Kurudi kutoka uhamishoni
1Mwenyezi-Mungu atawahurumia tena watu wa Yakobo, atawateua tena Waisraeli. Atawarudisha katika nchi yao wenyewe, na wageni watakuja na kukaa pamoja na watu wa Yakobo. 2Watu wa mataifa watawasaidia Waisraeli kurudi katika nchi waliyopewa na Mwenyezi-Mungu. Na hapo watawatumikia Waisraeli kama watumwa. Wale waliowateka sasa watatekwa na Waisraeli, na watawatawala wale waliowadhulumu.
Mfalme wa Babuloni miongoni mwa wafu
3Ewe Israeli, wakati Mwenyezi-Mungu atakapokufariji baada ya mateso, misukosuko na utumwa uliofanyiwa, 4utaimba utenzi huu wa kumdhihaki mfalme wa Babuloni:
“Jinsi gani mdhalimu alivyokomeshwa!
Ujeuri wake umekomeshwa!
5Mwenyezi-Mungu amelivunja gongo la waovu,
ameivunja fimbo ya kifalme ya watawala,
6ambao walipiga nayo watu kwa hasira bila kukoma,
na kuwatawala kwa udhalimu bila huruma.
7Sasa dunia yote ina utulivu na amani,
kila mtu anaimba kwa furaha.
8Misonobari inafurahia kuanguka kwako,
nayo mierezi ya Lebanoni pamoja yasema:
‘Kwa vile sasa umeangushwa,
hakuna mkata miti atakayekuja dhidi yetu!’
9“Kuzimu nako kumechangamka,
ili kukulaki wakati utakapokuja.
Kunaiamsha mizimu ije kukusalimu
na wote waliokuwa wakuu wa dunia;
huwaamsha kutoka viti vyao vya enzi
wote waliokuwa wafalme wa mataifa.
10Wote kwa pamoja watakuambia:
‘Nawe pia umedhoofika kama sisi!
Umekuwa kama sisi wenyewe!
11Fahari yako imeteremshwa kuzimu
pamoja na muziki wa vinubi vyako.
Chini mabuu ndio kitanda chako,
na wadudu ndio blanketi lako!’
12 “Jinsi gani ulivyoporomoshwa toka mbinguni,
wewe uliyekuwa nyota angavu ya alfajiri.
Jinsi gani ulivyoangushwa chini,
wewe uliyeyashinda mataifa!
13Wewe ulijisemea moyoni mwako:
‘Nitapanda mpaka mbinguni;
nitaweka kiti changu juu ya nyota za Mungu,
nitaketi juu ya mlima wakutanapo miungu,
huko mbali pande za kaskazini.
14Nitapanda vilele vya mawingu
nitajifanya kuwa sawa na Mungu Mkuu.’
15Lakini umeporomoshwa hadi kuzimu;
umeshushwa chini kabisa shimoni.
16“Watakaokuona watakukodolea macho,
watakushangaa wakisema:
‘Je, huyu ndiye aliyetetemesha dunia
na kuzitikisa falme,
17aliyegeuza dunia kuwa kama jangwa,
akaangamiza miji yake,
na kuwanyima wafungwa wake kurudi kwao?’
18Wafalme wote wa mataifa wamezikwa kwa heshima
kila mmoja ndani ya kaburi lake.
19Lakini wewe umetupwa nje ya kaburi lako;
kama mtoto wa kuchukiza aliyezaliwa mfu
maiti yako imekanyagwakanyagwa,
umerundikiwa maiti za waliouawa kwa upanga,
waliotupwa mashimoni penye mawe.
20Lakini wewe hutaunganishwa nao katika mazishi,
maana uliiharibu nchi yako,
wewe uliwaua watu wako.
Wazawa wa waovu na wasahaulike kabisa!
21Kaeni tayari kuwachinja watoto wake
kwa sababu ya makosa ya baba zao,
wasije wakaamka na kuimiliki nchi,
na kuijaza dunia yote miji yao.”
Mungu ataangamiza Babuloni
22Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Nitaushambulia mji wa Babuloni na kuuangamiza kabisa. Nitaharibu kila kitu, mji wote, watoto na yeyote aliyebaki hai. Mimi Mwenyezi-Mungu nimenena. 23Nitaufanya kuwa makao ya nungunungu, na utakuwa madimbwi ya maji. Nami nitaufagilia mbali kwa ufagio wa maangamizi. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimenena.”
Mwisho wa udhalimu wote
24Mwenyezi-Mungu wa majeshi ameapa:
“Kama nilivyopanga,
ndivyo itakavyokuwa;
kama nilivyokusudia,
ndivyo itakavyokamilika.
25Nitauvunja uwezo wa Waashuru nchini mwangu;
nitawakanyagakanyaga katika milima yangu.
Nitawaondolea watu wangu nira ya dhuluma yao,
na mzigo wa mateso yao.”
26Huu ndio uamuzi wake Mwenyezi-Mungu
kuhusu dunia yote;
hii ndiyo adhabu atakayotoa
juu ya mataifa yote.
27Kama Mwenyezi-Mungu wa majeshi ameamua,
nani atakayeweza kubatilisha uamuzi wake?
Kama amepania kutoa adhabu,
ni nani atakayempinga?
Mungu atawaangamiza Wafilisti
28Mwaka alipofariki mfalme Ahazi, Mungu alitoa kauli hii:
29“Msishangilie enyi Wafilisti wote,
kwamba Ashuru, fimbo iliyowapiga, imevunjika;
maana, nyoka wa kawaida atazaa nyoka mwenye sumu,
na nyoka mwenye sumu atazaa joka lirukalo.
30Wazaliwa wa kwanza wa maskini watashiba,
na fukara watakaa kwa usalama.
Lakini chipukizi wenu nitawaua kwa njaa;
na yeyote wenu atakayebaki nitamuua.
31Piga yowe ewe lango; lia ewe mji;
yeyuka kwa hofu ewe nchi yote ya Filistia.
Maana moshi wa askari waja kutoka kaskazini,
wala hakuna atakayechelewa katika majeshi yake.”
32Basi watapewa jibu gani wajumbe wa taifa hilo?
Wataambiwa: Mwenyezi-Mungu ameijenga imara Siyoni,
na maskini wa watu wake watakimbilia usalama huko.
Isaya14;1-32
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
No comments:
Post a Comment