Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday, 31 December 2019

Kikombe Cha Asubuhi; Yeremia 22....

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu



Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..!


Kisha wale walinzi wakarudi kwa makuhani wakuu na Mafarisayo; nao wakawauliza, “Kwa nini hamkumleta?” Walinzi wakawajibu, “Hakuna mtu aliyepata kamwe kusema kama asemavyo mtu huyu!” Mafarisayo wakawauliza, “Je, nanyi pia mmedanganyika? Je, mmekwisha kumwona hata mmoja wa viongozi wa watu, au mmoja wa Mafarisayo aliyemwamini?
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Lakini umati huu haujui sheria ya Mose; umelaaniwa!” Mmoja wao alikuwa Nikodemo ambaye hapo awali alikuwa amemwendea Yesu. Basi, yeye akawaambia, “Je, sheria yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza na kujua anafanya nini?”
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Nao wakamjibu, “Je, wewe pia umetoka Galilaya? Haya, kayachunguze Maandiko Matakatifu nawe utaona kwamba Galilaya hakutoki kamwe nabii!” [ Basi, wote wakaondoka, kila mtu akaenda nyumbani;
Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.


Ujumbe juu ya jumba la kifalme la Yuda
1Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nenda katika ikulu ya mfalme wa Yuda, uwape watu ujumbe huu: 2Wewe mfalme wa Yuda unayekikalia kiti cha enzi cha mfalme Daudi, pamoja na watumishi wako na watu wako wanaopita katika malango haya, sikilizeni neno langu mimi Mwenyezi-Mungu. 3Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Tendeni mambo ya haki na uadilifu. Mwokoeni mikononi mwa mdhalimu mtu yeyote aliyenyanganywa mali zake. Msiwatendee vibaya au ukatili wageni, yatima na wajane wala msimwage damu ya mtu asiye na hatia mahali hapa. 4Kama mkishika neno hili nililowaambia basi, wafalme wanaokikalia kiti cha enzi cha Daudi wataendelea kuingia kwa kupitia malango ya ikulu hii. Watapita pamoja na watumishi wao na watu wao, wakiwa wamepanda farasi na magari ya farasi. 5Lakini kama hamtatii maneno haya, mimi Mwenyezi-Mungu naapa kwa nafsi yangu kwamba mahali hapa patakuwa magofu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
6Mwenyezi-Mungu asema hivi kuhusu ikulu ya mfalme wa Yuda:
“Ingawa waonekana kuwa mzuri kama nchi ya Gileadi
kama kilele cha Lebanoni,
Lakini naapa kuwa nitakufanya uwe jangwa,
uwe mji usiokaliwa na watu.
7Nitawatayarisha waangamizi dhidi yako,
kila mmoja na silaha yake mkononi.
Wataikata mierezi yako mizuri,
na kuitumbukiza motoni.
8“Kisha watu wengi wa mataifa watapita karibu na mji huu, na kila mmoja atamwuliza mwenzake: ‘Kwa nini Mwenyezi-Mungu ameutenda hivi mji huu mkubwa?’ 9Wenzao watawajibu, ‘Ni kwa sababu waliliacha agano la Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, wakaiabudu miungu mingine na kuitumikia.’”
Ujumbe juu ya Shalumu
10Msimlilie mtu aliyekufa,
wala msiombolezee kifo chake.
Bali mlilieni kwa uchungu yule aendaye mbali,
kwa kuwa hatarudi tena kuiona nchi yake.
11Maana, Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya Shalumu mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, aliyetawala baada ya Yosia baba yake, na ambaye aliondoka mahali hapa: “Shalumu hatarudi tena mahali hapa, 12bali atafia hukohuko walikomchukua utumwani. Kamwe hataiona tena nchi hii.
Ujumbe juu ya Yehoyakimu
13“Ole wako Yehoyakimu
wewe unayejenga nyumba kwa dhuluma
na kuiwekea ghorofa bila kutumia haki.
Unawaajiri watu wakutumikie bure
wala huwalipi mishahara yao.
14Wewe wasema:
‘Nitalijenga jumba kubwa,
lenye vyumba vikubwa ghorofani.’
Kisha huifanyia madirisha,
ukafunika kuta zake kwa mbao za mierezi,
na kuipaka rangi nyekundu!
15Unadhani umekuwa mfalme
kwa kushindana kujenga kwa mierezi?
Baba yako alikula na kunywa,
akatenda mambo ya haki na mema
ndipo mambo yake yakamwendea vema.
16Aliwapatia haki maskini na wahitaji,
na mambo yake yakamwendea vema.
Hii ndiyo maana ya kunijua mimi Mwenyezi-Mungu.
17Lakini macho yako wewe na moyo wako,
hungangania tu mapato yasiyo halali.
Unamwaga damu ya wasio na hatia,
na kuwatendea watu dhuluma na ukatili.
18“Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi juu ya Yehoyakimu mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda:
Wakati atakapokufa,
hakuna atakayemwombolezea akisema,
‘Ole, kaka yangu!’
‘Ole, dada yangu!’
Hakuna atakayemlilia akisema,
‘Maskini, bwana wangu!’
‘Maskini, mfalme wangu!’
19Atazikwa bila heshima kama punda,
ataburutwa na kutupiliwa mbali,
nje ya malango ya Yerusalemu.”
Maafa yatakayoipata Yerusalemu
20Enyi watu wa Yerusalemu,
pandeni Lebanoni mpige kelele,
pazeni sauti zenu huko Bashani;
lieni kutoka milima ya Abarimu,
maana wapenzi wenu wote wameangamizwa.
21Mwenyezi-Mungu aliongea nanyi mlipokuwa na fanaka,
lakini nyinyi mkasema, “Hatutasikiliza.”
Hii ndiyo tabia yenu tangu ujana wenu,
hamjapata kuitii sauti ya Mwenyezi-Mungu.
22Viongozi wenu watapeperushwa na upepo,
wapenzi wenu watachukuliwa uhamishoni.
Ndipo mtakapoona haya na kufadhaika,
kwa sababu ya uovu wenu wote mliotenda.
23Enyi wakazi wote wa Lebanoni,
nyinyi mkaao salama kati ya mierezi;
jinsi gani mtakavyopiga kite uchungu utakapowakumba,
uchungu kama wa mama anayejifungua!
Hukumu ya Mungu juu ya Konia
24Na kuhusu Konia mfalme wa Yuda, mwanawe Yehoyakimu, Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Naapa kwa nafsi yangu mimi Mwenyezi-Mungu kwamba hata kama wewe Konia mwana wa Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, ungekuwa pete yangu ya mhuri katika mkono wangu wa kulia, ningekuvulia mbali. 25Nitakutia mikononi mwa wale wanaotaka kuyamaliza maisha yako; naam, mikononi mwa wale unaowaogopa, mikononi mwa Nebukadneza, mfalme wa Babuloni; naam, mikononi mwa Wakaldayo. 26Nitakufukuzia mbali katika nchi ya kigeni, wewe pamoja na mama yako mzazi. Mtakuwa watumwa katika nchi hiyo ambamo nyote wawili hamkuzaliwa, nanyi mtafia hukohuko. 27Mtatamani kwa hamu kubwa kurudi katika nchi hii, lakini hamtarudi kamwe.
28Je, huyu mtu Konia,
amekuwa kama chungu kilichovunjika,
ambacho hudharauliwa na kutupwa nje?
Kwa nini yeye na watoto wake wametupwa mbali
wakatupwa katika nchi wasiyoijua?
29Ee nchi, ee nchi, ee nchi!
Sikia neno la Mwenyezi-Mungu!
30Mwenyezi-Mungu asema hivi:
Mwandike mtu huyu kwamba hana watoto,
mtu ambaye hatafanikiwa maishani mwake.
Maana hakuna hata mmoja wa wazawa wake
atakayekikalia kiti cha enzi cha Daudi
na kutawala tena katika Yuda.


Yeremia22;1-30

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: