KITABU CHA TATU
(Zaburi 73–89)
Haki itatawala
(Zaburi ya Asafu)
1Hakika, Mungu ni mwema kwa watu wanyofu;
ni mwema kwa walio safi moyoni.
2Karibu sana ningejikwaa,
kidogo tu ningeteleza;
3maana niliwaonea wivu wenye kiburi,
nilipoona wakosefu wakifanikiwa.
4Maana hao hawapatwi na mateso;
miili yao ina afya na wana nguvu.
5Taabu za binadamu haziwapati hao;
hawapati mateso kama watu wengine.
6Kiburi kimekuwa mkufu wao shingoni,
uhasama ni kama nguo yao.
7Macho yao hufura kwa uovu;
mioyo yao hububujika mipango mibaya.
8Huwadhihaki wengine na kusema mabaya;
hujivuna na kupanga kufanya uhasama.
9Kwa vinywa vyao hutukana mbingu;
kwa ndimi zao hujitapa duniani.
10Hata watu wa Mungu wanawafuata,
hawaoni kwao chochote kibaya73:10 hawaoni … kibaya: Tafsiri yamkini ya Kiebrania kigumu. Wengine: Na kunywa maneno yao kama maji.
na kusadiki kila wanachosema.
11Wanasema: “Mungu hawezi kujua!
Mungu Mkuu hataweza kugundua!”
12Hivi ndivyo watu waovu walivyo;
wana kila kitu na wanapata mali zaidi.
13Je, nimetunza bure usafi moyoni,
na kujilinda nisitende dhambi?
14Mchana kutwa nimepata mapigo,
kila asubuhi nimepata mateso.
15Kama ningalisema hayo kama wao,
ningalikuwa mhaini miongoni mwa watu wako.
16Basi, nilijaribu kufikiria jambo hili,
lakini lilikuwa gumu mno kwangu,
17mpaka nilipoingia patakatifu pako.
Ndipo nikatambua yatakayowapata waovu.
18Kweli wewe wawaweka mahali penye utelezi;
wawafanya waanguke na kuangamia.
19Wanaangamizwa ghafla,
na kufutiliwa mbali kwa vitisho.
20Ee Bwana, uinukapo, wao hutoweka mara,
kama ndoto wakati mtu anapoamka asubuhi.
21Nilipoona uchungu moyoni
na kuchomwa rohoni,
22nilikuwa mpumbavu na mjinga,
nilikuwa kama mnyama mbele yako.
23Hata hivyo niko daima nawe, ee Mungu!
Wanishika mkono na kunitegemeza.
24Wewe waniongoza kwa mashauri yako;
mwishowe utanipokea kwenye utukufu.
25Mbinguni, nani awezaye kunisaidia ila wewe?
Na duniani hamna ninachotamani ila wewe!
26Hata nikikosa nguvu mwilini na rohoni,
wewe, ee Mungu, u mwamba wangu;
riziki yangu kuu ni wewe milele.
27Anayejitenga nawe, hakika ataangamia.
Anayekukana, utamwangamiza.
28Lakini, kwangu ni vema kuwa karibu na Mungu,
wewe Bwana Mwenyezi-Mungu ndiwe usalama wangu.
Nitatangaza mambo yote uliyotenda!
Zaburi73;1-28
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
No comments:
Post a Comment