Mungu awalinda Waisraeli
1Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: 2“Nenda ukawatangazie waziwazi wakazi wote wa Yerusalemu kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi:
Naukumbuka uaminifu wako ulipokuwa kijana,
jinsi ulivyonipenda kama mchumba wako,
ulivyonifuata jangwani
kwenye nchi ambayo haikupandwa kitu.
3Israeli, wewe ulikuwa mtakatifu kwangu,
ulikuwa matunda ya kwanza ya mavuno yangu.
Wote waliokudhuru walikuwa na hatia,
wakapatwa na maafa.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Dhambi ya wazee wa Israeli
4Sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu, enyi wazawa wa Yakobo. Sikilizeni enyi jamaa zote za wazawa wa Israeli.
5Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Wazee wenu waliona kosa gani kwangu
hata wakanigeuka na kuniacha,
wakakimbilia miungu duni,
hata nao wakawa watu duni?
6Hawakujiuliza:
‘Yuko wapi Mwenyezi-Mungu aliyetutoa nchini Misri,
aliyetuongoza nyikani
katika nchi ya jangwa na makorongo,
nchi kame na yenye giza nene,
nchi isiyopitiwa na mtu yeyote,
wala kukaliwa na binadamu?’
7Niliwaleta katika nchi yenye rutuba,
muyafurahie mazao yake na mema yake mengine.
Lakini mlipofika tu mliichafua nchi yangu,
mkaifanya chukizo nchi niliyowapa iwe yenu.
8Nao makuhani hawakujiuliza: ‘Yuko wapi Mwenyezi-Mungu?’
Wataalamu wa sheria hawakunijua,
viongozi2:8 viongozi: Kiebrania: Wachungaji. wa watu waliniasi;
manabii nao walitabiri kwa jina la Baali
na kuabudu sanamu zisizo na faida yoyote.”
Mashtaka ya Mwenyezi-Mungu dhidi ya watu wake
9Mwenyezi-Mungu asema,
“Kwa hiyo, mimi nitawalaumu nyinyi,
na nitawalaumu wazawa wenu.
10Haya, vukeni bahari hadi Kupro2:10 Kupro: Au Mwambao wa nchi za Ugiriki na Italia. mkaone,
au tumeni watu huko Kedari2:10 Kedari: Makazi ya Mabedui katika jangwa la Suria na Arabia. wakachunguze,
kama jambo kama hili limewahi kutokea:
11Kwamba kuna taifa lililowahi kubadilisha miungu yake
ingawa miungu hiyo si miungu!
Lakini watu wangu wameniacha mimi, utukufu wao,
wakafuata miungu isiyofaa kitu.
12Shangaeni enyi mbingu, juu ya jambo hili,
mkastaajabu na kufadhaika kabisa.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
13Maana, watu wangu wametenda maovu mawili;
wameniacha mimi niliye chemchemi ya maji ya uhai,
wakajichimbia visima vyao wenyewe,
visima vyenye nyufa, visivyoweza kuhifadhi maji.
Matokeo ya utovu wa imani ya Israeli
14“Je, Israeli ni mtumwa,
ama amezaliwa utumwani?
Mbona basi amekuwa kama mawindo?
15Simba wanamngurumia,
wananguruma kwa sauti kubwa.
Nchi yake wameifanya jangwa,
miji yake imekuwa magofu, haina watu.
16Isitoshe, watu wa Memfisi na Tahpanesi,
wameuvunja utosi wake.2:16 wameuvunja … wake: Kitendo kinachomaanisha angamizo kubwa.
17Israeli, je, hayo yote si umejiletea mwenyewe,
kwa kuniacha mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako,
niliyekuwa ninakuongoza njiani?
18Na sasa itakufaa nini kwenda Misri,
kunywa maji ya mto Nili?
Au itakufaa nini kwenda Ashuru,
kunywa maji ya mto Eufrate?
19Uovu wako utakuadhibu;
na uasi wako utakuhukumu.
Ujue na kutambua kuwa ni vibaya mno
kuniacha mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako,
na kuondoa uchaji wangu ndani yako.
Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimesema.
Israeli yakataa kumwabudu Mwenyezi-Mungu
20“Tangu zamani wewe ulivunja nira yako,
ukaikatilia mbali minyororo yako,
ukasema, ‘Sitakutumikia’.
Juu ya kila kilima kirefu
na chini ya kila mti wa majani mabichi,
uliinamia miungu ya rutuba kama kahaba.2:20 Katika Israeli kuabudu miungu mingine kulifananishwa na ukahaba.
21Lakini mimi nilikupanda kama mzabibu mteule,
mzabibu wenye afya na wa mbegu safi;
mbona basi umeharibika,
ukageuka kuwa mzabibu mwitu?
22Hata ukijiosha kwa magadi,
na kutumia sabuni nyingi,
madoa ya uovu wako bado yatabaki mbele yangu.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
23“Unawezaje kusema, ‘Mimi si najisi;
sijawafuata Mabaali?’
Tazama ulivyotenda dhambi kule bondeni;
angalia ulivyofanya huko!
Wewe ni kama mtamba wa ngamia,
akimbiaye huko na huko;
24kama pundamwitu aliyezoea jangwani.
Katika tamaa yake hunusanusa upepo;
nani awezaye kuizuia hamu yake?
Amtakaye hana haja ya kujisumbua;
wakati wake ufikapo watampata tu.
25Israeli, usiichakaze miguu yako
wala usilikaushe koo lako.
Lakini wewe wasema: ‘Hakuna tumaini lolote.
Nimeipenda miungu ya kigeni,
hiyo ndiyo nitakayoifuata.’
Israeli astahili kuadhibiwa
26“Kama vile mwizi aonavyo aibu akishikwa,
ndivyo Waisraeli watakavyoona aibu;
wao wenyewe, wafalme wao, wakuu wao,
makuhani wao na manabii wao.
27Hao huuambia mti: ‘Wewe u baba yangu,’
na jiwe: ‘Wewe ndiwe uliyenizaa;’
kwa maana wamenipa kisogo,
wala hawakunielekezea nyuso zao.
Lakini wakati wa shida husema: ‘Inuka utuokoe!’
28“Lakini iko wapi miungu yako uliyojifanyia?
Iinuke basi, kama inaweza kukusaidia,
wakati unapokuwa katika shida.
Ee Yuda, idadi ya miungu yako
ni sawa na idadi ya miji yako!
29Mbona mnanilalamikia?
Nyinyi nyote mmeniasi.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
30Niliwaadhibu watu wako bila kufanikiwa,
wao wenyewe walikataa kukosolewa.
Upanga wako uliwamaliza manabii wako
kama simba mwenye uchu.
31Enyi watu! Sikilizeni ninachosema mimi Mwenyezi-Mungu:
Je, nimekuwa jangwa kwa Israeli
au nchi yenye giza nene?
Kwa nini basi watu wangu waseme:
‘Sisi tu watu huru;
hatutakuja kwako tena!’
32Kijana msichana aweza kusahau mapambo yake
au bibi arusi mavazi yake?
Lakini watu wangu wamenisahau
kwa muda wa siku zisizohesabika.
33Kweli wewe ni bingwa wa kutafuta wapenzi!
Hata wanawake wabaya huwafundisha njia zako.
34Nguo zako zina damu ya maskini wasio na hatia,
japo hukuwakuta wakivunja nyumba yako.
“Lakini licha ya hayo yote,
35wewe wasema: ‘Mimi sina hatia;
hakika hasira yake imegeuka mbali nami.’
Lakini mimi nitakuhukumu kwa sababu unasema:
‘Sikutenda dhambi.’
36Kwa nini unajirahisisha hivi,
ukibadilibadili mwenendo wako?
Utaaibishwa na Misri,
kama ulivyoaibishwa na Ashuru.
37Na huko pia utatoka,
mikono kichwani kwa aibu.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimewakataa wale uliowategemea,
wala hutafanikiwa kwa msaada wao.
Yeremia2;1-37
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
No comments:
Post a Comment