Onyo dhidi ya ibada za sanamu
1Mtu mwadilifu akifa,
hakuna mtu anayejali;
mtu mwema akifariki,
hakuna mtu anayefikiri na kusema:
“Mtu huyo mwema ameondolewa asipatwe na maafa,
2ili apate kuingia kwenye amani.”
Watu wanaofuata njia ya haki,
watakuwa na amani na kupumzika.
3Lakini Mwenyezi-Mungu asema:
“Njoni hapa nyinyi wana wa wachawi;
nyinyi wazawa wa wachawi, wazinzi na malaya.
4Je, mnadhani mnamdhihaki nani?
Mnamfyonya nani na kumtolea ulimi?
Nyinyi wenyewe ni wahalifu tangu mwanzo,
nyinyi ni kizazi kidanganyifu.
5Nyinyi mnawaka tamaa kwenye miti ya mialoni,
na katika kila mti wa majani mabichi.
Mnawachinja watoto wenu
na kuwatambika katika mabonde na nyufa za majabali.
6Mnachagua mawe laini mabondeni,
na kuyafanya kitovu cha maisha yenu.
Mnayamiminia tambiko ya kinywaji
na kuyapelekea tambiko ya nafaka!
Je, mimi nitaridhishwa kwa vitu hivyo?
7Mmeweka vitanda vyenu juu ya milima mikubwa,
na kwenda huko kutoa tambiko.
8Nyuma ya milango na miimo
mmetundika kinyago chenu.
Nyinyi mnaniacha mimi
na kutandika na kuvipanua vitanda vyenu.
Mnafanya mapatano na hao mliopenda vitanda vyao.
Humo mnazitosheleza tamaa zenu mbaya,
huku mnakodolea macho kinyago chenu.57:8 huku … chenu: Maana katika Kiebrania si dhahiri.
9Mnajitia marashi na manukato kwa wingi
kisha mnakwenda kumwabudu Moleki.57:9 Moleki: Au Mfalme.
Mnawatuma wajumbe wenu huko na huko,
kujitafutia miungu ya kuabudu;
hata kuzimu walifika.
10Mlichoshwa na safari zenu ndefu,
hata hivyo hamkukata tamaa;
mlijipatia nguvu mpya,
ndiyo maana hamkuzimia.
11“Mlimwogopa na kutishwa na nani
hata mkasema uongo,
mkaacha kunikumbuka mimi
na kuacha kabisa kunifikiria?
Mimi sikuwaambia kitu kwa muda mrefu;
ndio maana labda mkaacha kuniheshimu!
12Mnafikiri mnafanya sawa,
lakini nitayafichua matendo yenu,
nayo miungu yenu haitawafaa kitu.
13Mtakapolia kuomba msaada,
rundo la vinyago vyenu na liwaokoe!
Upepo utavipeperushia mbali;
naam, pumzi itavitupilia mbali.
Lakini watakaokimbilia usalama kwangu,
wataimiliki nchi,
mlima wangu mtakatifu utakuwa mali yao.”
Huruma ya Mungu
14Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Jengeni! Jengeni! Tayarisheni njia!
Ondoeni vikwazo vyote njiani mwa watu wangu!”
15Hivi ndivyo asemavyo Mungu aliye juu kabisa,
aishiye milele na ambaye jina lake ni “Mtakatifu”:
“Mimi nakaa huko juu, mahali patakatifu,
nakaa pia na wenye majuto na wanyenyekevu.
Mimi nitawatia moyo walio wanyenyekevu
na kuwapa nguvu wenye majuto.
16Maana sitaendelea kuwalaumu
wala kuwakasirikia daima.
La sivyo hao niliowaumba watadhoofika mbele yangu,
nami ndiye niliyewapa pumzi yangu ya uhai.
17Niliwakasirikia kwa sababu ya uovu na tamaa zao;
niliwaadhibu, nikauficha uso wangu na kukasirika.
Lakini wao waliendelea kufuata njia zao wenyewe.
18Niliiona mienendo yao, lakini nitawaponya;
nitawaongoza na kuwapa faraja,
nitawatuliza hao wanaoomboleza.
19Mimi nitawapa amani,
amani kwa walio mbali na walio karibu!
Mimi nitawaponya.
20Lakini waovu ni kama bahari iliyochafuka,
ambayo haiwezi kutulia;
mawimbi yake hutupa tope na takataka.”
21Mungu wangu asema hivi:
“Watu waovu sitawapa amani.”
Isaya57;1-21
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
No comments:
Post a Comment