Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday, 24 December 2019

Kikombe Cha Asubuhi; Yeremia 17....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu



Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..!

Baada ya ndugu zake kwenda kwenye sikukuu, Yesu naye alikwenda, lakini hakuenda kwa hadhara bali kwa siri. Viongozi wa Wayahudi walikuwa wanamtafuta kwenye sikukuu hiyo; wakauliza, “Yuko wapi?”
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Kulikuwa na minongono mingi katika umati wa watu. Baadhi yao walisema, “Ni mtu mwema.” Wengine walisema, “La! Anawapotosha watu.” Hata hivyo hakuna mtu aliyethubutu kusema habari zake hadharani kwa kuwaogopa viongozi wa Wayahudi.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Sikukuu hiyo ilipofikia katikati, Yesu naye alikwenda hekaluni, akaanza kufundisha. Basi, Wayahudi wakashangaa na kusema, “Mtu huyu amepataje elimu naye hakusoma shuleni?” Hapo Yesu akawajibu, “Mafundisho ninayofundisha si yangu, bali ni yake yeye aliyenituma.
Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.


Dhambi na adhabu ya Yuda
1“Dhambi ya watu wa Yuda, imeandikwa kwa kalamu ya chuma; kwa ncha ya almasi imechorwa mioyoni mwao na katika pembe za madhabahu zao, 2wakati watu wake wanakumbuka madhabahu zao na sanamu za mungu wa kike, Ashera, zilizowekwa kando ya miti mibichi juu ya vilele vya vilima, 3na juu ya milima katika sehemu tambarare. Mali yenu na hazina zenu zote nitazitoa zitekwe nyara kulipia dhambi zenu mlizotenda17:3 kulipia dhambi zenu mlizotenda: Kiebrania: Mahali penu pa juu kwa ajili ya dhambi. kila mahali nchini mwenu. 4Itawabidi muiachilie17:4 muiachilie: Kiebrania si dhahiri. hiyo nchi yenu niliyowapeni, nami nitawafanya muwatumikie maadui zenu katika nchi msiyoijua, kwa sababu hasira yangu imewaka moto usiozimika milele.”
Misemo mbalimbali
5Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Alaaniwe mtu anayemtegemea binadamu,
mtu ambaye anategemea nguvu za binadamu,
mtu ambaye moyo wake umeniacha mimi Mwenyezi-Mungu.
6Huyo ni kama kichaka jangwani,
hataona chochote chema kikimjia.
Ataishi mahali pakavu nyikani,
katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu.
7“Abarikiwe mtu anayemtegemea Mwenyezi-Mungu,
mtu ambaye Mwenyezi-Mungu ndiye tegemeo lake.
8Huyo ni kama mti uliopandwa kando ya maji,
upenyezao mizizi yake karibu na chemchemi.
Hauogopi wakati wa joto ufikapo,
majani yake hubaki mabichi.
Hauhangaiki katika mwaka wa ukame,
na hautaacha kuzaa matunda.
9“Moyo wa mtu ni mdanganyifu kuliko vitu vyote;
hauwezi kuponywa, hakuna awezaye kuuelewa!
10Mimi Mwenyezi-Mungu hupima akili
na kuchunguza mpaka ndani ya moyo wa mtu.
Na hivyo humtendea kila mmoja,
kulingana na mwenendo wake,
kadiri ya matendo yake.”
11Mtu apataye mali isiyo halali
ni kama kware akusanyaye makinda ambayo hakuyaangua:
Wakati wa kilele cha ujana wake itamchopoka,
na mwishoni atakuwa mtu mpumbavu.
12Kuna kiti cha enzi kitukufu
kiti kilichoinuliwa juu;
huko ndiko mahali petu patakatifu.
13Ee Mwenyezi-Mungu tumaini la Israeli,
wote wanaokukataa wataaibishwa;
wanaokuacha wewe watatoweka,
kama majina yaliyoandikwa vumbini,17:13 kwa majina yaliyoandikwa vumbini: Au watatowekea kuzimu.
kwa maana wamekuacha wewe Mwenyezi-Mungu,
uliye chemchemi ya maji ya uhai.
Sala ya Yeremia
14Uniponye, ee Mwenyezi-Mungu, nami nitapona;
uniokoe, nami nitaokoka;
maana, wewe ndiwe sifa yangu.
15Tazama watu wanavyoniambia:
“Jambo alilotishia Mwenyezi-Mungu liko wapi?
Acha basi lije!”
16Sikuikimbia huduma yako ya kuwa mchungaji
wala sikutamani ile siku ya maafa ije.
Wewe mwenyewe wajua nilichosema kwa mdomo wangu,
nilichotamka wakijua waziwazi.
17Usiwe tisho kwangu;
wewe ndiwe kimbilio langu siku ya maafa.
18Waaibishwe wale wanaonitesa,
lakini mimi usiniache niaibike.
Wafedheheshwe watu hao,
lakini mimi usiniache nifedheheke.
Uwaletee siku ya maafa,
waangamize kwa maangamizi maradufu!
Kuadhimisha Sabato
19Mwenyezi-Mungu aliniambia hivi: “Nenda ukasimame penye lango la watu ambapo wafalme wa Yuda huingia na kutoka mjini, na katika malango mengine yote ya Yerusalemu useme: 20Sikieni neno la Mwenyezi-Mungu enyi wafalme wa Yuda, nanyi watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu ambao huingia kwa kupitia malango haya. 21Waambie kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kwa usalama wa maisha yenu, muwe na hadhari msije mkabeba mzigo siku ya Sabato, au kuingiza mzigo mjini kupitia malango ya Yerusalemu. 22Msibebe mzigo kutoka majumbani mwenu siku ya Sabato wala kufanya kazi. Iadhimisheni siku ya Sabato kama siku takatifu kama nilivyowaamuru wazee wenu. 23Lakini wazee wenu hawakunisikiliza wala kujali, bali walivifanya vichwa vyao kuwa vigumu, wakakataa kusikia na kufuata maagizo yangu.
24“Lakini mkinisikiliza mimi Mwenyezi-Mungu, mkaacha kuingiza mzigo wowote kupitia malango ya mji huu siku ya Sabato, wala kufanya kazi siku hiyo, 25basi, wafalme na wana wa wafalme wanaomfuata mfalme Daudi katika utawala, pamoja na watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu, wataingia kwa kupitia malango ya mji huu, wakiwa wamepanda farasi na magari ya farasi. Nao mji huu utakuwa na watu daima. 26Watu watakuja kutoka miji ya Yuda na maeneo ya kandokando ya Yerusalemu, kutoka nchi ya Benyamini, kutoka Shefela,17:26 Shefela: Maana yake nchi ya mabonde. kutoka nchi ya milima na kutoka Negebu, wakileta sadaka za kuteketezwa na tambiko, sadaka za nafaka na ubani wa harufu nzuri, pamoja na matoleo ya shukrani. Vyote hivyo watavileta katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 27Lakini msiponisikiliza na kuiadhimisha siku ya Sabato kama siku takatifu, msipoacha kubeba mizigo na kuingia nayo kupitia malango ya Yerusalemu siku ya Sabato, basi, nitawasha moto katika malango yake, nao utayateketeza majumba yote ya fahari ya Yerusalemu nao hautazimwa kamwe.”


Yeremia17;1-27

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: