Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday, 9 July 2019

Kikombe Cha Asubuhi ; Methali 14...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

“Mimi siwezi kufanya kitu kwa uwezo wangu mwenyewe. Mimi ninahukumu kama ninavyosikia kutoka kwa Baba, nayo hukumu yangu ni ya haki. Nia yangu si kufanya nipendavyo mwenyewe, bali apendavyo yule aliyenituma.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Nikijishuhudia mimi mwenyewe, ushahidi wangu hauwezi kukubaliwa kuwa wa kweli. Lakini yuko mwingine ambaye hutoa ushahidi juu yangu, nami najua kwamba yote anayosema juu yangu ni ya kweli.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...

Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

Nyinyi mlituma ujumbe kwa Yohane naye aliushuhudia ukweli. Si kwamba mimi nautegemea ushahidi wa wanadamu, lakini nasema mambo haya ili mpate kuokolewa.
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.

1Mwanamke mwenye hekima huijenga nyumba yake,
lakini mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.
2Mwenye mwenendo mnyofu humcha Mwenyezi-Mungu,
lakini mpotovu humdharau Mungu.
3Mpumbavu hujiadhibu mwenyewe kwa kuropoka kwake,
lakini mwenye hekima hulindwa na maneno yake.
4Bila ng'ombe wa kulima ghala za mtu ni tupu,
mavuno mengi hupatikana kwa nguvu ya ng'ombe wa kulima.
5Shahidi mwaminifu hasemi uongo,
lakini asiyeaminika hububujika uongo.
6Mwenye dharau hutafuta hekima bure,
lakini mwenye busara hupata maarifa kwa urahisi.
7Ondoka mahali alipo mpumbavu,
maana hapo alipo hamna maneno ya hekima.
8Hekima ya mwenye busara humwonesha njia yake,
lakini upumbavu wa wapumbavu huwadanganya wenyewe.
9Wapumbavu huchekelea dhambi,
bali wanyofu hupata fadhili kwa Mungu.14:9 aya ya 9 makala ya Kiebrania si dhahiri.
10Moyo waujua uchungu wake wenyewe,
wala mgeni hawezi kushiriki furaha yake.
11Nyumba ya mtu mwovu itabomolewa,
lakini hema ya wanyofu itaimarishwa.
12 Taz Meth 16:25 Njia unayodhani kuwa ni sawa,
mwishoni yaweza kukuongoza kwenye kifo.
13Huzuni yaweza kufichika katika kicheko;
baada ya furaha huja majonzi.
14Mtu mpotovu atavuna matunda ya mwenendo wake,
naye mtu mwema atapata tuzo la matendo yake.
15Mjinga huamini kila kitu anachoambiwa,
lakini mwenye busara huwa na tahadhari.
16Mwenye hekima ni mwangalifu na huepa uovu,
lakini mpumbavu hajizuii wala hana uangalifu.
17Mwenye kuwaka hasira haraka hutenda kipumbavu,
lakini mwenye busara ana uvumilivu.
18Wajinga hurithi upumbavu,
lakini wenye busara hutuzwa taji ya maarifa.
19Waovu watapiga magoti mbele ya watu wema,
watu wabaya mlangoni mwa waadilifu.
20Maskini huchukiwa hata na jirani yake,
lakini tajiri ana marafiki wengi.
21Anayemdharau jirani yake ni mwenye dhambi,
bali ana heri aliye mwema kwa maskini.
22Anayepanga maovu kweli anakosea!
Wanaopanga kutenda mema hufadhiliwa.
23Bidii katika kila kazi huleta faida,
lakini maneno matupu huleta umaskini.
24Mali ni taji ya fahari ya wenye hekima,
lakini ujinga ni shada la wapumbavu.
25Shahidi wa kweli huokoa maisha,
lakini msema uongo ni msaliti.
26Amchaye Mwenyezi-Mungu ana tumaini imara,
na watoto wake watapata kimbilio salama.
27Kumcha Mwenyezi-Mungu ni chemchemi ya uhai;
humwezesha mtu kuepa mitego ya kifo.
28Fahari ya mfalme ni wingi wa watu wake,
lakini bila watu mtawala huangamia.
29Mtu asiye mwepesi wa hasira ana busara kubwa,
lakini akasirikaye upesi hukuza upumbavu.
30Amani rohoni humpa mtu afya,
lakini tamaa huozesha mifupa.
31Anayemdhulumu maskini anamtukana Muumba wake,
lakini amwoneaye huruma mhitaji anamtukuza Mungu.
32Mwovu huangamizwa kwa matendo yake maovu,
lakini mwadilifu hupata usalama kwa unyofu wake.14:32 kwa unyofu wake: Kiebrania; katika kifo chake.
33Hekima imo moyoni mwa mtu mwenye busara;
haipatikani kamwe mioyoni mwa wapumbavu.
34Uadilifu hukuza taifa,
lakini dhambi ni balaa kwa taifa lolote.
35Mfalme humfadhili mtumishi atendaye kwa hekima,
lakini hasira yake huwakumba watendao yasiyofaa.

Methali14;1-35

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: