(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi)
1Mungu ainuka, na maadui zake watawanyika;
wanaomchukia wakimbia mbali naye!
2Kama moshi unavyopeperushwa na upepo,
ndivyo anavyowapeperusha;
kama nta inavyoyeyuka karibu na moto,
ndivyo waovu wanavyoangamia mbele ya Mungu!
3Lakini waadilifu hufurahi ajapo Mungu,
hushangilia na kuimba kwa furaha.
4Mwimbieni Mungu, lisifuni jina lake;
mtengenezeeni njia yake apandaye mawinguni.68:4 apandaye mawinguni: Au apitaye jangwani.
Jina lake ni Mwenyezi-Mungu; furahini mbele yake.
5Mungu akaaye mahali pake patakatifu,
ni Baba wa yatima na mlinzi wa wajane.
6Mungu huwapa fukara makao ya kudumu,
huwafungua wafungwa na kuwapa fanaka.
Lakini waasi wataishi katika nchi kame.
7Ee Mungu, ulipowaongoza watu wako,
uliposafiri kule jangwani,
8dunia ilitetemeka, mbingu zilitiririsha mvua;
kwa kuweko kwako, Mungu wa Sinai,
naam, kwa kuweko kwako, Mungu wa Israeli!
9Ee Mungu, uliinyeshea nchi mvua nyingi,
uliiburudisha nchi yako ilipokuwa imechakaa.
10Watu wako wakapata humo makao;
ukawaruzuku maskini kwa wema wako.
11Bwana alitoa amri,
nao wanawake wengi wakatangaza habari:
12“Wafalme na majeshi yao wanakimbia ovyo!”
Kina mama majumbani waligawana nyara,
13ingawa walibaki mazizini:
Sanamu za njiwa wa madini ya fedha,
na mabawa yao yanangaa kwa dhahabu.
14Mungu Mwenye Nguvu alipowatawanya wafalme huko,
theluji ilianguka juu ya mlima Salmoni.
15Ewe mlima mrefu, mlima wa Bashani,
ewe mlima wa vilele vingi, mlima wa Bashani!
16Mbona unauonea kijicho
mlima aliochagua Mungu akae juu yake?
Mwenyezi-Mungu atakaa huko milele!
17Akiwa na msafara mkubwa,
maelfu na maelfu ya magari ya kukokotwa,
Bwana anakuja patakatifuni pake kutoka Sinai.
18Anapanda juu akichukua mateka;
anapokea zawadi kutoka kwa watu,
hata kutoka kwa watu walioasi;
Mwenyezi-Mungu apate kukaa huko.68:18 Taz Efe 4:8. Mstari wa mwisho wa aya hii si dhahiri katika makala ya Kiebrania.
19Mwenyezi-Mungu asifiwe siku kwa siku!
Yeye hutubebea mizigo yetu;
yeye ndiye Mungu wa wokovu wetu.
20Mungu wetu ni Mungu mwenye kutuokoa;
Bwana Mungu pekee ndiye aokoaye katika kifo.
21Mungu ataviponda vichwa vya maadui zake,
naam, vichwa vya wanaoshikilia njia mbaya.
22Bwana alisema: “Nitawarudisha maadui kutoka Bashani;
nitawarudisha kutoka vilindi vya bahari,
23uoshe miguu katika damu ya maadui zako,
nao mbwa wako wale shibe yao.”
24Ee Mungu, misafara yako ya ushindi yaonekana;
misafara ya Mungu wangu, mfalme wangu, hadi patakatifu pake!
25Mbele waimbaji, nyuma wanamuziki,
katikati wasichana wanavumisha vigoma.
26“Msifuni Mungu katika jumuiya kubwa ya watu.
Msifuni Mwenyezi-Mungu, enyi wazawa wa Israeli!”
27Kwanza ni Benyamini, mdogo wa wote;
kisha viongozi wa Yuda na kundi lao,
halafu wakuu wa Zebuluni na Naftali.
28Onesha, ee Mungu, nguvu yako kuu;
enzi yako uliyotumia kwa ajili yetu,
29kutoka hekaluni mwako, Yerusalemu,
ambapo wafalme watakujia na zawadi zao.
30Uwakemee wale wanyama wakaao bwawani,
kundi la mabeberu na fahali,
mpaka mataifa hayo yakupe heshima na kodi.
Uwatawanye hao watu wenye kupenda vita!68:30 aya ya 30 Kiebrania si dhahiri.
31Mabalozi68:31 Mabalozi: Au Madini ya fedha yataletwa; maana katika Kiebrania si dhahiri. watakuja kutoka Misri,
Waethiopia watamletea Mungu mali zao.68:31 watamletea … zao: Au watamnyoshea Mungu mikono yao.
32Enyi falme za dunia, mwimbieni Mungu,
mwimbieni Bwana nyimbo za sifa;
33mwimbieni yeye apitaye katika mbingu,
mbingu za kale na kale.
Msikilizeni akinguruma kwa kishindo.
34Itambueni nguvu kuu ya Mungu;
yeye atawala juu ya Israeli,
enzi yake yafika katika mbingu.
35Mungu ni wa kutisha patakatifuni pake,
naam, yeye ni Mungu wa Israeli!
Huwapa watu wake nguvu na enzi.
Asifiwe Mungu!
Zaburi68;1-35
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
No comments:
Post a Comment