Hoja ya pili ya Elifazi
(15:1–21:34)
1Kisha Elifazi, Mtemani, akajibu:
2“Je, mtu wa hekima hujibu kwa maneno ya upuuzi?
Je, mtu huyo amejaa maneno matupu?
3Je, mwenye hekima hujitetea kwa maneno yasiyofaa,
au kwa maneno yasiyo na maana?
4Lakini wewe unapuuza uchaji wa Mungu;
na kuzuia kutafakari mbele ya Mungu.
5Uovu wako ndio unaokifundisha kinywa chako,
nawe wachagua kusema kama wadanganyifu.
6Maneno yako mwenyewe yanakuhukumu, sio mimi;
matamshi yako yashuhudia dhidi yako.
7Je, wewe ni mtu wa kwanza kuzaliwa?
Je, wewe ulizaliwa kabla ya kuweko vilima?
8Je, ulipata kuweko katika halmashauri ya Mungu?
au, wewe ndiwe peke yako mwenye hekima?
9Unajua kitu gani tusichokijua sisi?
Unafahamu kitu gani tusichokifahamu sisi?
10Miongoni mwetu wapo wazee wenye hekima,
wenye miaka mingi kuliko baba yako.
11Je, faraja anazokupa Mungu ni ndogo mno?
Au je, neno lake la upole kwako si kitu?
12Mbona moyo unakusukuma kukasirika
na kutoa macho makali,
13hata kumwasi Mungu
na kusema maneno mabaya kama hayo?
14 Taz Yobu 25:4-6 Mtu ni nini hata aweze kuwa mwadilifu?
au yule aliyezaliwa na mwanamke hata aweze kuwa mwema?
15Ikiwa Mungu hawaamini hata watakatifu wake,
nazo mbingu si safi mbele yake,
16sembuse binadamu aliye kinyaa na mpotovu
binadamu atendaye uovu kama kunywa maji!
17“Sasa nisikilize, nami nitakuonesha,
nitakuambia yale niliyoyaona,
18mafundisho ya wenye hekima,
mambo ambayo wazee wao hawakuyaficha,
19ambao Mungu aliwapa hiyo nchi peke yao,
wala hakuna mgeni aliyepita miongoni mwao.
20Mwovu atateseka kwa maumivu siku zote,
miaka yote waliyopangiwa wakatili.
21Sauti za vitisho zitampigia kelele masikioni,
anapodhani amestawi mwangamizi atamvamia.
22Mwovu hana tumaini la kutoka gizani;
mwisho wake ni kufa kwa upanga.
23Hutangatanga kutafuta chakula,
akisema, ‘Kiko wapi?’
Ajua kwamba siku ya giza inamkaribia.
24Taabu na uchungu, vyamtisha;
vyamkabili kama jeshi la mfalme anayeshambulia.
25Kwa sababu amenyosha mkono wake dhidi ya Mungu;
akadiriki kumpinga huyo Mungu mwenye nguvu;
26alikimbia kwa kiburi kumshambulia,
huku ana ngao yenye mafundo makubwa.
27Uso wake ameunenepesha kwa mafuta,
na kiuno chake kimejaa mafuta.
28Ameishi katika miji iliyoachwa tupu,
katika nyumba zisizokaliwa na mtu;
nyumba zilizotakiwa ziwe lundo la uharibifu.
29Mtu huyo kamwe hatakuwa tajiri;
wala utajiri wake hautadumu duniani.
30Hatalikwepa giza la kifo.
Ndimi za moto zitakausha chipukizi zake,
maua yake yatapeperushwa na upepo.
31Heri aache kutumainia upuuzi na kujidanganya,
maana upuuzi ndio utakaokuwa tuzo lake.
32Atalipwa kikamilifu kabla ya kufa kwake,
na wazawa wake hawatadumu.
33Atakuwa kama mzabibu unaopukutisha zabibu mbichi,
kama mzeituni unaoangusha maua yake.
34Wote wasiomcha Mungu hawatapata watoto,
moto utateketeza mahema ya wala rushwa.
35Wanatunga udanganyifu na kuzaa uovu.
Mioyo yao hupanga udanganyifu.”
Yobu15;1-35
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
No comments:
Post a Comment