Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday, 2 December 2019

Kikombe Cha Asubuhi; Tunamshukuru Mungu kwa kumaliza Kitabu cha Isaya,Leo Tunaanza Kitabu cha Yeremia 1....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki/Mwezi
Mwingine tena Mungu wetu ametuchagua

na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....


Tunamshukuru Mungu kwa kutupa kibali cha

 kupitia kitabu cha "ISAYA
"
Ni matumaini yangu kuna mengi tumejifunza/kufaidika
na kutupa mwanga/kuelewa kwenye kitabu hiki...


Leo tunapokwenda anza kupitia Kitabu cha"YEREMIA"tunamuomba Mungu wetu akatupe kibali,macho ya rohoni
 na akili ya kuelewa katika kujifunza NENO lake...
Ee Mungu  tunaomba ukatuongoze...!!

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni
Neema yako yatutosha  Mungu wetu..!


Mafarisayo walisikia kwamba Yesu alikuwa anabatiza na kuwapata wanafunzi wengi kuliko Yohane. (Lakini ukweli ni kwamba Yesu hakuwa anabatiza ila wanafunzi wake.) Basi, Yesu aliposikia hayo, alitoka Yudea akarudi Galilaya; na katika safari hiyo ilimbidi apitie Samaria.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza
kuwasamehe wale wote waliotukosea,
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,

Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Basi, akafika Sukari, mji mmoja wa Samaria, karibu na shamba ambalo Yakobo alikuwa amempa mwanawe, Yosefu. Mahali hapo palikuwa na kisima cha Yakobo, naye Yesu, kutokana na uchovu wa safari, akaketi kando ya kisima. Ilikuwa yapata saa sita mchana.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Basi, mwanamke mmoja Msamaria akafika kuteka maji. Yesu akamwambia, “Nipatie maji ninywe.” (Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wamekwenda mjini kununua chakula.) Lakini huyo mwanamke akamwambia, “Wewe ni Myahudi; mimi ni mwanamke Msamaria! Unawezaje kuniomba maji?” (Wayahudi hawakuwa na ushirikiano na Wasamaria katika matumizi ya vitu).
Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....
Nawapenda.

1Yafuatayo ni maneno ya Yeremia mwana wa Hilkia, mmoja wa makuhani wa mji wa Anathothi, katika nchi ya Benyamini. 2Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia mnamo mwaka wa kumi na tatu wa utawala wa Yosia mwana wa Amoni, mfalme wa Yuda. 3Lilimjia tena wakati Yehoyakimu mwana wa Yosia, alipokuwa mfalme wa Yuda. Yeremia aliendelea kupata neno la Mwenyezi-Mungu hadi mwishoni mwa mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Sedekia mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda. Mnamo mwezi wa tano wa mwaka huo, watu wa Yerusalemu walipelekwa uhamishoni.
Yeremia anaitwa kuwa nabii
4Mwenyezi-Mungu aliniambia neno lake:
5“Kabla hujachukuliwa mimba, mimi nilikujua,
kabla hujazaliwa, mimi nilikuweka wakfu;
nilikuteua uwe nabii kwa mataifa.”
6Nami nikajibu, Aa! Bwana Mwenyezi-Mungu,
mimi sijui kusema, kwa kuwa bado ningali kijana.
7Lakini Mwenyezi-Mungu akaniambia,
“Usiseme kwamba wewe ni kijana bado.
Utakwenda kwa watu wote nitakaokutuma kwao,
na yote nitakayokuamuru utayasema.
8Wewe usiwaogope watu hao,
kwa maana niko pamoja nawe kukulinda.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
9Kisha Mwenyezi-Mungu akaunyosha mkono wake, akagusa kinywa changu, akaniambia,
“Tazama nimeyatia maneno yangu kinywani mwako.
10Leo nimekupa mamlaka juu ya mataifa na falme,
uwe na mamlaka ya kungoa na kubomoa,
mamlaka ya kuharibu na kuangamiza,
mamlaka ya kujenga na ya kupanda.”
Maono mawili
11Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Yeremia, unaona nini?” Nami nikasema, “Ninaona tawi la mlozi1:11 mlozi: Mti wa kwanza kuchanua baada ya mvua nchini Palestina; aidha hapa tunapewa picha ya mti ambao ulikuwa “macho” tayari kuchanua mara baada ya mvua. unaochanua.” 12Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Umeona vizuri, maana niko macho kulitekeleza neno langu.”
13Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia mara ya pili: “Unaona nini?” Nami nikasema, “Ninaona chungu kinatokota kimeinama upande wangu kutoka kaskazini.”
14Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Maangamizi yataanzia kutoka kaskazini na kuwapata wakazi wote wa nchi hii. 15Maana naziita falme zote za kaskazini na makabila yote. Wafalme wake wote watakuja na kila mmoja wao ataweka kiti chake cha enzi mbele ya malango ya Yerusalemu na kandokando ya kuta zake zote, na kuizunguka miji yote ya Yuda. 16Nami nitawahukumu Waisraeli kwa ajili ya uovu wao wote wa kuniacha mimi, wakafukizia ubani miungu mingine na kuabudu sanamu walizojitengenezea wenyewe. 17Sasa basi, wewe Yeremia jiweke tayari. Haya! Nenda ukawaambie mambo yote ninayokuamuru. Usiwaogope, nisije nikakufanya mwoga mbele yao. 18Leo hii nakufanya kuwa imara kama mji uliozungukwa na ngome, kama mnara wa chuma na kama ukuta wa shaba nyeusi, dhidi ya nchi yote, dhidi ya wafalme wa Yuda, wakuu wake, makuhani wake na watu wake wote. 19Watapigana nawe, lakini hawatashinda kwa sababu mimi niko pamoja nawe kukuokoa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”


Yeremia1;1-19

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: