Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday, 25 July 2019

Kikombe Cha Asubuhi ; Methali 26...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

Lakini kama sadaka hiyo ya amani ni ya nadhiri au ya hiari, italiwa siku hiyohiyo inapotolewa na sehemu nyingine yaweza kuliwa kesho yake. Lakini nyama yoyote ya sadaka hiyo inayobaki hadi siku ya tatu itateketezwa.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Tena nyama yoyote ya sadaka ya amani ikiliwa siku ya tatu, haitakubaliwa, wala haitapokelewa kwa faida yake mtu aliyeitoa. Nyama hiyo ni chukizo na mtu atakayeila atawajibika kwa uovu wake.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...

Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

“Nyama yoyote inayogusa kitu najisi isiliwe. Nyama hiyo itateketezwa kwa moto. Wote walio safi wanaweza kula nyama iliyotolewa sadaka ya amani kwa Mwenyezi-Mungu. Lakini mtu yeyote aliye najisi, akila nyama hiyo, atatengwa na watu wake.
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.

1Heshima apewayo mpumbavu haimfai;
ni kama theluji ya kiangazi,
au mvua ya wakati wa mavuno.
2Kama shomoro au mbayuwayu wasiotua,
kadhalika laana asiyostahili mtu haimtui.
3Mjeledi kwa farasi, lijamu kwa punda,
na fimbo kwa mgongo wa mpumbavu.
4Usimjibu mpumbavu kipumbavu,
usije ukafanana naye.
5Mjibu mpumbavu kama ustahilivyo upumbavu wake,
asije akajiona kuwa mwenye hekima zaidi.
6Kumtuma mpumbavu ujumbe,
ni kama kujikata miguu au kujitafutia shida.
7Methali mdomoni mwa mpumbavu,
ni kama miguu ya kiwete inayoninginia.
8Kumpa mpumbavu heshima,
ni kama kufunga jiwe kwenye kombeo.
9Mpumbavu anayejaribu kutumia methali,
ni kama mlevi anayejaribu kungoa mwiba mkononi.
10Mtu amwajiriye mpumbavu au mlevi,
ni kama mpiga upinde anayejeruhi kila mtu.26:10 aya ya 10 makala ya Kiebrania si dhahiri.
11Mpumbavu anayerudiarudia upumbavu wake,
ni kama mbwa anayekula matapishi yake.
12Wamwona mtu ajionaye kuwa mwenye hekima?
Nakuambia mpumbavu ni nafuu kuliko huyo.
13Mvivu husema: “Huko nje kuna simba;
siwezi kwenda huko.”
14Kama vile mlango uzungukiapo bawaba zake,
ndivyo mvivu juu ya kitanda chake.
15Mvivu huutia mkono wake katika sahani ya chakula,
lakini hawezi kuuinua hadi mdomoni.
16Mvivu hujiona kuwa mwenye hekima
kuliko watu saba wawezao kujibu kwa busara.
17Ajiingizaye katika ugomvi usiomhusu,
ni kama mtu amshikaye masikio mbwa anayepita.
18Kama mwendawazimu achezeavyo mienge,
au mishale ya kifo,
19ndivyo alivyo mtu ampotoshaye jirani,
kisha aseme, “Nilikuwa natania tu!”
20Bila kuni, moto huzimika;
bila mchochezi, ugomvi humalizika.
21Kama vile makaa au kuni huchochea moto,
ndivyo mgomvi achocheavyo ugomvi.
22Maneno ya msengenyaji ni kama kitoweo;
hushuka mpaka ndani kabisa tumboni.
23Kama rangi angavu iliyopakwa kigae,
ndivyo yalivyo maneno matamu yenye nia mbaya.
24Mwenye chuki huficha chuki yake kwa maneno mazuri,
lakini huwa ana hila moyoni mwake.
25Akiongea vizuri usimwamini,
moyoni mwake mna chuki chungu nzima.
26Huenda akaficha chuki yake,
lakini nia zake mbaya zitajulikana kwa wote.
27Amchimbiaye mwenzake shimo, hutumbukia mwenyewe;
abingirishaye jiwe litamrudia mwenyewe.
28Asemaye uongo huwachukia hao anaowaumiza,
naye abembelezaye huleta maangamizi.

Methali26;1-28

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: