|
Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tumshukuru Mungu wetu katika yote...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu
Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni Jehovah Jireh..!Jehovah Nissi..!Jehovah Raah..! Jehovah Rapha..!Jehovah Shammah..!Jehovah Shamlom..! Emanuel-Mungu pamohja nasi..!! Neema yako yatutosha Baba wa Mbinguni..!
Baada ya muda mrefu, Mwenyezi-Mungu aliwajalia Waisraeli amani kwa kuwaokoa na maadui zao pande zote. Wakati huo Yoshua alikuwa mzee wa miaka mingi. Yoshua aliwaita Waisraeli wote pamoja na viongozi na wazee wao, waamuzi na maofisa, akawaambia, “Sasa mimi nimekuwa mzee wa miaka mingi. Nyinyi mmeona mambo yote Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu aliyoyatendea mataifa haya yote kwa ajili yenu. Mwenyezi-Mungu Mungu wenu ndiye aliyewapigania.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti, Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona.....
Nchi za mataifa yaliyobaki na yale niliyoyaangamiza nimewagawieni ziwe mali ya makabila yenu, kutoka Yordani mpaka bahari ya Mediteranea, upande wa magharibi. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawaondoa mbele yenu na kuwafukuza kabisa, nanyi mtaimiliki nchi yao kama vile Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alivyowaahidi. Kwa hiyo, muwe imara katika kuzingatia yote yaliyoandikwa katika kitabu cha sheria ya Mose, kamwe msiyaache.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe
Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu, watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu Mungu wetu tunaomba ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya Baba wa Mbinguni ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Mungu wetu Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama inavyokupendeza wewe Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...
Msishirikiane na mataifa haya yaliyobaki kati yenu. Msiitaje miungu yao wala msiape kwa majina ya miungu yao; msiitumikie wala msiisujudie. Bali ambataneni na Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu kama mlivyofanya mpaka leo. Maana Mwenyezi-Mungu ameyafukuza mbele yenu mataifa makubwa na yenye nguvu na hakuna mtu ambaye ameweza kuwapinga nyinyi hadi leo.
Tazama wenye shida/tabu,watoto wako wanaokutafuta kwa bidii na imani Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu Yahweh tunaomba ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake Mungu wetu unajua haja za mioyo ya kila mmoja Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao Jehovah ukaonekane katika maisha yao Nuru yako ikaangaze katika maisha yao Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele Amina....!!!
Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana kwakuwanami/kunisoma Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba ukae nanyi daima.... Nawapenda. |
Sala ya kuomba ulinzi wa Mungu
(Kwa Mwimbishaji. Utenzi wa Wakorahi)
1Ee Mungu, sisi tumesikia kwa masikio yetu,
wazee wetu wametusimulia
mambo uliyotenda nyakati zao,
naam, mambo uliyotenda hapo kale:
2Kwa mkono wako mwenyewe uliyafukuza mataifa mengine,
na mahali pao ukawakalisha watu wako;
uliyaadhibu mataifa mengine,
na kuwafanikisha watu wako.
3Watu wako hawakuitwaa nchi kwa silaha zao,
wala hawakupata ushindi kwa nguvu zao;
ila uliwasalimisha kwa mkono wako mwenyewe,
kwa kuwaangazia uso wako,
kwani wewe uliwapenda.
4Wewe ni mfalme wangu na Mungu wangu!
Wawajalia ushindi wazawa wa Yakobo.
5Kwa nguvu yako twawashinda maadui zetu,
kwa jina lako twawakanyaga wanaotushambulia.
6Mimi siutegemei upinde wangu,
wala upanga wangu hauwezi kuniokoa.
7Wewe ndiwe uliyetuokoa na maadui zetu;
uliwavuruga wale waliotuchukia.
8Daima tutaona fahari juu yako, ee Mungu;
tutakutolea shukrani milele.
9Lakini sasa umetuacha na kutufedhehesha;
huandamani tena na majeshi yetu.
10Umetufanya tuwakimbie maadui zetu,
nao wakaziteka nyara mali zetu.
11Umetufanya kama kondoo wanaopelekwa kuchinjwa;
umetutawanya kati ya mataifa mengine.
12Umewauza watu wako kwa bei ya chini;
wala hukupata faida yoyote.
13Umetufanya kuwa kioja kwa jirani zetu,
nao wanatudhihaki na kutucheka.
14Umetufanya tudharauliwe na watu wa mataifa;
wanatutikisia vichwa vyao kwa kutupuuza.
15Mchana kutwa fedheha yaniandama,
na uso wangu umejaa aibu tele
16kwa maneno na madharau ya wenye kunitukana,
kwa kukabiliwa na maadui zangu na walipiza kisasi.
17Hayo yote yametupata sisi
ijapokuwa hatujakusahau,
wala hatujavunja agano lako.
18Hatujakuasi wewe,
wala hatujaziacha njia zako.
19Hata hivyo umetuacha hoi kati ya wanyama wakali;
umetuacha katika giza kuu.
20Tungalikuwa tumekusahau wewe Mungu wetu,
tukamkimbilia mungu wa uongo,
21ee Mungu, ungalikwisha jua jambo hilo,
kwa maana wewe wazijua siri za moyoni.
22 Taz Rom 8:36 Lakini kwa ajili yako twakikabili kifo kila siku;
tunatendewa kama kondoo wanaopelekwa kuchinjwa.
23Amka, ee Bwana! Mbona umelala?
Inuka! Tafadhali usitutupe milele!
24Mbona wajificha mbali nasi,
na kusahau dhiki na mateso yetu?
25Tumedidimia hata mavumbini,
tumegandamana na ardhi.
26Uinuke, uje kutusaidia!
Utukomboe kwa sababu ya fadhili zako.
Zaburi44;1-26
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
No comments:
Post a Comment