Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday, 22 October 2019

Kikombe Cha Asubuhi;Isaya 38....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

Wakati Apolo alipokuwa Korintho, Paulo alisafiri sehemu za bara, akafika Efeso ambako aliwakuta wanafunzi kadhaa. Akauliza, “Je, mlipopata kuwa waumini mlipokea Roho Mtakatifu?” Nao wakamjibu, “La! Hata hatujasikia kwamba kuna Roho Mtakatifu.” Naye akasema, “Sasa mlipata ubatizo wa namna gani?” Wakamjibu, “Ubatizo wa Yohane.” Naye Paulo akasema, “Ubatizo wa Yohane ulikuwa wa kuonesha kwamba watu wametubu. Yohane aliwaambia watu wamwamini yule ambaye alikuwa anakuja baada yake, yaani Yesu.”
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Baada ya kusikia hayo, walibatizwa kwa jina la Bwana Yesu. Basi, Paulo akawawekea mikono, na Roho Mtakatifu akawashukia, wakaanza kusema lugha ngeni na kutangaza ujumbe wa Mungu. Wote jumla walikuwa watu wapatao kumi na wawili.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

Kwa muda wa miezi mitatu Paulo alikuwa akienda katika sunagogi, akawa na majadiliano ya kuvutia sana juu ya ufalme wa Mungu. Lakini wengine walikuwa wakaidi, wakakataa kuamini, wakaanza kuongea vibaya juu ya hiyo njia ya Bwana katika kusanyiko la watu. Hapo Paulo alivunja uhusiano nao, akawachukua pembeni wale wanafunzi wake, akawa anazungumza nao kila siku katika jumba la masomo la Turano. Aliendelea kufanya hivyo kwa muda wa miaka miwili hata wakazi wote wa Asia, Wayahudi na watu wa mataifa mengine, wakaweza kusikia neno la Bwana.
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.

Mfalme Hezekia anaugua
(2Fal 20:1-11; 2Nya 32:24-26)
1Wakati huo, mfalme Hezekia aliugua sana karibu kufa. Ndipo nabii Isaya mwana wa Amozi, akamwendea, akamwambia, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu: Panga mambo yako sawasawa katika nyumba yako kwa kuwa utakufa, hutapona.”
2Hezekia akageukia upande wa ukuta na kumwomba Mwenyezi-Mungu, 3akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, nakusihi ukumbuke jinsi nilivyokutumikia kwa uaminifu na kwa moyo wangu wote, na kutenda yaliyo sawa mbele yako.” Hezekia akalia kwa uchungu sana.
4Kisha neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Isaya: 5“Nenda ukamwambie Hezekia, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa baba yako Daudi, anasema hivi: Nimesikia ombi lako na nimeyaona machozi yako. Basi, nakuongezea miaka kumi na mitano ya kuishi. 6Nitakuokoa wewe pamoja na mji huu mikononi mwa mfalme wa Ashuru na kuulinda.”
21Basi, Isaya akasema, “Chukueni andazi la tini mkaliweke kwenye jipu lake, apate kupona.”38:21-22 aya ya 21-22 zimehamishiwa hapa kuleta maana yake kamili katika simulizi hilo. 22Hezekia akauliza, “Ni ishara gani itakayonijulisha kwamba mimi nitakwenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu?” 7Isaya akamjibu, “Hii itakuwa ishara kwako kutoka kwa Mwenyezi-Mungu kwamba Mwenyezi-Mungu atafanya kama alivyoahidi. 8Nitafanya kivuli kwenye ngazi iliyojengwa na Ahazi, kirudi nyuma hatua kumi.” Nacho kivuli kikarudi nyuma hatua kumi.38:8 ngazi … hatua kumi … hatua kumi: Au Kwenye saa ya jua … hatua kumi … hatua kumi.
9Kisha mfalme Hezekia alipopona, akatunga wimbo huu wa shukrani:
10“Nilisema: Nikiwa mbichi kabisa,
inanibidi niage dunia.
Mimi nimepangiwa kwenda kuzimu
siku zote zilizonibakia.
11Nilisema sitamwona tena Mwenyezi-Mungu,
katika nchi ya walio hai;
wala sitamwona mtu yeyote tena,
miongoni mwa wakazi wa ulimwengu.
12Makao yangu yamengolewa kwangu,
kama hema la mchungaji;
kama, mfumanguo nimefungasha maisha yangu;
Mungu amenikatilia mbali;
kabla hata mwisho wa siku amenikomesha.38:12 maana ya aya hii katika Kiebrania si dhahiri.
13Usiku kucha nililia kuomba msaada;
kama simba, anavunjavunja mifupa yangu;
mchana na usiku ananikomesha.38:13 maana ya aya hii katika Kiebrania si dhahiri.
14“Ninalia kama mbayuwayu,
nasononeka kama njiwa.
Macho yangu yamefifia kwa kuangalia juu.
Ee Bwana, nateseka;
uwe wewe usalama wangu!
15Lakini niseme nini:
Yeye mwenyewe aliniambia,
naye mwenyewe ametenda hayo.
Usingizi wangu wote umenitoroka
kwa sababu ya uchungu moyoni mwangu.
16“Ee Bwana, Sisi twaishi kutokana na yote uliyotenda,
kwa hayo yote mimi binafsi pia ninaishi.38:16 aya hii maana ya Kiebrania si dhahiri.
Nirudishie afya, uniwezeshe kuishi.
17Nilipata mateso makali kwa faida yangu;
lakini umeyaokoa maisha yangu
kutoka shimo la uharibifu,
maana umezitupa dhambi zangu nyuma yako.
18Huko kuzimu mtu hawezi kukushukuru wewe;
waliokufa hawawezi kukushukuru wewe.
Wala washukao huko shimoni
hawawezi tena kutumainia uaminifu wako.
19Walio hai ndio wanaokushukuru,
kama na mimi ninavyofanya leo.
Kina baba huwajulisha watoto wao uaminifu wako.
20“Mwenyezi-Mungu ataniokoa.
Nasi tutamsifu kwa nyimbo za vinubi
siku zote za maisha yetu,
nyumbani kwake Mwenyezi-Mungu.”


Isaya38;1-20

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: