Sala katika shida kubwa
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi)
1Kwako, ee Mwenyezi-Mungu, nakimbilia usalama,
usiniache niaibike kamwe;
kwa uadilifu wako uniokoe.
2Unitegee sikio, uniokoe haraka!
Uwe kwangu mwamba wa usalama,
ngome imara ya kuniokoa.
3Naam, wewe ni mwamba wangu na ngome yangu;
kwa hisani yako uniongoze na kunielekeza.
4Unitoe katika mtego walionitegea mafichoni;
maana wewe ni kimbilio la usalama wangu.
5 Taz Luka 23:46 Mikononi mwako naiweka roho yangu;
umenikomboa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu mwaminifu.
6Wawachukia wanaoabudu sanamu batili;
lakini mimi nakutumainia wewe, ee Mwenyezi-Mungu.
7Nitashangilia na kufurahia fadhili zako,
maana wewe waiona dhiki yangu,
wajua na taabu ya nafsi yangu.
8Wewe hukuniacha nitiwe mikononi mwa maadui zangu;
umenisimamisha mahali pa usalama.
9Unionee huruma, ee Mwenyezi-Mungu, niko taabuni;
macho yangu yamechoka kwa huzuni,
nimeishiwa nguvu mwilini na rohoni.
10Maisha yangu yamekwisha kwa majonzi;
naam, miaka yangu kwa kulalamika.
Nguvu zangu zimeniishia kwa kutaabika;
hata mifupa yangu imekauka.
11Nimekuwa dharau kwa maadui zangu wote;
kioja kwa majirani zangu.
Rafiki zangu waniona kuwa kitisho;
wanionapo njiani hunikimbia.
12Nimesahaulika kama mtu aliyekufa;
nimekuwa kama chungu kilichovunjikavunjika.
13Nasikia watu wakinongonezana,
vitisho kila upande;
wanakula njama dhidi yangu,
wanafanya mipango ya kuniua.
14Lakini mimi nakutumainia wewe, ee Mwenyezi-Mungu.
Nasema: “Wewe ni Mungu wangu!”
15Maisha yangu yamo mikononi mwako;
uniokoe na maadui zangu,
niokoe na hao wanaonidhulumu.
16Uniangalie kwa wema mimi mtumishi wako;
uniokoe kwa fadhili zako.
17Usiniache niaibike ee Mwenyezi-Mungu,
maana mimi ninakuomba;
lakini waache waovu waaibike,
waache wapotelee kwa mshangao huko kuzimu.
18Izibe midomo ya hao watu waongo,
watu walio na kiburi na majivuno,
ambao huwadharau watu waadilifu.
19Jinsi gani ulivyo mwingi wema wako,
uliowawekea wale wanaokucha!
Wanaokimbilia usalama kwako
wawapa mema binadamu wote wakiona.
20Wawaficha mahali salama hapo ulipo,
mbali na mipango mibaya ya watu;
wawaweka salama katika ulinzi wako,
mbali na ubishi wa maadui zao.
21Asifiwe Mwenyezi-Mungu,
maana amenionesha fadhili zake kwa namna ya ajabu,
nilipozingirwa kama mji unaoshambuliwa.
22Nami niliogopa na kudhani kwamba ulikuwa umenitupa;
kumbe, ulisikia kilio changu nilipokuita unisaidie.
23Mpendeni Mwenyezi-Mungu, enyi watakatifu wake wote.
Mwenyezi-Mungu huwalinda watu waaminifu;
lakini huwaadhibu kabisa wenye kiburi wanavyostahili.
24Muwe hodari na kupiga moyo konde,
enyi nyote mnaomtumainia Mwenyezi-Mungu.
Zaburi31;1-24
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
No comments:
Post a Comment