1Yobu akaendelea kutoa hoja yake, akasema:
2“Naapa kwa Mungu aliye hai,
aliyeniondolea haki yangu,
Mungu Mwenye Nguvu aliyeifanya nafsi yangu iwe na uchungu!
3Naapa kuwa kadiri ninavyoweza kupumua,
roho ya Mungu ikiwa bado ndani yangu;
4midomo yangu kamwe haitatamka uongo,
wala ulimi wangu kusema udanganyifu.
5Siwezi kabisa kusema kuwa nyinyi mnasema ukweli
mpaka kufa kwangu nasema sina hatia.
6Nashikilia unyofu wangu, wala sitauacha;
katika dhamiri yangu sina cha kunihukumu maishani mwangu.
7“Adui yangu na apate adhabu ya mwovu,
anayeinuka kunilaumu aadhibiwe kama mbaya.
8Asiyemcha Mungu ana tumaini gani,
Mungu anapomkatilia mbali,
anapomwondolea uhai wake?
9Je, atakapokumbwa na taabu,
Mungu atasikia kilio chake?
10Mwovu hawezi kufurahi mbele ya Mungu Mwenye Nguvu;
hataweza kudumu akimwomba Mungu.
11Nitawafundisheni kitendo cha Mungu kilivyo,
sitawaficheni mipango yake Mungu Mwenye Nguvu.
12Lakini nyinyi mnajua jambo hilo vizuri sana!
Mbona, basi mnaongea upuuzi?
13“Hiki ndicho Mungu alichomwekea mtu mwovu,
alichopangiwa mdhalimu kupata ni hiki:
14Watoto wake hata wawe wengi watauawa kwa upanga;
wazawa wake hawatakuwa na chakula cha kutosha.
15Wale watakaopona watakufa kwa maradhi mabaya,
na wajane wao hawatawaombolezea.
16Hata akirundika fedha kama mavumbi,
na mavazi kama udongo wa mfinyanzi,
17na arundike tu, lakini mnyofu ndiye atakayeyavaa,
na fedha yake watagawana watu wasio na hatia.
18Nyumba ajengayo mwovu ni kama utando wa buibui,27:18 kama utando wa buibui makala ya Kiebrania ina: “Kama nondo”.
ni kama kibanda cha mlinzi shambani.
19Huenda kulala tajiri, lakini ni mara ya mwisho;
atafungua macho yake, na utajiri wake umetoweka!
20Vitisho humvamia kama mafuriko;
usiku hukumbwa na kimbunga.
21Upepo wa mashariki humpeperusha akatoweka;
humfagilia mbali kutoka makao yake.
22Upepo huo humvamia bila huruma;
atajaribu kuukimbia lakini mbio za bure.
23Upepo humzomea akimbiapo,
na kumfyonya toka mahali pake.
Yobu27;1-23
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
No comments:
Post a Comment