Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday, 6 September 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; Nehemia 11...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana..
Tumshukuru Mungu wetu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Baba wa Upendo,Baba wa faraja,Baba wa huruma,Baba wa Baraka
Mungu mwenye nguvu,Mungu mwenye kuponya
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Muweza wa yote
Wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho,Alfa na Omega...!!


Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Sifa na Utukufu tunakurudishia wewe ee Mungu wetu....!!



Sasa, ndugu, napenda kuwakumbusha ile Habari Njema niliyowahubirieni, nanyi mkaipokea na kusimama imara ndani yake. Kwa njia yake mnaokolewa, ikiwa mnayazingatia maneno niliyowahubirieni, na kama kuamini kwenu hakukuwa bure. Mimi niliwakabidhi nyinyi mambo muhimu sana ambayo mimi niliyapokea: Kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu kufuatana na Maandiko Matakatifu; kwamba alizikwa, akafufuka siku ya tatu kufuatana na Maandiko Matakatifu; kwamba alimtokea Kefa, na baadaye aliwatokea wale kumi na wawili. Kisha aliwatokea ndugu zaidi ya 500 kwa mara moja; wengi wao wanaishi bado, lakini baadhi yao wamekwisha kufa.


Tazama Jana imepita ee Mungu wetu Leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingineJehovah...
Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha

na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti 

yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Baadaye alimtokea Yakobo kisha akawatokea mitume wote. Baada ya wote, akanitokea hata mimi, mimi niliyekuwa kama mtu aliyezaliwa kabla ya wakati. Maana mimi ni mdogo kabisa miongoni mwa mitume, na wala sistahili kuitwa mtume, kwa sababu nililidhulumu kanisa la Mungu. Lakini, kwa neema yake Mungu, nimekuwa kama nilivyo, na neema yake kwangu haikuwa bure. Mimi nimefanya kazi kuliko wote; si mimi hasa, ila ni neema ya Mungu ifanyayo kazi pamoja nami. Lakini hata hivyo, iwe wao ndio wahubirio au mimi nihubiriye, haidhuru, hiki ndicho tunachohubiri, na hiki ndicho mnachoamini.


Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji

Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni
tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe....



Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii

 Mungu wetu ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu

Baba wa Mbinguni tukanene yaliyo yako
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Tukawe barua njema  ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...



Sasa, maadamu inahubiriwa kwamba Kristo amefufuliwa kutoka kwa wafu, baadhi yenu wanawezaje kusema kwamba hakuna ufufuo wa wafu? Kama hakuna ufufuo wa wafu, basi, Kristo naye hakufufuka; na kama Kristo hakufufuka, basi mahubiri yetu hayana maana na imani yenu haina maana. Zaidi ya hayo sisi tungekuwa mashahidi wa uongo mbele ya Mungu, maana tulisema kwamba Mungu alimfufua Kristo kutoka kwa wafu na kumbe yeye hakumfufua – kama ni kweli kwamba wafu hawafufuliwi. Maana, ikiwa ni kweli kwamba wafu hawafufuki, basi naye Kristo hakufufuka. Na kama Kristo hakufufuliwa, basi, imani yenu ni ya bure; mngali bado katika dhambi zenu. Zaidi ya hayo, wale wote waliokufa wakiwa wameungana na Kristo wamepotea kabisa. Kama matumaini yetu katika Kristo yanahusu tu maisha haya ya sasa, basi, sisi ni watu wa kusikitikiwa zaidi kuliko wengine wote duniani.


Mungu Baba tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabuwote wanaopotia magumu/majaribu mbalimbali
watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Yahweh tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Jehovah tunaomba ukawaokoe,ukawavushe salama na  kuwalinda
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimaie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Baba wa Mbinguni ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.


Watu waliokaa Yerusalemu

1Kisha, viongozi wa watu wakakaa mjini Yerusalemu; watu wengine wote, wakapiga kura kati ya kila jamaa kumi ili kuchagua jamaa moja itakayokaa mjini Yerusalemu, mji mtakatifu. Jamaa nyingine tisa zikakaa katika miji yao mingine. 2Watu wakawasifu wale wote waliokubali kukaa mjini Yerusalemu.
3Na katika miji mingine, watu wa Israeli, makuhani, Walawi, walinzi wa malango na wazawa wa watumishi wa Solomoni, walikaa katika maeneo yao wenyewe, katika miji yao.
4Baadhi ya watu wa kabila la Yuda na wa kabila la Benyamini walikaa katika mji wa Yerusalemu. Wafuatao ndio watu wa ukoo wa Yuda waliokaa mjini Yerusalemu: Athaya, mwana wa Uzia, mwana wa Zekaria, mwana wa Amaria, mwana wa Shefatia, mwana wa Mahalaleli. Wote hao ni wazawa wa Peresi. 5Pia Maaseya, mwana wa Baruku, mwana wa Kolhoze, mwana wa Hazaya, mwana wa Adaya, mwana wa Yoyaribu, mwana wa Zekaria, Mshilo. 6Wazawa wote wa Peresi waliokaa mjini Yerusalemu walikuwa wanaume mashujaa 468.
7Watu wa ukoo wa Benyamini waliokaa mjini Yerusalemu ni: Salu, mwana wa Meshulamu, mwana wa Yoedi, mwana wa Pedaya, mwana wa Kolaya, mwana wa Maaseya, mwana wa Ithieli na mwana wa Yeshaya. 8Baada ya huyo walikuwako Gabai na Salai. Jumla yao 928. 9Yoeli, mwana wa Zikri, alikuwa ndiye mkuu wao; naye Yuda mwana wa Hasenua alikuwa mkuu wa pili wa mji.
10Makuhani waliokaa mjini Yerusalemu walikuwa: Yedaya, mwana wa Yoaribu, Yakini, 11Seraya, mwana wa Hilkia, mwana wa Meshulamu, mwana wa Sadoki, mwana wa Merayothi, mwana wa Ahitubu aliyekuwa msimamizi wa nyumba ya Mungu; 12hao pamoja na ndugu zao waliofanya kazi hekaluni; walikuwa watu 822. Pamoja na hao, kulikuwa na Adaya, mwana wa Yerohamu, mwana wa Pelalia, mwana wa Amsi, mwana wa Zekaria, mwana wa Pashuri, mwana wa Malkiya; 13pia kulikuwa ndugu zake waliokuwa wakuu wa jamaa za baba zao; wote pamoja walikuwa watu 242. Pia walikuwako Amaasai, mwana wa Azareli, mwana wa Ahzai, mwana wa Meshilemothi, mwana wa Imeri, 14pamoja na ndugu zao; wote wakiwa 128, watu mashujaa. Na mkuu wao alikuwa Zabdieli mwana wa Hagedolimu.
15Nao Walawi waliokaa mjini Yerusalemu walikuwa: Shemaya, mwana wa Hashubu, mwana wa Azrikamu, mwana wa Hashabia, na mwana wa Buni. 16Shabethai na Yozabadi, wakuu wa ukoo wa Walawi, walikuwa wasimamizi wa kazi za nje ya nyumba ya Mungu, 17na Matania, mwana wa Mika, mwana wa Zabdi, mzawa wa Asafu, aliyekuwa kiongozi wakati wa kuomba sala za shukrani. Bakbukia alikuwa msaidizi wake. Pamoja nao alikuwako Abda, mwana wa Shamua, mwana wa Galali na mzawa wa Yeduthuni. 18Walawi wote waliokaa mjini Yerusalemu, mji mtakatifu, walikuwa 284.
19Wangoja malango waliokaa mjini Yerusalemu walikuwa: Akubu na Talmoni pamoja na ndugu zao waliokuwa wakilinda malango, walikuwa 172. 20Watu wengine wa Israeli, makuhani na Walawi walikaa katika miji ya Yuda, kila mmoja katika urithi wake. 21Lakini watumishi wa hekalu walikaa mjini Yerusalemu katika eneo la Ofeli wakiwa chini ya usimamizi wa Ziha na Gishpa.
22Kiongozi wa Walawi waliokaa mjini Yerusalemu alikuwa, Uzi, mwana wa Bani, mwana wa Hashabia, mwana wa Matania, mwana wa Mika wa ukoo wa Asafu, waliokuwa waimbaji, viongozi waangalizi wa shughuli za nyumba ya Mungu. 23Mfalme alikuwa ametoa amri kuhusu zamu zao na mahitaji yao ya kila siku. 24Pethahia, mwana wa Meshezabeli, wa ukoo wa Zera katika kabila la Yuda, alikuwa mwakilishi kwa mfalme kuhusu mambo yote ya watu wa Yuda.

Watu wa miji mingine

25Watu wengine walikaa katika miji karibu na mashamba yao. Baadhi ya watu wa kabila la Yuda walikaa Kiriath-arba, Diboni na Yekabzeeli pamoja na vijiji vilivyoizunguka. 26Wengine pia walikaa katika miji ya Yeshua, Molada, Beth-peleti, 27Hasar-shuali na Beer-sheba pamoja na vijiji vilivyoizunguka. 28Wengine walikaa katika mji wa Ziklagi, Mekona na vijiji vilivyoizunguka. 29Wengine walikaa katika miji ya Enrimoni, Sora, Yarmuthi, 30Zanoa na Adulamu pamoja na vijiji vilivyoizunguka, Lakishi na mashamba yaliyouzunguka, na katika Azeka pamoja na vijiji vilivyouzunguka. Hii ina maana kwamba watu wa Yuda walikaa katika eneo lililoko kati ya Beer-sheba upande wa kusini na Bonde la Hinomu upande wa kaskazini.
31Watu wa kabila la Benyamini walikaa Geba, Mikmashi, Ai, Betheli na vijiji vinavyoizunguka. 32Wengine walikaa Anathothi, Nobu, Anania, 33Hazori, Rama, Gitaimu, 34Hadidi, Seboimu, Nebalati, 35Lodi na Ono lililokuwa Bonde la Mafundi. 36Baadhi ya Walawi wa Yuda walichanganyikana na watu wa Benyamini.





Nehemia11;1-36

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: