Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday, 12 September 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; Esta 2.....



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?


Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana
Tumshukuru Mungu wetu kila wakati
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni
Uabudiwe Jehovah,Uhimidiwe Yahweh,Matendo yako ni makuu mno,
Matendo yako ni ya ajabu,Matendo yako yanatisha
Hakuna kama wewe ee Mungu wetu..

Neema yako yatutosha Baba wa Mbinguni...!!



Mpeni Mwenyezi-Mungu heshima enyi viumbe vya mbinguni, semeni Mwenyezi-Mungu ni mtukufu na mwenye nguvu. Semeni jina la Mwenyezi-Mungu ni tukufu. Mwabuduni katika mahali pake patakatifu. Sauti ya Mwenyezi-Mungu yasikika juu ya maji; Mungu mtukufu angurumisha radi, sauti ya Mwenyezi-Mungu yasikika juu ya bahari! Sauti ya Mwenyezi-Mungu ina nguvu, sauti ya Mwenyezi-Mungu imejaa fahari. Sauti ya Mwenyezi-Mungu huvunja mierezi; Mwenyezi-Mungu avunja mierezi ya Lebanoni.


Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona...


Huirusha milima ya Lebanoni kama ndama, milima ya 
Sirioni kama mwananyati. Sauti ya Mwenyezi-Mungu hutoa miali ya moto. Sauti ya Mwenyezi-Mungu hutetemesha jangwa, Mwenyezi-Mungu hutetemesha jangwa la Kadeshi.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii

 Mungu wetu ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye barua  njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Sauti ya Mwenyezi-Mungu huitikisa mivule, hukwanyua majani ya miti msituni, na hekaluni mwake wote wasema: “Utukufu kwa Mungu!” Mwenyezi-Mungu ameketi juu ya gharika; Mwenyezi-Mungu ni mfalme atawalaye milele. Mwenyezi-Mungu na awape watu wake nguvu! Mwenyezi-Mungu na awabariki watu wake kwa amani!

Baba wa Mbinguni tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu
wote wanaopotia magumu/majaribu mbalimbali
watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Yahweh tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Jehovah tunaomba ukawaokoe,ukawavushe salama na  kuwalinda
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimaie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Baba wa Mbinguni ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee  kama inavyokupendeza wewe
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
sawasawa na mapenzi yake....

Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo 
wa Mungu Baba ukae nanyi daima....
Nawapenda.


Esta anateuliwa kuwa malkia

1Baadaye, hasira yake ilipokwisha tulia, mfalme Ahasuero alimkumbuka Vashti, akawa anatafakari juu ya ukaidi wake na hatua iliyochukuliwa dhidi yake. 2Basi, watumishi wake, waliokuwa wanamhudumia yeye binafsi, wakamshauri, “Kuna wasichana wengi wazuri; kwa nini usitafutiwe mmoja? 3Unaweza kuteua maofisa katika kila mkoa wa utawala wako, na kuwaagiza wawalete wasichana wazuri wote kwenye nyumba ya wanawake hapa Susa, mji mkuu. Halafu wawekwe chini ya uangalizi wa Hegai, towashi mwangalizi wa wanawake wako; na hapo wapewe mafuta na vifaa vingine ili wajirembeshe zaidi. 4Yule atakayekupendeza zaidi, na afanywe malkia badala ya Vashti.” Mfalme akaona shauri hilo ni jema, akafanya hivyo.
5Mjini Susa, palikuwa na mtu mmoja Myahudi, jina lake Mordekai, mwana wa Yairi mwana wa Shimei, mwana wa Kishi wa kabila la Benyamini. 6Mordekai alikuwa miongoni mwa watu wale waliochukuliwa mateka wakati mfalme Yekonia wa Yuda alipotekwa na mfalme Nebukadneza wa Babuloni.
7Alikuwa na binamu, Esta, ambaye jina lake la Kiebrania lilikuwa Hadasa. Esta alikuwa msichana mzuri wa sura na umbo. Wazazi wake walipofariki, Mordekai alimchukua Esta, akamlea kama binti yake.
8Amri ya mfalme ilipotangazwa hadharani, wasichana wengi walipelekwa Susa, mji mkuu, wakawekwa chini ya ulinzi wa Hegai. Esta naye, alipelekwa kwenye ikulu ya mfalme, akawekwa chini ya uangalizi wa Hegai, yule mwangalizi wa wanawake. 9Hegai alipendezwa na Esta hata kiasi cha kumpendelea. Bila kupoteza wakati, alimpa Esta mafuta na chakula maalumu. Isitoshe, alimhamishia mahali pazuri kabisa katika nyumba hiyo ya wanawake, akamteulia watumwa wa kike saba kutoka ikulu ya mfalme, wamhudumie.
10Esta alikuwa hajajitambulisha ukoo wala kabila lake, maana Mordekai alikuwa amemwonya asifanye hivyo. 11Kila siku Mordekai alipitapita mbele ya ua wa nyumba hiyo ya wanawake ili apate kujua hali ya Esta na mambo ambayo yangempata.
12Kipindi cha hao wasichana kujiremba na kujitia uzuri kilichukua mwaka mmoja: Miezi sita ya kwanza walitumia mafuta ya manemane, na miezi sita ya mwisho walitumia manukato na mafuta mengineyo. Baada ya hapo, kila mwali, peke yake, alipelekwa kwa mfalme Ahasuero. 13Wakati wa kwenda kwa mfalme, kila mwali alipewa kila alichotaka kuchukua kutoka nyumba ya wanawake kwenda nacho ikulu. 14Jioni ulikuwa ndio wakati wa kwenda, na kesho yake asubuhi, mwali huyo alipelekwa katika nyumba nyingine ya wanawake, chini ya Shaashgazi, towashi msimamizi wa masuria wa mfalme. Mwali haikumpasa kurudi kwa mfalme, isipokuwa kama mfalme amependezwa naye kiasi cha kuagiza aitwe kwa jina.
15Wakati uliwadia wa Esta kwenda kwa mfalme. Huyo, binti Abihaili, binamu ya Mordekai, na ambaye alilelewa na Mordekai, hakuomba chochote zaidi ya kile alichopangiwa na Hegai, towashi mwangalizi wa wanawake wa mfalme. Kila mtu aliyemwona Esta, alipendezwa naye. 16Basi, Esta alipelekwa ikulu kwa mfalme katika mwaka wa saba wa utawala wa mfalme Ahasuero, mwezi wa kumi uitwao Tebethi. 17Mfalme alipendezwa zaidi na Esta kuliko alivyopendezwa na wanawake wengine wote. Alipendwa sana kuliko wasichana wengine. Basi, mfalme akamvika taji ya kimalkia kichwani, akamfanya malkia badala ya Vashti. 18Kisha mfalme akaandaa karamu kubwa kwa heshima ya Esta, akawaalika viongozi na watumishi wote wa serikali yake. Pia, mfalme alitangaza msamaha wa kodi2:18 msamaha wa kodi: Au siku ya mapumziko. katika mikoa yote, akatoa zawadi nyingi kulingana na hadhi yake ya kifalme.

Mordekai aokoa maisha ya mfalme

19Wasichana walipokusanyika mara ya pili, Mordekai alikuwa ameketi penye lango la mfalme.2:19 ameketi penye lango la mfalme: Kunaweza kumaanisha kwamba Mordekai alikuwa ameajiriwa kama msimamizi. 20Esta alikuwa bado hajajitambulisha ukoo wala kabila lake kama Mordekai alivyokuwa amemwonya asifanye hivyo; naye Esta alimtii kama alivyokuwa akimtii wakati wa utoto wake, alipolelewa naye.
21Wakati Mordekai alipokuwa anaketi penye lango la mfalme, Bigthana na Tereshi, wawili baadhi ya matowashi wa mfalme waliokuwa walinzi wa milango ya vyumba vya mfalme, waliudhika kiasi cha kula njama kumuua mfalme Ahasuero. 22Mordekai aliingamua njama hiyo, akamjulisha malkia Esta, naye Esta akampasha habari mfalme. 23Uchunguzi ulipofanywa, iligunduliwa kuwa ni kweli; basi, watu hao wawili wakatundikwa kwenye mti wa kuulia. Habari kuhusu tukio hilo iliandikwa katika kitabu cha kumbukumbu mbele ya mfalme.



Esta2;1-23

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: