Ibada ya uongo na ya kweli
1Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Mbingu ni kiti changu cha enzi,
dunia ni kiti cha kuwekea miguu yangu.
Mtanijengea nyumba ya namna gani basi,
Mahali nitakapoweza kupumzika?
2Mimi mwenyewe nilivifanya vitu hivi vyote,
na hivi vyote ni mali yangu.
Lakini ninachojali mimi
ni mtu mnyenyekevu na mwenye majuto,
mtu anayetetemeka asikiapo neno langu.
3“Lakini watu hawa wanafanya wanavyotaka:
Wananitolea tambiko ya ng'ombe
na mara wanaua watu kutambikia.
Wananitolea sadaka ya mwanakondoo
na pia wanamvunja mbwa shingo.
Wananitolea tambiko ya nafaka
na pia kupeleka damu ya nguruwe.
Wanachoma ubani mbele yangu
na kwenda kuabudu miungu ya uongo.
Hao wamechagua kufuata njia zao wenyewe.
4Basi, nitawaletea taabu;
yatawapata yaleyale wanayoyahofia;
maana nilipoita hakuna aliyeitika,
niliponena hawakusikiliza.
Bali walifanya yaliyo maovu mbele yangu,
walichagua yale ambayo hayanipendezi.”
Adhabu na wokovu
5Sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu,
enyi msikiao neno lake mkatetemeka:
“Ndugu zenu ambao wanawachukia,
na kuwapiga marufuku kwa sababu yangu,
wamesema kwa dharau
‘Mungu na aoneshe utukufu wake,
nasi tuwaone nyinyi mkishinda!’
Lakini wao wenyewe ndio watakaoaibishwa!
6Sikilizeni, ghasia kutoka mjini,
sauti kutoka hekaluni!
Hiyo ni sauti ya Mwenyezi-Mungu
akiwaadhibu maadui zake!
7 66:7 Taz Ufu 12:5 “Mji wangu mtakatifu,
ni kama mama ajifunguaye bila kuona uchungu;
kabla uchungu kuanza, amekwisha zaa mtoto.
8Ni nani aliyepata kusikia jambo kama hilo?
Ni nani aliyewahi kuona jambo kama hilo?
Je, nchi nzima yaweza kuzaliwa siku moja?
Je, taifa zima laweza kuzaliwa mara moja?
Maana Siyoni, mara tu alipoanza kuona uchungu,
alijifungua watoto wake.
9Je, nitawatunza watu wangu mpaka karibu wazaliwe,
halafu niwazuie wasizaliwe?
Au mimi mwenye kuwajalia watoto,
nitafunga kizazi chao?
Mimi Mungu wenu nimesema.”
10Shangilieni na kufurahi pamoja na Yerusalemu enyi mnaoupenda!
Shangilieni pamoja nao enyi nyote mlioulilia!
11Kama mama, Yerusalemu utawanyonyesha,
nanyi mtashiba kwa riziki zake;
mtakunywa shibe yenu na kufurahi,
kutokana na wingi wa fahari yake.
12Maana Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Nitakuletea fanaka nyingi kama mto,
utajiri wa mataifa kama mto uliofurika.
Nanyi mtanyonya na kubebwa kama mtoto mchanga,
mtabembelezwa kama mtoto magotini mwa mama yake.
13Kama mama amtulizavyo mwanawe,
kadhalika nami nitawatuliza;
mtatulizwa mjini Yerusalemu.
14Mtayaona hayo na mioyo yenu itafurahi;
mifupa yenu itapata nguvu kama majani mabichi.
Hapo itajulikana kuwa mimi Mwenyezi-Mungu huwalinda watumishi wangu,
lakini nikikasirika huwaadhibu maadui zangu.”
15Mwenyezi-Mungu atakuja kama moto,
na magari yake ya vita ni kimbunga.
Ataiacha hasira yake ifanye kazi yake kwa ukali,
na onyo lake litekelezwe kwa miali ya moto.
16Mwenyezi-Mungu atatoa hukumu kwa moto,
atawaadhibu watu wote kwa upanga;
nao atakaowaangamiza watakuwa wengi.
17Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Wapo watu wanaojitakasa na kutawadha wapate kuingia kwenye bustani za ibada za sanamu; wanafanya maandamano na kuhani akiwa kati yao. Watu hao hula nguruwe, panya na vyakula vingine haramu. Watu hao hakika watakufa wote pamoja. 18Nayajua matendo yao na mawazo yao. Naja kuwakusanya watu wa mataifa yote na lugha zote, wajumuike pamoja na kuuona utukufu wangu. 19Nitaweka kati yao alama ya uwezo wangu. Watakaosalimika kati yao nitawapeleka kwa watu wa mataifa huko Tarshishi, Puti,66:19 Puti: Kiebrania: Puli. Ludi, nchi zenye wapiga upinde stadi; watakwenda pia Tubali na Yowani na nchi ambapo watu hawajapata kusikia umaarufu wangu wala kuuona utukufu wangu. Hao wajumbe wangu watautangaza utukufu wangu katika mataifa hayo. 20Watawarejesha ndugu zenu wote kutoka katika mataifa yote kama matoleo yangu mimi Mwenyezi-Mungu. Watawaleta wamepanda farasi, nyumbu, ngamia na magari ya farasi mpaka Yerusalemu, kwenye mlima wangu mtakatifu. Watawaleta kama Waisraeli waletavyo sadaka ya nafaka katika chombo safi hadi nyumbani kwangu mimi Mwenyezi-Mungu. 21Pia nitawachagua baadhi yao kuwa makuhani na baadhi yao kuwa Walawi. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
22“Kama vile mbingu mpya na dunia mpya nitakazoumba
zitakavyodumu milele kwa uwezo wangu,
ndivyo wazawa wako na jina lako litakavyodumu.
23Katika kila sikukuu ya mwezi mpya,
na katika kila siku ya Sabato,
binadamu wote watakuja kuniabudu.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
24“Kisha watakwenda kuziona maiti za wale walioniasi. Wadudu watakaowala hawatakufa, na moto utakaowachoma hautazimika kamwe. Watakuwa chukizo kwa watu wote.”
Isaya66;1-24
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
No comments:
Post a Comment