Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday, 6 February 2019

Kikombe Cha Asubuhi ;Zaburi 55...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

“Tiini amri zote ninazowaamuru siku hii ya leo, ili muweze kuingia na kuimiliki nchi mnayoiendea, mpate kuishi kwa muda mrefu katika nchi hiyo inayotiririka maziwa na asali; nchi ambayo Mwenyezi-Mungu aliahidi kuwapa babu zenu na wazawa wao.

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Kwa kuwa nchi mnayokwenda kuimiliki si kama nchi ya Misri mlikotoka, ambako mlipanda nafaka, mkamwagilia maji kwa miguu kama mashamba ya mboga. Lakini nchi mnayokwenda kuimiliki, ni nchi ya milima na mabonde, nchi ambayo hupata maji ya mvua kutoka mbinguni, nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, huitunza; Mwenyezi-Mungu huiangalia daima tangu mwanzo wa mwaka hadi mwisho wa mwaka.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji

Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni
tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe....


Yahweh  tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni

Yahweh ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Baba wa Mbinguni tukanene yaliyo yako
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

“Basi, mkizitii amri zangu ninazowapeni leo, mkampenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mkamtumikia kwa moyo wenu wote na kwa roho yenu yote, yeye ataipatia mvua nchi yenu wakati wake, mvua za masika na mvua za vuli, nanyi mtavuna nafaka yenu, divai yenu na mafuta yenu. Ataotesha majani mashambani kwa ajili ya ng'ombe wenu, nanyi mtakula na kushiba.

Tazama watoto wako wanaokutafuta/kukuomba kwa bidii na imani, Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,
wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe Yahweh tunaomba ukawape neema ya kujiombea
Kufuata njia zako nazo zikawaweke huru
Ukawape macho ya rohoni ee Mungu wetu na masikio ya kusikia
sauti yako,Ukawaokoe na kuwalinda,ukawaponye kimwili na kiroho
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao,Amani ikatawale katika maisha yao,Upendo ukadumu kati yao Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako,kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...

Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,
Mungu Baba aendelee kuwatendea sawasawa na mapezni yake...

Nawapenda.

Sala ya mtu anayedhulumiwa
(Kwa Mwimbishaji: Na ala za nyuzi za muziki. Utenzi wa Daudi)
1Ee Mungu, tega sikio usikie sala yangu;
usiangalie pembeni ninapokuomba.
2Unisikilize na kunijibu;
nimechoshwa na lalamiko langu.
3Nina hofu kwa vitisho vya maadui zangu,
na kwa kudhulumiwa na watu waovu.
Watu waovu wananitaabisha,
kwa hasira wananifanyia uhasama.
4Moyo wangu umejaa hofu,
vitisho vya kifo vimenisonga.
5Natetemeka kwa hofu kubwa,
nimevamiwa na vitisho vikubwa.
6Laiti ningekuwa na mabawa kama njiwa!
Ningeruka mbali na kupata pumziko;
7naam, ningesafiri mbali sana,
na kupata makao jangwani.
8Ningekimbilia mahali pa usalama,
mbali na upepo mkali na dhoruba.
9Ee Bwana, uwaangamize na kuvuruga lugha yao;
maana naona ukatili na ugomvi mjini,
10vikiuzunguka usiku na mchana,
na kuujaza maafa na jinai.
11Uharibifu umeenea pote mjini,
uhasama na udhalimu kila mahali.
12Kama adui yangu angenitukana,
ningeweza kustahimili hayo;
kama mpinzani wangu angenidharau,
ningeweza kujificha mbali naye.
13Kumbe, lakini, ni wewe mwenzangu;
ni wewe rafiki yangu na msiri wangu!
14Sisi tulizoea kuzungumza kirafiki;
pamoja tulikwenda nyumbani kwa Mungu.
15Acha kifo kiwafumanie maadui zangu;
washuke chini Kuzimu wangali hai;
maana uovu umewajaa moyoni mwao.55:15 maana … moyoni mwao: Kiebrania: Nyumba zao na mioyo yao vimejaa uovu.
16Lakini mimi namlilia Mungu,
naye Mwenyezi-Mungu ataniokoa.
17Jioni, asubuhi na adhuhuri, nalalama na kulia,
naye ataisikia sauti yangu.
18Atanikomboa salama katika vita ninayoikabili,
kwa maana maadui zangu ni wengi.
19Mungu atawalaye tangu milele,
atanisikia na kuwaaibisha maadui zangu,
maana hawapendi kujirekebisha,
wala hawamwogopi Mungu.
20Mwenzangu amewashambulia rafiki yake,
amevunja mapatano yake.
21Maneno yake ni laini kuliko siagi,
lakini mawazo yake ni ya kufanya vita.
Maneno yake ni mororo kama mafuta,
lakini yanakata kama upanga mkali.
22Mwachie Mwenyezi-Mungu mzigo wako,
naye atakutegemeza;
kamwe hamwachi mwadilifu ashindwe.
23Wewe, ee Mungu, utawaporomosha shimoni chini kabisa,
watu hao wauaji na wadanganyifu;
hao hawatafikia nusu ya maisha yao.
Lakini mimi nitakutumainia wewe ee Mungu!



Zaburi55;1-23

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: