Jibu la Yobu
1Kisha Yobu akajibu:
2“Mtaendelea kunitesa mpaka lini,
na kunivunjavunja kwa maneno?
3Mara hizi zote kumi mmenishutumu.
Je, hamwoni aibu kunitendea vibaya?
4Hata kama ingekuwa nimekosa kweli,
kosa langu lanihusu mimi mwenyewe.
5Mnaishusha hadhi yangu mpate kujikuza;
mnanilaumu kwa kunyenyekezwa kwangu.
6Jueni kwamba Mungu amenitendea vibaya,
na kuninasa katika wavu wake.
7Tazama napiga yowe: ‘Dhuluma!’
Lakini sijibiwi.
Naita kwa sauti kubwa,
lakini sipati haki yangu.
8Njia yangu ameiziba kwa ukuta ili nisipite
amezitia giza njia zangu.
9Amenivua fahari yangu;
ameiondoa taji yangu kichwani.
10Amenivunja pande zote, nami nimekwisha;
tumaini langu amelingoa kama mti.
11Ameichochea ghadhabu yake dhidi yangu;
ameniona kuwa kama adui yake.
12Majeshi yake yanijia kwa pamoja;
yametengeneza njia ya kuja kwangu,
yamepiga kambi kuizunguka nyumba yangu.
13Mungu amewaweka ndugu zangu mbali nami;
rafiki zangu wakuu wamenitoroka kabisa.
14Jamaa zangu na marafiki hawanisaidii tena.
15Wageni nyumbani mwangu wamenisahau;
watumishi wangu wa kike waniona kuwa mgeni.
Mimi nimekuwa kwao mtu wasiyemjua.
16Namwita mtumishi wangu lakini haitikii,
ninalazimika kumsihi sana kwa maneno.
17Nimekuwa kinyaa kwa mke wangu;
chukizo kwa ndugu zangu mwenyewe.
18Hata watoto wadogo hunidharau,
mara ninapojitokeza wao hunizomea.
19 Taz Sir 6:8 “Rafiki zangu wakuu wanachukizwa nami,
wale niliokuwa nikiwapenda wamenipa kisogo.
20Mwili wangu umebakia tu mifupa na ngozi,
nimeponea chupuchupu baada ya kupoteza yote.
21Nioneeni huruma,
nioneeni huruma enyi rafiki zangu;
maana mkono wa Mungu umenifinya.
22Kwa nini mnanifuatia kama Mungu?
Mbona hamtosheki na mwili wangu?
23“Laiti maneno yangu yangeandikwa!
Laiti yangeandikwa kitabuni!
24Laiti yangechorwa kwa chuma na risasi
juu ya jiwe ili yadumu!
25Najua wazi Mkombozi wangu anaishi,
mwishowe yeye atanipa haki yangu hapahapa duniani.
26Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivyo,
nitamwona Mungu kwa macho yangu mwenyewe.19:26 kwa macho yangu mwenyewe: Au Katika mwili huu.
27Mimi mwenyewe nitakutana naye;
mimi mwenyewe na si mwingine nitamwona kwa macho.
28“Nyinyi mwaweza kujisemea:
‘Tutamfuatia namna gani?
29Tutapataje kwake kisa cha kumshtaki?’
Lakini tahadharini na adhabu.
Chuki yenu yaweza kuwaletea kifo!
Mnapaswa kujua: Mungu peke yake ndiye hakimu.”
Yobu19;1-29
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
No comments:
Post a Comment