Utenzi wa ushindi
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi, mtumishi wa Mungu, aliyomwimbia Mungu wakati alipomwokoa mkononi mwa Shauli na adui wengine)
1Nakupenda, ee Mwenyezi-Mungu, nguvu yangu!
2Mwenyezi-Mungu ni mwamba wangu,
ngome yangu na mkombozi wangu;
Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia usalama;
ngao yangu, nguvu za wokovu wangu na ngome yangu.
3Namwita Mwenyezi-Mungu astahiliye sifa anisaidie,
nami naokolewa kutoka kwa maadui zangu.
4Kamba za kifo zilinizingira,
mawimbi ya maangamizi yalinivamia;
5kamba za kuzimu zilinizinga,
mitego ya kifo ilinikabili.
6Katika taabu yangu nilimwita Mwenyezi-Mungu,
nilimlilia Mungu wangu anisaidie.
Aliisikia sauti yangu hekaluni mwake;
kilio changu kilimfikia masikioni mwake.
7Hapo dunia ikatetemeka na kutikisika;
misingi ya milima ikayumbayumba,
kwani Mungu alikuwa amekasirika.
8Moshi ulifuka kutoka puani mwake,
moto uunguzao ukatoka kinywani mwake;
makaa ya moto yalilipuka kutoka kwake.
9Aliinamisha anga, akashuka chini;
na wingu jeusi chini ya miguu yake.
10Alipanda kiumbe chenye mabawa18:10 kiumbe chenye mabawa: Kiebrania: Kerubi. akaruka;
akapaa kasi juu ya mabawa ya upepo.
11Alijifunika giza pande zote,
mawingu mazito yaliyojaa maji yalimzunguka.
12Umeme ulimulika mbele yake;
kukatokea mawinguni mvua ya mawe na makaa ya moto.
13Mwenyezi-Mungu alinguruma kutoka mbinguni;
Mungu Mkuu akatoa sauti yake,
kukatokea mvua ya mawe na makaa ya moto.
14Aliwapiga maadui mishale yake, akawatawanya,
alirusha umeme, akawatimua.
15Ulipowakemea maadui zako ee Mwenyezi-Mungu,
ulipowatisha kwa ghadhabu yako,
vilindi vya bahari vilifunuliwa,
misingi ya dunia ikaonekana.
16Mungu alinyosha mkono kutoka juu akanichukua,
kutoka katika maji mengi alininyanyua.
17Aliniokoa kutoka kwa maadui zangu wenye nguvu nyingi,
aliniokoa kutoka kwa hao walionichukia,
maana walikuwa na nguvu kunishinda.
18Walinivamia nilipokuwa taabuni,
lakini Mwenyezi-Mungu alikuwa kinga yangu.
19Alinileta, akaniweka mahali pa usalama;
alinisalimisha, kwani alipendezwa nami.
20Mwenyezi-Mungu alinipa tuzo kadiri ya uadilifu wangu;
alinituza kwa vile mikono yangu haina hatia.
21Maana nimefuata njia za Mwenyezi-Mungu,
wala sikujitenga na Mungu wangu kwa uovu.
22Nimeshika maagizo yake yote,
sikuacha kufuata masharti yake.
23Mbele yake sikuwa na hatia;
nimejikinga nisiwe na hatia.
24Mwenyezi-Mungu amenituza kadiri ya uadilifu wangu;
yeye ajua kwamba mikono yangu haina hatia.
25Wewe ni mwaminifu kwa walio waaminifu;
mwema kwa wale walio wema.
26Wewe ni mkamilifu kwa walio wakamilifu;
lakini mkatili kwa watu walio waovu.
27Wewe wawaokoa walio wanyenyekevu,
lakini wenye majivuno huwaporomosha.
28Wewe ee Mwenyezi-Mungu, waniangazia;
walifukuza giza langu, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu.
29Kwa msaada wako nakishambulia kikosi;
wewe wanipa nguvu ya kuruka ukuta.
30Huyu Mungu matendo yake hayana dosari!
Ahadi ya Mwenyezi-Mungu ni ya kuaminika;
yeye ni ngao kwa wote wanaomkimbilia usalama.
31Nani aliye Mungu isipokuwa Mwenyezi-Mungu?
Nani aliye mwamba wa usalama ila Mungu wetu?
32Mungu ndiye anijaliaye nguvu kila upande;
ndiye anayeifanya salama njia yangu.
33Ameiimarisha miguu yangu kama ya paa,
na kuniweka salama juu ya vilele.
34Hunifunza kupigana vita,
mikono yangu iweze kuvuta upinde wa shaba.
35Umenipa ngao yako ya kuniokoa;
mkono wako wa kulia umenitegemeza;
wema wako umenifanikisha.
36Umenirahisishia njia yangu;
wala miguu yangu haikuteleza.
37Niliwafuatia adui zangu na kuwakamata;
sikurudi nyuma mpaka nimewaangamiza.
38Niliwaangusha chini wasiweze kuinuka tena;
walianguka chini ya miguu yangu.
39Wewe ulinijalia nguvu ya kupigana vita;
uliwaporomosha maadui chini yangu.
40Uliwafanya maadui zangu wakimbie,
na wale walionichukia niliwaangamiza.
41Walipiga yowe lakini hapakuwa na wa kuwaokoa;
walimlilia Mwenyezi-Mungu lakini hakuwajibu.
42Niliwatwanga wakawa kama vumbi inayopeperushwa na upepo;
niliwakanyaga18:42 niliwakanyaga: Kiebrania: Niliwatupa nje. kama tope la njiani.
43Wewe uliniokoa na mashambulizi ya watu,
ukanifanya mtawala wa mataifa.
Watu nisiowajua walinitumikia.
44Mara waliposikia habari zangu walinitii.
Wageni walinijia wakinyenyekea.
45Wageni walikufa moyo;
wakaja kutoka ngome zao wakitetemeka.
46Mwenyezi-Mungu yu hai!
Asifiwe mwamba wa usalama wangu;
atukuzwe Mungu wa wokovu wangu.
47Yeye ameniwezesha kulipiza kisasi;
na kuyashinda mataifa chini yangu.
48Ameniokoa kutoka kwa maadui zangu,
akanikuza juu ya wapinzani wangu,
na kunisalimisha mbali na watu wakatili.
49 Taz Rom 15:9 Kwa hiyo nitakutukuza kati ya mataifa,
ee Mwenyezi-Mungu nitaliimbia sifa jina lako.
50Mungu humjalia mfalme wake ushindi mkubwa;
humwonesha fadhili zake huyo mteule wake,
naam, humfadhili Daudi na wazawa wake milele.
Zaburi18;1-50
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
No comments:
Post a Comment