Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday, 20 September 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; Esta 8.....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana..
Tumshukuru Mungu wetu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Baba wa Upendo,Baba wa faraja,Baba wa huruma,Baba wa Baraka
Mungu mwenye nguvu,Mungu mwenye kuponya
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Muweza wa yote
Wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho,Alfa na Omega...!!


Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Sifa na Utukufu tunakurudishia wewe ee Mungu wetu....!!



Kisha wakaidharau nchi ile ya kupendeza, kwa sababu hawakuwa na imani na ahadi ya Mungu. Walinungunika mahemani mwao, wala hawakumsikiliza Mwenyezi-Mungu. Hivyo Mungu akainua mkono akaapa kwamba atawaangamizia jangwani; atawatawanya wazawa wao kati ya watu, na kuwasambaza duniani kote.


Tazama Jana imepita ee Mungu wetu Leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingineJehovah...
Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha

na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti 

yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Kisha wakajiunga kumwabudu Baali kule Peori, wakala tambiko zilizotambikiwa mizimu. Waliichochea hasira ya Mwenyezi-Mungu kwa matendo yao, maradhi mabaya yakazuka kati yao. Lakini Finehasi akasimama kufanya malipizi, na yale maradhi yakakoma. Jambo hilo lakumbukwa kwa heshima yake, tangu wakati huo na nyakati zote. Walimkasirisha Mungu penye maji ya Meriba, Mose akapata taabu kwa ajili yao. Walimtia Mose uchungu rohoni, hata akasema maneno bila kufikiri. Hawakuwaua watu wa mataifa mengine kama Mwenyezi-Mungu alivyowaamuru. Bali walijumuika na watu wa mataifa, wakajifunza kutenda mambo yao. Waliabudu sanamu za miungu yao, nazo zikawa mtego wa kuwaangamiza. Waliwaua watoto wao wa kiume na wa kike, wakawatoa tambiko kwa pepo. Walimwaga damu ya wasio na hatia, damu ya watoto wao wa kiume na wa kike ambao waliwatoa tambiko kwa sanamu za Kanaani, nayo nchi ikatiwa unajisi kwa mauaji hayo. Hivyo wakafanywa najisi kwa matendo yao, 2wakakosa uaminifu kwa Mungu kama wazinzi.


Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji

Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni
tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe....



Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii

 Mungu wetu ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu

Baba wa Mbinguni tukanene yaliyo yako
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Tukawe barua njema  ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...




Hasira ya Mwenyezi-Mungu ikawawakia watu wake, akachukizwa sana na hao waliokuwa mali yake. Akawatia makuchani mwa watu wa mataifa, hao wenye kuwachukia wakawatawala. Maadui zao waliwakandamiza, wakawatumikisha kwa nguvu. Mara nyingi Mungu aliwaokoa watu wake, lakini wao wakachagua kumwasi, wakazidi kuzama katika uovu wao. Hata hivyo Mungu alizijali taabu zao, wakati aliposikia kilio chao; kwa ajili yao alilikumbuka agano lake, akawahurumia kwa wingi wa fadhili zake. Aliwafanya waliowakandamiza wawaonee huruma. Utuokoe, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, utukusanye pamoja kutoka kwa mataifa, tupate kulisifu jina lako takatifu, na kuona fahari juu ya sifa zako. Asifiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, tangu milele na hata milele! Na watu wote waseme: “Amina!” Asifiwe Mwenyezi-Mungu!


Mungu Baba tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabuwote wanaopotia magumu/majaribu mbalimbali
watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Yahweh tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Jehovah tunaomba ukawaokoe,ukawavushe salama na  kuwalinda
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimaie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Baba wa Mbinguni ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.


Wayahudi waruhusiwa kujihami

1Siku hiyohiyo, mfalme Ahasuero alimkabidhi malkia Esta mali yote ya Hamani, adui ya Wayahudi. Esta akamjulisha mfalme kwamba Mordekai ni jamaa yake. Basi, tangu wakati huo, Mordekai akaruhusiwa kumwona mfalme. 2Mfalme akaivua pete yake ya mhuri aliyokuwa amemnyanganya Hamani, akampa Mordekai. Esta naye akampa Mordekai mamlaka juu ya mali ya Hamani.
3Kisha Esta akazungumza tena na mfalme; akajitupa chini, miguuni pa mfalme, huku analia, akamsihi mfalme aukomeshe mpango mbaya ambao Hamani, wa uzao wa Agagi, alikuwa amepanga dhidi ya Wayahudi. 4Mfalme akamnyoshea Esta fimbo yake ya dhahabu, naye Esta akasimama na kusema, 5“Ukipenda, ewe mfalme, na kama unanijali na ukiona inafaa, tafadhali, toa tangazo la kufutilia mbali mipango ambayo Hamani alikuwa ameamuru itekelezwe. Mipango hiyo ni ile ya mwana wa Hamedatha, mzaliwa wa Agagi, aliyopanga ili kuwaangamiza Wayahudi wote katika mikoa yote. 6Maana, ninawezaje kuvumilia kuona watu wangu wanaangamizwa na jamaa zangu wanauawa?”
7Mfalme Ahasuero akawaambia malkia Esta na Mordekai, yule Myahudi, “Tazameni! Nimempa Esta mali yake Hamani, naye wamekwisha mnyonga kwa sababu ya njama zake dhidi ya Wayahudi. 8Mwaweza kuwaandikia Wayahudi lolote mpendalo. Tena mwaweza kuandika kwa jina langu na kutumia mhuri wa kifalme, kwa sababu tangazo ambalo limetolewa kwa jina la mfalme na kupigwa mhuri wa mfalme, haliwezi kubatilishwa.”
9Basi, mnamo siku ya ishirini na tatu ya mwezi wa tatu uitwao Siwani, Mordekai aliwaita makatibu wote wa mfalme, akawaagiza waandike barua kwa Wayahudi na wakuu, watawala na maofisa wa mikoa yote 127, kuanzia India mpaka Kushi. Nyaraka hizo ziliandikwa kwa kila mkoa katika lugha yake na hati yake ya maandishi, hali kadhalika kwa Wayahudi. 10Mordekai alikuwa ameandika nyaraka hizo kwa jina la mfalme Ahasuero, akazipiga mhuri kwa pete ya mfalme. Na waliozipeleka walikuwa matarishi waliopanda farasi wenye nguvu waendao kasi.
11Kwa njia ya nyaraka hizi mfalme aliwaruhusu Wayahudi katika kila mji kukusanyika ili kuyalinda maisha yao. Walikuwa na ruhusa ya kuharibu, kuua bila huruma na kuangamiza kundi lolote la watu au mkoa, lenye kuwashambulia kwa silaha pamoja na wanawake na watoto wao, na kuziteka nyara mali zao. 12Jambo hili lingefanyika katika mikoa yote ya mfalme Ahasuero, mnamo siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, yaani Adari. 13Nakala za tangazo hili ambalo lilitolewa kama sheria katika kila mkoa zilisambazwa kwa kila mtu katika kila mkoa, ili Wayahudi wajiandae kulipiza kisasi siku hiyo ifikapo. 14Kwa amri ya mfalme, matarishi waliopanda farasi wenye nguvu waendao kasi, waliondoka mbio. Tangazo hili pia lilitolewa katika mji mkuu, Susa.
15Mordekai alipotoka ikulu kwa mfalme, akiwa amevalia mavazi ya kifalme ya rangi ya urujuani na nyeupe, joho la kitani safi la rangi ya zambarau, na taji kubwa ya dhahabu, mji wa Susa ulijaa shangwe na vigelegele. 16Hapo Wayahudi waliona fahari, heshima na furaha, wakajisikia wenye nafuu na ushindi. 17Katika kila mkoa na kila mji, popote pale tangazo hili liliposomwa, Wayahudi walifurahi na kushangilia, wakafanya sherehe na mapumziko; na watu wengine wengi wakajifanya kuwa Wayahudi, maana waliwaogopa sana Wayahudi.



Esta8;1-17

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: