Mungu anamjibu Yobu
1Hapo Mwenyezi-Mungu alimjibu Yobu kutoka dhoruba:
2“Nani wewe unayevuruga mashauri yangu
kwa maneno yasiyo na akili?
3Jikaze kama mwanamume,
nami nitakuuliza nawe utanijibu.
4“Ulikuwa wapi nilipoiweka misingi ya dunia?
Niambie, kama una maarifa.
5Ni nani aliyeweka vipimo vyake, wajua bila shaka!
Au nani aliyelaza kamba juu yake kuipima?
6Je, nguzo za dunia zimesimikwa juu ya nini,
au nani aliyeliweka jiwe lake la msingi,
7 Taz Bar 3:34 nyota za asubuhi zilipokuwa zikiimba pamoja,
na wana wa Mungu wakapaza sauti za shangwe?
8 Taz Yer 5:22 Ni nani aliyeyafunga mafuriko ya bahari
wakati yalipozuka na kuvuma kutoka vilindini?
9Mimi ndiye niliyeifunika bahari kwa mawingu
na kuiviringishia giza nene.
10Niliiwekea bahari mipaka,
nikaizuia kwa makomeo na milango,
11nikaiambia: ‘Mwisho wako ni hapa, si zaidi!
Mawimbi yako ya nguvu yatakomea hapa!’
12“Yobu, tangu uzaliwe umewahi kuamuru kupambazuke?
na kulifanya pambazuko lijue mahali pake,
13ili lipate kuikamata dunia kwa pembe zake
na kuwatimulia mbali waovu waliomo?
14Dunia hugeuka na kupata rangi kama vazi;
kama udongo wa mfinyanzi unavyogeuzwa na mhuri.
15Lakini waovu watanyimwa mwanga wao,
mkono wanaonyosha kupiga watu utavunjwa.
16“Je, umepata kufika kwenye chemchemi za bahari?
au kutembea juu ya sakafu ya kilindi cha bahari?
17Je, umewahi kuoneshwa malango ya kifo,
au kuyaona malango ya makazi ya giza nene?
18Je, wajua ukubwa wa dunia?
Niambie kama unajua haya yote.
19“Je, makao ya mwanga yako wapi?
Nyumbani kwa giza ni wapi,
20ili upate kulipeleka kwenye makao yake,
na kuifahamu njia ya kwenda huko kwake.
21Wewe unapaswa kujua,
wewe ambaye umekwisha ishi miaka mingi!
22“Je, umewahi kuingia katika bohari za theluji,
au kuona bohari za mvua ya mawe
23ambavyo nimevihifadhi kwa ajili ya wakati wa fujo,
kwa ajili ya siku ya mapigano na vita?
24Ipi njia ya kwenda mahali mwanga unapogawanywa,
au huko kunakotoka upepo wa mashariki ukasambazwa duniani?
25“Nani aliyechora angani njia kwa ajili ya mvua?
Nani aliyeionesha radi njia yake mawinguni,
26ikasababisha mvua kunyesha nchini kusikoishi mtu
na jangwani ambako hakuna mtu,
27ili kuiburudisha nchi kavu na kame
na kuifanya iote nyasi?
28“Je, mvua ina baba?
Au nani ameyazaa matone ya umande?
29Je, barafu ilitoka tumboni kwa nani?
Nani aliyeizaa theluji?
30Maji hugeuka kuwa magumu kama jiwe,
na uso wa bahari ukaganda.
31 Taz Yobu 9:9; Amo 5:8 “Angalia makundi ya nyota:
Je, unaweza kuifunga minyororo Kilimia,
au kuvilegeza vifungo vya Orioni?
32Je, waweza kuziongoza nyota katika majira yake,
au kumwongoza Dubu pamoja na watoto wake?
33Je, wazijua kanuni zinazotawala mbingu;
Je, waweza kuzipangia taratibu zao duniani?
34“Je, waweza kupaza sauti na kuyaamuru mawingu
yakufunike kwa mtiririko wa mvua?
35Je, wewe ukiamuru umeme umulike,
utakujia na kusema: ‘Nipo hapa?’
36Ni nani aliyemjulisha kwarara kujaa kwa mto Nili
au aliyemwambia jogoo kwamba mvua inakuja?38:36 aya hii si dhahiri. Ilifikiriwa zamani kwamba ndege kwarara na jogoo walikuwa wanaweza kujua majira fulani.
37Nani mwenye akili ya kuweza kuhesabu mawingu,
au kuinamisha viriba vya maji huko mbinguni?
38ili vumbi duniani igandamane
na udongo ushikamane na kuwa matope?
39“Je, waweza kumwindia simba mawindo yake
au kuishibisha hamu ya wana simba;
40wanapojificha mapangoni mwao,
au kulala mafichoni wakiotea?
41Ni nani awapaye kunguru chakula chao,
makinda yao yanaponililia mimi Mungu,
na kurukaruka huku na huko kwa njaa?
Yobu38;1-41
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
No comments:
Post a Comment