Wakati wa taabu ya kitaifa
(Utenzi wa Ethani Mwezrahi)
1Ee Mwenyezi-Mungu, nitaimba fadhili zako milele;
nitavitangazia vizazi vyote uaminifu wako.
2Natamka kuwa fadhili zako zadumu milele;
uaminifu wako ni thabiti kama mbingu.
3Umesema: “Nimefanya agano na mteule wangu,
nimemwapia mtumishi wangu Daudi:
4 Taz Zab 132:11; Mate 2:30 ‘Daima nitamweka mzawa wako kuwa mfalme,
tena nitaudumisha ufalme wako milele.’”
5Mbingu na zisifu maajabu yako, ee Mwenyezi-Mungu;
uaminifu wako usifiwe katika kusanyiko la watakatifu.
6Nani mbinguni awezaye kulinganishwa nawe ee Mwenyezi-Mungu?
Nani aliye sawa nawe kati ya viumbe vya mbinguni?
7Wewe waogopwa katika baraza la watakatifu;
wote wanaokuzunguka wanatiwa hofu kuu.
8Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi,
ni nani mwenye nguvu kama wewe, ee Mwenyezi-Mungu?
Uaminifu umekuzunguka pande zote.
9Wewe watawala machafuko ya bahari;
mawimbi yake yakiinuka, wayatuliza.
10Uliliponda joka Rahabu na kuliua;
uliwatawanya adui zako kwa nguvu yako.
11Mbingu ni zako na dunia ni yako pia;
ulimwengu na vitu vyote vilivyomo wewe uliviumba.
12Wewe uliumba kaskazini na kusini;
milima Tabori na Hermoni inakusifu kwa furaha.
13Mkono wako una nguvu,
mkono wako una nguvu na umeshinda!
14Uadilifu na haki ni msingi wa utawala wako;
fadhili na uaminifu vyakutangulia!
15Heri watu wanaojua kukushangilia,
wanaoishi katika mwanga wa wema wako, ee Mwenyezi-Mungu.
16Wanafurahi mchana kutwa kwa sababu yako,
na kukusifu kwa ajili ya uadilifu wako.
17Wewe ndiwe fahari na nguvu yao;
kwa wema wako twapata ushindi.
18Ee Mwenyezi-Mungu, mlinzi wetu ni wako,
mfalme wetu ametoka kwako ewe Mtakatifu wa Israeli.
Ahadi ya Mungu kwa Daudi
19Zamani ulinena katika maono,
ukawaambia watumishi wako waaminifu:
“Nimempa nguvu shujaa mmoja,
nimemkuza huyo niliyemteua kati ya watu.
20 Taz Mate 13:22 Nimempata Daudi, mtumishi wangu;
nimemweka wakfu kwa mafuta yangu matakatifu.
21Mkono wangu wa nguvu utakuwa naye daima;
mkono wangu mimi mwenyewe utamwimarisha.
22Maadui hawataweza kumshinda,
wala waovu hawatamnyanyasa.
23Mimi nitawaponda wapinzani wake;
nitawaangamiza wote wanaomchukia.
24Nitakuwa mwaminifu kwake na kumfadhili,
kwa jina langu atapata ushindi mkubwa.
25Nitaimarisha nguvu na utawala wake,
toka bahari hata mito.
26Yeye ataniita: ‘Wewe ni Baba yangu,
Mungu wangu, mwamba wa wokovu wangu.’
27 Taz Ufu 1:5 Nami nitamfanya kuwa mzaliwa wangu wa kwanza,
mkuu kuliko wafalme wote duniani.
28Fadhili zangu nitamwekea milele,
na agano langu kwake litadumu daima.
29Nitaudumisha daima ukoo wake wa kifalme,
na ufalme wake kama mbingu.
30“Lakini wazawa wake wakiiacha sheria yangu,
wasipoishi kadiri ya maagizo yangu,
31kama wakizivunja kanuni zangu,
na kuacha kutii amri zangu,
32hapo nitawaadhibu makosa yao;
nitawapiga kwa sababu ya uovu wao.
33Lakini sitaacha kumfadhili Daudi,
wala kuwa mwongo kuhusu uaminifu wangu.
34Sitavunja agano langu naye,
wala kubatili neno nililotamka kwa mdomo wangu.
35“Nimeapa mara moja tu kwa utakatifu wangu;
nami sitamwambia Daudi uongo.
36Ukoo wake utadumu milele;
na ufalme wake kama jua.
37Utadumu milele
kama mwezi utokezavyo angani.”
Majonzi ya sasa
38Lakini sasa ee Mungu, umemtupa na kumkataa,
umejaa ghadhabu dhidi ya huyo uliyemweka wakfu.
39Umefuta agano ulilofanya na mtumishi wako;
umeitupa taji yake mavumbini.
40Kuta zote za mji wake umezibomoa;
ngome zake umezivunjavunja.
41Wote wapitao wanampokonya mali zake;
amekuwa dharau kwa jirani zake.
42Maadui zake umewapa ushindi;
umewafurahisha maadui zake wote.
43Silaha zake umezifanya butu;
ukamwacha ashindwe vitani.
44Umemvua madaraka yake ya kifalme89:44 Umemvua … kifalme: Kiebrania: Umemvua usafi wake wa kifalme.
ukauangusha chini utawala wake.
45Umezipunguza siku za ujana wake,
ukamfunika fedheha tele.
Kuomba usalama
46Ee Mwenyezi-Mungu, utajificha hata milele?
Hata lini hasira yako itawaka kama moto?
47Ukumbuke, ee Bwana, ufupi wa maisha yangu;
kwamba binadamu uliyemuumba anaishi muda mfupi!
48Ni mtu gani aishiye asipate kufa?
Nani awezaye kujiepusha na kifo?
49Ee Bwana, ziko wapi basi fadhili zako,
ulizomwapia Daudi kwa uaminifu wako?
50Ee Bwana, ukumbuke anavyotukanwa mtumishi wako,
jinsi nivumiliavyo matusi ya wasiokujua.
51Ona wanavyomzomea, ee Mwenyezi-Mungu;
jinsi wanavyomdhihaki mteule wako kila aendako.
52Asifiwe Mwenyezi-Mungu milele!
Amina! Amina!
Zaburi89;1-52
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
No comments:
Post a Comment