Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday, 3 September 2019

Kikombe Cha Asubuhi;Isaya 3....

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

Basi, walikwenda kwa mfalme na kumshtaki Danieli kwa kutumia ile sheria, wakisema, “Mfalme Dario, je, hukutia sahihi hati ya sheria kuwa kwa muda wa siku thelathini hakuna mtu yeyote atakayeruhusiwa kuomba kitu chochote, kwa mungu yeyote, au kwa mtu yeyote isipokuwa kutoka kwako wewe, ee mfalme, na kwamba yeyote atakayevunja sheria hii atatumbukizwa katika pango la simba?” Mfalme akaitikia, “Hivyo ndivyo ilivyo, kulingana na sheria ya Wamedi na Wapersi ambayo haiwezi kubatilishwa.”
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Wakamwambia mfalme, “Yule Danieli aliye mmoja wa mateka kutoka nchi ya Yuda hakuheshimu wewe mfalme wala haitii amri uliyotia sahihi. Yeye anasali mara tatu kila siku.” Mfalme aliposikia maneno hayo, alisikitika sana. Akajitahidi sana kupata njia ya kumwokoa Danieli. Aliendelea kujaribu mpaka jua likatua.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...

Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

Wale watu wakamwendea mfalme Dario kwa pamoja na kumwambia, “Ee mfalme, ujue kuwa hakuna sheria wala amri yoyote ya Wamedi na Wapersi inayoweza kubatilishwa baada ya kuwekwa na mfalme.”
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.

Msukosuko Yerusalemu
1Sasa, Bwana Mwenyezi-Mungu wa majeshi
ataondoa kutoka Yerusalemu na Yuda kila tegemeo:
Tegemeo lote la chakula,
na tegemeo lote la kinywaji.
2Ataondoa mashujaa na askari,
waamuzi na manabii,
waaguzi na wazee,
3majemadari wa vikosi vya watu hamsini,
na watu wenye vyeo,
washauri, wachawi stadi na walozi hodari.
4Mungu ataweka watoto wawatawale;
naam, watoto wachanga watawatawala.
5Watu watadhulumiana,
kila mtu na jirani yake;
vijana watawadharau wazee wao,
na watu duni watapuuza wakuu wao.
6Wakati huo ndugu atamwambia ndugu yake
wakiwa bado nyumbani kwa baba yao:
“Wewe unalo koti;
utakuwa kiongozi wetu.
Chukua hatamu juu ya uharibifu huu!”
7Lakini siku hiyo atasema,
“Mimi siwezi kuwa mwuguzi,
nyumbani mwangu hamna chakula wala mavazi.
Msinifanye mimi kuwa kiongozi wenu.”
8Watu wa Yerusalemu wamejikwaa,
watu wa Yuda wameanguka,
kwa kuwa wanampinga Mwenyezi-Mungu
kwa maneno na matendo,
wakipuuza utukufu wake miongoni mwao.
9Ubaguzi wao unashuhudia dhidi yao;
wanatangaza dhambi yao kama ya Sodoma,
wala hawaifichi.
Ole wao watu hao,
kwani wamejiletea maangamizi wenyewe.
10Waambieni waadilifu jinsi walivyo na bahati:
Kwani watakula matunda ya matendo yao.
11Lakini ole wao watu waovu!
Mambo yatawaendea vibaya,
kwani waliyotenda yatawapata wao wenyewe.
12Watu wangu watadhulumiwa na watoto;
wanawake ndio watakaowatawala.
Enyi watu wangu, viongozi wenu wanawapotosha,
wanavuruga njia mnayopaswa kufuata.

Mwenyezi-Mungu awahukumu watu wake
13Mwenyezi-Mungu yu tayari kuanza mashtaka,
anasimama kuwahukumu watu wake.
14Mwenyezi-Mungu anawashtaki
wazee na wakuu wa watu wake:
“Nyinyi ndio mlioliharibu shamba la mizabibu;
mali walizowanyanganywa maskini zimo nyumbani kwenu.
15Mnamaanisha nini kuwakandamiza watu wangu,
kuwatendea ukatili watu maskini?
Nauliza mimi Bwana, Mwenyezi-Mungu wa majeshi.”

Onyo kwa wanawake wa Yerusalemu
16Mwenyezi-Mungu asema:
“Wanawake wa Siyoni wana kiburi;
wanatembea wameinua shingo juu,
wakipepesa macho yao kwa tamaa.
Hatua zao ni za maringo,
na miguuni njuga zinalia.
17Basi, mimi Mwenyezi-Mungu nitawaadhibu;
nitawanyoa nywele hao wanawake wa Siyoni,
na kuwavua nguo za kufunika uchi wao.”
18Siku yaja ambapo Mwenyezi-Mungu atawanyanganya wanawake wa Yerusalemu vitu vyote wanavyoringia: Njuga, kaya, mikufu, 19vipuli, vikuku, shungi, 20vitambaa vya kichwani, bangili, vibwebwe, vibweta vya marashi, hirizi, 21pete, hazama, 22mavazi ya sikukuu, mitandio, majoho, mikoba, 23mavazi yaoneshayo, mavazi ya kitani, vilemba na shela.
24Badala ya kunukia marashi watatoa uvundo;
badala ya mishipi mizuri watatumia kamba;
badala ya nywele nzuri watakuwa na upara;
badala ya mavazi mazuri watavaa matambara;
uzuri wao wote utageuka kuwa aibu.
25Wanaume wenu wataangamia kwa upanga,
watu wenu wenye nguvu watakufa vitani.
26Malango ya mji yatalia na kuomboleza;
nao mji utakuwa kama mwanamke aliyepokonywa kila kitu, ameketi mavumbini.

Isaya3;1-26

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: