Hukumu dhidi ya Babuloni
1“Teremka uketi mavumbini
ewe Babuloni binti mzuri!
Keti chini pasipo kiti cha enzi
ewe binti wa Wakaldayo!
Tokea sasa hutaitwa tena mwororo wala nadhifu.
2Twaa mawe ya kusagia, usage unga kama mtumwa!
Vua utaji wako, ukavue na mavazi yako!
Pandishia vazi lako miguuni, ukavuke mito.
3Watu watauona uchi wako;
naam, wataiona aibu yako.
Mimi nitalipiza kisasi,
wala sitamhurumia yeyote.”
4Mkombozi wetu ndiye Mtakatifu wa Israeli;
Mwenyezi-Mungu wa majeshi ndilo jina lake.
5Mwenyezi-Mungu asema:
“Ewe taifa la Wakaldayo
lililo kama binti mzuri,
keti kimya na kutokomea gizani.
Maana umepoteza hadhi yako
ya kuwa bimkubwa wa falme.
6Niliwakasirikia watu wangu Israeli,
nikawafanya watu wangu kuwa haramu.
Niliwatia mikononi mwako,
nawe hukuwaonea huruma;
na wazee uliwatwisha nira nzito mno.
7Ulijisemea moyoni: ‘Nitakuwa malkia milele’,
nawe hukuyatafakari mambo yanayotokea,
wala kufikiri mwisho wake.
8 47:8-9 Taz Ufu 18:7-8 “Sasa, basi, sikiliza ewe mpenda anasa,
wewe unayedhani kuwa u salama,
na kujisemea: ‘Ni mimi tu,
na hakuna mwingine isipokuwa mimi.
Kamwe sitakuwa mjane,
wala sitafiwa na wanangu.’
9Haya yote mawili yatakupata,
ghafla, katika siku moja:
Kupoteza watoto wako na kuwa mjane,
ijapokuwa una wingi wa uchawi wako,
na nguvu nyingi za uganga wako.
10“Ulijiona salama katika uovu wako;
ukajisemea, ‘Hakuna mtu anayeniona.’
Hekima na elimu yako vilikupotosha,
ukajisemea moyoni mwako, ‘Mimi ndiye;
hakuna mwingine anayenishinda.’
11Lakini maafa yatakupata
ambayo hutaweza kujiepusha nayo.
Balaa litakukumba
ambalo hutaweza kulipinga;
maangamizi yatakujia ghafla
ambayo hujapata kamwe kuyaona.
12Endelea basi na uganga wako,
tegemea wingi wa uchawi wako.
Wewe uliyapania hayo tangu ujana wako
ukitumainia kwamba utafanikiwa
au kusababisha kitisho kwa watu!
13Wewe umejichosha bure na washauri wako.
Basi, na wajitokeze hao wanajimu wakuokoe!
Wao huzigawa mbingu sehemusehemu,
huzichunguza nyota
na kubashiri kila mwezi yatakayokupata.
14“Kumbuka, wao ni kama mabua makavu:
Moto utayateketezea mbali!
Hawawezi hata kujiokoa wenyewe
mbali na ukali wa moto huo.
Moto huo si wa kujipatia joto,
huo si moto wa kuota!
15Ndivyo watakavyokuwa hao uliowategemea hivyo,
hao uliojishughulisha nao tangu ujana wako.
Watatangatanga kila mmoja njia yake;
hakuna hata mmoja atakayeweza kukuokoa.”
Isaya47;1-15
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
No comments:
Post a Comment