Mfalme mwadilifu
1Kutatokea mfalme atakayetawala kwa uadilifu,
nao viongozi wataongoza kwa kufuata haki.
2Kila mmoja atakuwa kama mahali pa kujikinga na upepo,
kama mahali pa kujificha wakati wa tufani.
Watakuwa kama vijito vya maji katika nchi kame,
kama kivuli cha mwamba mkubwa jangwani.
3Macho hayatafumbwa tena,
masikio yatabaki wazi.
4Wafanyao mambo kwa hamaki wataamua kwa busara,
wenye kigugumizi wataongea sawasawa.
5Wapumbavu hawataitwa tena waungwana,
wala walaghai hawataitwa tena waheshimiwa.
6Wapumbavu hunena upumbavu,
na fikira zao hupanga kutenda uovu,
kutenda mambo yasiyo mema,
kusema mambo ya kumkufuru Mwenyezi-Mungu.
Huwaacha wenye njaa bila chakula,
na wenye kiu huwanyima kinywaji.
7Ulaghai wa walaghai ni mbaya;
hao huzua visa viovu,
na kumwangamiza maskini kwa maneno ya uongo,
hata kama madai ya maskini ni halali.
8Lakini waungwana hutenda kiungwana,
nao hutetea mambo ya kiungwana.
Mawaidha kwa wanawake wa Yerusalemu
9Inukeni, enyi wanawake mnaostarehe, mnisikilize;
sikilizeni ninayosema enyi mabinti mlioridhika.
10Katika mwaka mmoja hivi mtatetemeka nyinyi mliotosheka;
maana hamtapata mavuno yoyote,
na mavuno ya zabibu yatatoweka.
11Tetemekeni kwa woga, enyi mnaojikalia tu;
tetemekeni kwa hofu, enyi mnaostarehe!
Vueni nguo zenu, mbaki uchi,
mjifunge vazi la gunia viunoni mwenu.
12Jipigeni vifua kwa huzuni,
ombolezeni, kwa sababu ya bustani zilizokuwa nzuri,
kwa mizabibu iliyokuwa ikizaa sana,
13kwa ardhi ya watu wangu inayoota miiba na mbigili,
kwa nyumba zote zilizojaa watu wenye furaha,
kwa mji uliokuwa na shangwe.
14Maana ikulu ya mfalme itaachwa mahame,
mji huo wa watu wengi utahamwa.
Mlima na mnara wa ulinzi utakuwa mapango milele,
pundamwitu watapitapita huko kwa furaha,
kondoo watapata malisho yao humo.
Nyakati za amani
15Hali itaendelea kuwa hivyo
mpaka tumiminiwe roho ya Mungu kutoka juu.
Hapo jangwa litakuwa shamba la rutuba tena,
na mashamba ya rutuba yatakuwa msitu.
16Haki itadumu katika nchi iliyokuwa nyika,
uadilifu utatawala katika mashamba yenye rutuba.
17Kutokana na uadilifu watu watapata amani,
utulivu na usalama utadumu milele.
18Watu wangu watakaa katika makao ya amani,
katika maskani salama na mazingira matulivu.
19Msitu wa adui utatoweka kabisa,32:19 Msitu … utatoweka kabisa: Au Patanyesha mvua ya mawe msitu utakapoanguka.
na mji wake utaangamizwa.
20Lakini heri yenu nyinyi:
Mtapanda mbegu zenu popote penye maji,
ng'ombe na punda wenu watatembeatembea watakavyo.
Isaya32;1-20
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
No comments:
Post a Comment