Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday, 26 December 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;Zaburi 25...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante

 kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Jehovah  Jireh..!Jehovah Nissi..!Jehovah Raah..!
Jehovah Rapha..!Jehovah Shammah..!Jehovah Shamlom..!
Emanuel-Mungu pamohja nasi..!!
Neema yako yatutosha Baba wa Mbinguni..!

Wakumbushe watu kuwastahi watawala na wenye mamlaka, kuwatii na kuwa tayari kwa kila namna kutenda mambo yote mema. Waambie wasimtukane mtu yeyote; bali waishi kwa amani na masikilizano, wawe daima wapole kwa kila mtu. Maana, wakati mmoja sisi tulikuwa wapumbavu, wakaidi na wapotovu. Tulikuwa watumwa wa tamaa na anasa za kila aina. Tuliishi maisha ya uovu na wivu; watu walituchukia nasi tukachukiana.

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona.....
Lakini wakati wema na upendo wa Mungu, Mwokozi wetu ulipofunuliwa, alituokoa si kwa sababu ya jambo lolote jema tulilotenda sisi, bali kwa sababu ya huruma yake, kwa njia ya Roho Mtakatifu anayetujalia tuzaliwe upya na kuwa na maisha mapya kwa kutuosha kwa maji. Mungu alitumiminia Roho Mtakatifu bila kipimo kwa njia ya Yesu Kristo, Mwokozi wetu, ili kwa neema yake tupate kukubaliwa kuwa waadilifu na kuupokea uhai wa milele tunaotumainia.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu wetu tunaomba ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya Baba wa Mbinguni ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Mungu wetu

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Jambo hili ni kweli. Ninakutaka uyatilie mkazo mambo haya, ili wale wanaomwamini Mungu wawe na hamu ya kuutumia wakati wao katika kutenda mema, yaani mambo mazuri na ya kuwafaa watu. Lakini jiepushe na ubishi wa kipumbavu, ugomvi na mabishano juu ya sheria. Mambo hayo hayana faida yoyote na ni ya bure tu. Mtu anayesababisha mafarakano mpe onyo la kwanza na la pili, kisha achana naye. Wajua kwamba mtu wa namna hiyo amepotoka kabisa, na dhambi zake zathibitisha kwamba amekosea.
Tazama wenye shida/tabu,watoto wako wanaokutafuta kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Yahweh tunaomba  ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu  unajua haja za mioyo ya kila mmoja
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Jehovah ukaonekane katika maisha yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....
Nawapenda.

Kumwomba Mungu uongozi na ulinzi
(Zaburi ya Daudi)
1Ee Mwenyezi-Mungu, kwako naielekeza nafsi yangu!
2Nakutumainia wewe, ee Mungu wangu,
usiniache niaibike;
adui zangu wasifurahie kushindwa kwangu.
3Usimwache anayekutumainia apate aibu;
lakini waaibike wote wanaokuasi kwa makusudi.
4Unijulishe njia zako, ee Mwenyezi-Mungu;
unifundishe nifuate unayotaka.
5Uniongoze katika ukweli wako na kunifundisha,
kwani wewe ni Mungu, mwokozi wangu;
ninakutegemea wewe kila siku.
6Uikumbuke huruma yako ee Mwenyezi-Mungu;
uzikumbuke na fadhili zako kuu,
ambazo zimekuwako tangu kale.
7Usikumbuke dhambi na makosa ya ujana wangu;
unikumbuke kadiri ya fadhili zako,
kwa ajili ya wema wako, ee Mwenyezi-Mungu.
8Mwenyezi-Mungu ni mwema na mnyofu,
kwa hiyo huwafundisha wenye dhambi njia.
9Huwaongoza wanyenyekevu katika uadilifu;
naam, huwafundisha hao njia yake.
10Mwenyezi-Mungu hutenda kwa fadhili na uaminifu,
kwa wale wanaoshika agano lake na maamuzi yake.
11Kwa ajili ya jina lako, ee Mwenyezi-Mungu,
unisamehe kosa langu kwani ni kubwa.
12Kila mtu anayemcha Mwenyezi-Mungu,
Mwenyezi-Mungu atamfunza njia ya kufuata.
13Mtu wa namna hiyo atafanikiwa daima,
na wazawa wake watamiliki nchi.
14Mwenyezi-Mungu ni rafiki ya wale wamchao;
yeye huwajulisha hao agano lake.
15Namwangalia Mwenyezi-Mungu daima;
yeye atainasua miguu yangu mtegoni.
16Unielekee, ee Mungu, unionee huruma,
maana mimi ni mpweke na mnyonge.
17Uniondolee mahangaiko ya moyoni mwangu;
unitoe katika mashaka yangu.
18Uangalie mateso yangu na dhiki yangu;
unisamehe dhambi zangu zote.
19Angalia jinsi walivyo wengi maadui zangu;
ona jinsi wanavyonichukia kwa ukatili.
20Uyalinde maisha yangu, uniokoe;
nakimbilia usalama kwako,
usikubali niaibike.
21Wema na uadilifu vinihifadhi,
maana ninakutumainia wewe.
22Ee Mungu, uwaokoe watu wako, Israeli;
uwaokoe katika taabu zao zote.



Zaburi25;1-22

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: