwa kwa kusudi hilo; na kwenye mkono wake wa kulia walikuwa wamesimama Matithia, Shema, Anaya, Uria, Hilkia na Maaseya; na kwenye mkono wake wa kushoto walikuwa wamesimama Pedaya, Mishaeli, Malkiya, Hashumu, Hashbadana, Zekaria na Meshulamu.
5Ezra akasimama kwenye mimbari, mbele ya watu wote, nao wakawa wanamkazia macho yao kwa utulivu mkubwa. Mara tu Ezra alipokifungua kitabu cha sheria, watu wote wakasimama wima. 6Ezra akamshukuru Mwenyezi-Mungu, Mungu Mkuu na watu wote wakaitikia “Amina! Amina!” Huku wakiwa wameinua mikono yao juu. Kisha wakamsujudia Mungu huku nyuso zao zikigusa ardhi.
7Walawi wafuatao walisaidia kuwaelewesha watu sheria: Yeshua, Bani, Sherebia, Yamini, Akubu, Shabethai, Hodia, Maaseya, Kelita, Azaria, Yozabadi, Hanani na Pelaya; walifanya hivyo kila mmoja akiwa amesimama mahali pake. 8Wakasoma vizuri toka kitabu cha sheria ya Mungu na kuifafanua na watu wote waliweza kuielewa. 9Watu waliposikia sheria, waliguswa mioyoni mwao, ndipo wote walipoanza kulia. Hivyo Nehemia aliyekuwa mtawala na Ezra kuhani na mwandishi, pamoja na Walawi waliowafundisha watu waliwaambia watu wote, “Siku hii ni siku takatifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, hivyo msiomboleze wala kulia. 10Sasa rudini nyumbani mkafanye sherehe, mle vinono na kunywa divai nzuri, lakini kumbukeni kuwapelekea wale ambao hawana cha kutosha; kwani leo ni siku takatifu kwa Bwana wetu. Msihuzunike kwa sababu furaha anayowajalia Mwenyezi-Mungu itawapeni nguvu.”
11Hivyo, Walawi wakawatuliza watu wote, wakisema, “Tulieni kwani siku ya leo ni takatifu; msihuzunike.” 12Watu wote wakarudi nyumbani kwao kula na kunywa; wakifurahi na kuwagawia wengine chakula kwa kuwa waliyaelewa yote waliyotangaziwa.
13Kesho yake, wakuu wa koo pamoja na makuhani na Walawi wakakusanyika kwa Ezra mwandishi, ili kujifunza sheria. 14Wakagundua kuwa, imeandikwa katika kitabu cha sheria kuwa Mwenyezi-Mungu alimwamuru Mose, kwamba watu wanapaswa kukaa vibandani wakati wa sikukuu ya mwezi wa saba. 15Hivyo wakatangaza katika miji yao yote na huko Yerusalemu, wakisema, “Nendeni milimani, mkalete matawi ya mizeituni, mizeituni mwitu, mihadasi, mitende na miti mingineyo ili kujengea vibanda, kama ilivyoandikwa.”
16Basi, watu wakaenda kuleta matawi, wakajijengea vibanda kila mtu kwenye dari na kwenye baraza ya nyumba yake, kwenye baraza za nyumba ya Mungu, kwenye uwanja wa Lango la Maji na uwanja wa Lango la Efraimu. 17Watu wote waliorudi kutoka uhamishoni wakatengeneza vibanda wakaishi humo. Hii ilikuwa ni mara ya kwanza watu kuishi katika vibanda tangu wakati Yeshua, mwana wa Nuni alipokuwa akiishi. Watu walifurahi sana. 18Kila siku, tangu siku ya kwanza hadi ya mwisho, Ezra aliwasomea watu kitabu cha sheria ya Mungu. Waliadhimisha sikukuu hiyo kwa muda wa siku saba, na siku ya nane wakafanya mkutano mkubwa wa kufunga sikukuu, kama ilivyoagizwa.
Nehemia8;1-18
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
No comments:
Post a Comment