Jibu la Yobu laendelea
1“Tazama, hayo yote nimeyaona kwa macho yangu;
nimeyasikia kwa masikio yangu mwenyewe na kuelewa.
2Yote mnayoyajua, mimi pia nayajua.
Mimi si mtu duni kuliko nyinyi.
3Lakini ningependa kusema na Mungu mwenye nguvu,
natamani kujitetea mbele zake Mungu.
4Lakini nyinyi mnaupakaa uongo chokaa;
nyinyi nyote ni waganga wasiofaa kitu.
5Laiti mngekaa kimya kabisa,
ikafikiriwa kwamba mna hekima!
6Sikilizeni basi hoja yangu,
nisikilizeni ninapojitetea.
7Je, mnadhani mwamtumikia Mungu kwa kusema uongo?
Mnafikiri kusema kwa hila kunamfaa yeye?
8Je, mnajaribu kumpendelea Mungu?
Je, mtamtetea Mungu mahakamani?
9Je, akiwakagua nyinyi mtapona?
Au mnadhani mnaweza kumdanganya Mungu kama watu?
10Hakika yeye atawakemea
kama mkionesha upendeleo kwa siri.
11Je, fahari yake haiwatishi?
Je, hampatwi na hofu juu yake?
12Misemo yenu ni methali za majivu,
hoja zenu ni ngome za udongo.
13“Nyamazeni, nami niongee.
Yanipate yatakayonipata.
14Niko tayari hata kuhatarisha
maisha yangu;13:14 kadiri ya tafsiri ya kale ya Kigiriki yaani Septuaginta. Kiebrania aya yaanza na “Kwa nini…?” Na msemo “Kushika nyama yangu katikati ya meno yangu” haupatikani penginepo na maana yake si dhahiri – lakini kutokana na aya hiyo maana yake ni sawa na kuhatarisha maisha.
15Mungu aniue akitaka, sina la kupoteza,
hata hivyo nitautetea mwenendo wangu mbele yake.
16Kama nikifaulu hapo nitakuwa nimeshinda,
maana mtu mwovu hawezi kwenda mbele yake.
17Sikilizeni kwa makini maneno yangu,
maelezo yangu na yatue masikioni mwenu.
18Kesi yangu nimeiandaa vilivyo,
nina hakika mimi sina hatia.
19“Nani atakayeipinga hoja yangu?
Niko tayari kunyamaza na kufa.
20Mungu wangu, nijalie tu haya mawili,
nami sitajificha mbali na wewe:
21Kwanza uniondolee mkono wako unaonipiga,
na usiniangamize kwa kitisho chako.
22“Uanze kutoa hoja yako nami nikujibu.
Au mimi nianze, nawe unijibu.
23Makosa na dhambi zangu ni ngapi?
Nijulishe hatia na dhambi yangu.
24“Mbona unaugeuza uso wako mbali nami?
Kwa nini unanitendea kama adui yako?
25Je, utalitisha jani linalopeperushwa,
au kuyakimbiza makapi?
26Wewe umetoa mashtaka makali dhidi yangu,
na kunibebesha dhambi za ujana wangu.
27 Taz Yobu 33:11 Wanifunga minyororo miguuni,
wazichungulia hatua zangu zote,
na nyayo zangu umeziwekea kikomo.
28Nami naishia kama mti uliooza,
mithili ya vazi lililoliwa na nondo.
Yobu13;1-28
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
No comments:
Post a Comment