Bwana anakuja
13Ndugu, twataka mjue ukweli kuhusu wale ambao wamekwisha fariki dunia, ili msipatwe na huzuni kama watu wengine wasio na matumaini. 14Sisi tunaamini kwamba Yesu alikufa, akafufuka; na hivyo sisi tunaamini kwamba Mungu atawaleta pamoja na Yesu wale wote waliofariki wakiwa wanamwamini.
15Hili tunalowaambieni ni fundisho la Bwana, kwamba sisi tulio hai, ambao tutakuwa tumebaki wakati Bwana atakapokuja, hakika hatutawatangulia wale waliokwisha fariki dunia. 16Maana patatolewa amri, sauti ya malaika mkuu, sauti ya tarumbeta ya Mungu, naye Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni. Ndipo wale waliokufa wakiwa wanamwamini Kristo watafufuliwa kwanza. 17Kisha sisi tulio hai wakati huo tutakusanywa pamoja nao katika mawingu kumlaki Bwana hewani. Na hivyo tutakuwa daima pamoja na Bwana. 18Basi, farijianeni kwa maneno haya.
Muwe tayari kwa siku ya Bwana
1Ndugu, hakuna haja ya kuwaandikieni juu ya nyakati na majira ya mambo haya yatakapotukia. 2Maana nyinyi wenyewe mwajua kwamba siku ya Bwana itakuja kama mwizi ajavyo usiku. 3Watu watakapokuwa wanasema: “Kila kitu ni shwari na salama”, ndipo uharibifu utakapowaangukia ghafla! Mambo hayo yatatukia ghafla kama uchungu wa uzazi unavyomjia mama anayejifungua, wala watu hawataweza kuepukana nayo. 4Lakini nyinyi, ndugu, hamko gizani, na siku hiyo haipaswi kuwajieni ghafla kama vile mwizi. 5Nyinyi nyote ni watu mnaoishi katika mwanga, watu wa mchana. Sisi si watu wa usiku, wala wa giza. 6Basi, tusilale usingizi kama wengine; tunapaswa kukesha na kuwa na kiasi. 7Wanaolala hulala usiku, na walevi hulewa usiku. 8Lakini sisi ni watu wa mchana na tunapaswa kuwa na kiasi. Tunapaswa kuvaa imani na upendo kama vazi la kujikinga kifuani, na tumaini letu la wokovu kama kofia ya chuma. 9Maana Mungu hakututeua ili tuangamizwe na ghadhabu yake, bali tuupate wokovu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo 10ambaye alikufa kwa ajili yetu, ili tuishi pamoja naye, iwe tu hai au tumekufa. 11Kwa hiyo farijianeni na kusaidiana nyinyi kwa nyinyi, kama mnavyofanya sasa.
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
No comments:
Post a Comment